Ni vigumu waziri mkuu kuwa rais?


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 01 February 2012

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli

HISTORIA ya uongozi nchini inaonyesha kwamba si rahisi kwa kiongozi yeyote, ukimwacha Mwalimu Julius Nyerere, aliyewahi kuwa Waziri Mkuu kisha baadaye akafanikiwa kuwa rais. Imethibitika hivyo na mifano ipo.

Hata upande wa Zanzibar , hakuna mtu yeyote aliyewahi kuwa Waziri Kiongozi baadaye akachanga vizuri karata zake na akaja kupitishwa kuwania kiti cha urais. Mifano ipo.

Hiki ndicho, kinamtisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na kumfanya ajiengue mapema kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Pinda hataki kuendeleza historia hiyo ya kukataliwa tena baada ya jina lake kuchafuliwa sana kutokana na siasa za chuki na kuumbuana.

Mara baada ya kupata uhuru kutoka kwa Mwingereza mwaka 1961, Mwalimu Nyerere aliteuliwa Waziri Mkuu wa kwanza lakini miezi michache baadaye akijua ugumu wa nafasi hiyo, alijiuzulu na kumwachia mpambanaji “Simba wa Vita’, Rashid Mfaume Kawawa.

Baada ya kujijenga kwa wananchi na hasa ilipofanyiwa marekebisho katiba ya nchi kuwa na cheo cha rais, Mwalimu Nyerere alirejea na kutawala kwa miaka 25 hadi alipostaafu mwaka 1985. Kawawa ndiye alikuwa anapewa nafasi ya kupendekeza mgombea urais hivyo haikuwa rahisi kujipendekeza.

Miaka ya kuelekea uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani mwaka 1985, kulikuwa na uvumi kwamba Mwalimu Nyerere alikuwa anamwandaa Waziri Mkuu, Edward Sokoine (1977 – 1980 na 1983 – 1984) kurithi mikoba yake.

Loo, ajali mbaya ya gari ilichukua maisha ya Sokoine 12 Aprili 1984 na kuacha msiba mkubwa. Alhaji Ali Hassan Mwinyi alichaguliwa kuwa rais (1985 – 1995).

Kwa kuwa mwaka 1992 ulirejeshwa mfumo wa vyama vingi, Watanzania walishuhudia, kwa mara ya kwanza, orodha ndefu ya wagombea urais kutoka ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na vyama vya upinzani. Miongoni mwa waliojitosa ni waliopata kuwa mawaziri wakuu.

John Samuel Malecela (Waziri Mkuu 1990 – 1994), na ambaye mwaka 1985 aliteuliwa kuwa mtu mashuhuri katika nchi za Jumuiya ya Madola alipambana na akina Cleopa David Msuya (1980 – 1983 na 1994 – 1995), na Joseph Sinde Warioba (1985 – 1990).

Wengine waliojitokeza walikuwa Katibu Mkuu, Horace Kolimba, Tuntemeke Sanga, Prof. Kighoma Malima, Njelu Kasaka, Benjamin Mkapa, Pius Msekwa, Edward Lowassa, Jakaya Kikwete, Mark Bomani, Rose Lugendo na Fred Rutakyamirwa.

Warioba aliwahi kukataa katakata kuwania nafasi hiyo ya juu katika uongozi wa nchi, lakini baadaye alitangaza kujaribu kina cha maji.

Mwalimu Nyerere alishinikiza Malecela na Kolimba waondolewe kwenye orodha kwa maelezo hawafai kupitia kitabu cha “Hatima ya Tanzania na Uongozi Wake”.

Aliyefanikiwa kufika nafasi ya juu kati ya mawaziri wakuu hao watatu ni Msuya aliyechuana na Kikwete na Mkapa aliyeshinda.

Mwaka 2005 Frederick Sumaye, baada ya miaka 10 ya uwaziri mkuu (1995 – 2005) alijiona ametenda mema yatakayowashawishi wajumbe ateuliwe kuendeleza kazi ya bosi wake Mkapa. Alijitokeza kupambana pamoja na wagombea wengine, mwanadiplomasia wa siku nyingi na waziri mkuu mwenzake Dk. Salm Ahmed Salim (1984 – 1985).

Jina la Sumaye lilipitishwa na Kamati Kuu kwenda Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ambako liliishia huku jina la Dk. Ahmed Salim likipelekwa kwenye Mkutano Mkuu pamoja na Prof Mark Mwandosya na Kikwete aliyeshinda.

Baada ya Mwalimu Nyerere kufariki dunia Malecela alidhani kikwazo kimeondoka, akajaribu mara ya pili mwaka 2005. Balaa! Jina lake liliishia Kamati Kuu.

Japokuwa kila mmoja amezaliwa na mvuto na bahati yake, matukio haya yatamfanya kila aliye makini kufikiri mara mbili.

Hali iko hivyo hata Zanzibar . Mwanasiasa machachari Maalim Seif Sharrif Hamad aliyekulia kwenye siasa za mizengwe, aliombwa mwaka 1985 amwachie nafasi Mzee Idriss Abdul Wakil.

Hamad aliyekuwa waziri kiongozi kuanzia 1984 hadi 1988 hakukubaliana nao akachuana naye. Hakushinda.

Baadaye siasa za visa na chuki zilimsukuma mwanasiasa huyo shupavu nje ya CCM akaangukia Chama cha Wananchi (CUF).

Hata alipogombea mfululizo kuanzia mwaka 1995, 2000 na 2010 kupitia CUF, “hakushinda” kwa macho ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar, na baada ya uchaguzi wa mwaka 2010 ‘akapewa’ nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inayoendeshwa kwa mfumo wa Umoja wa Kitaifa.

Mwaka 2000, Dk. Mohammed Gharib Bilal alijitosa katika kinyanganyiro cha kurithi mikoba ya Rais wa awamu ya tano wa Zanzibar , Dk. Salimn Amour. Kama ilivyokuwa kwa watangulizi wake hakufanikiwa, kwani alibwagwa kwenye ngazi ya NEC na Amani Karume aliyekuwa anamaliza muda wake.

Hatukupata fursa ya kujua ushawishi wa Dk. Omar Ali Juma, maana baada ya kuwa waziri kiongozi (1988 – 1995), mwaka 1995 aliteuliwa kuwa makamu wa rais. Aliteuliwa tena mwaka 2000 lakini akafariki dunia 2001.

Dk. Bilal alijaribu tena mwaka 2005, lakini jina lake liliishia Kamati Kuu kwa kile kinachoitwa “utamaduni wa CCM wa kumwachia rais aliyeko madarakani vipindi viwili”.

Mwaka 2010 alijitokeza tena, jina lake likafika NEC, lakini pamoja na Waziri Kiongozi aliyemaliza muda wake, Shamsi Vuai Nahodha waliangushwa vibaya na aliyekuwa Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohamed Shein aliyeshinda urais.

Pamoja na tishio la Wazanzibari kurejesha kadi za CCM kushinikiza Dk. Bilal apitishwe, aliambulia kupewa nafasi ya kumfuta machozi ya mgombea mwenza hivyo amekuwa Makamu wa Rais wa Tanzania .

Jambo jingine baya, mtu anayejitokeza kuwania nafasi ya urais huchafuliwa sana ama kwa kuibua ufisadi dhidi yake au kupakaziwa tu. Kashfa nyingi za ufisadi zimeibuka wakati huo na hata wengine kama Dk. Ahmed Salim mwaka 2005 wapinzani wake wakafikia kudai eti si raia na pia ana mizizi ya Hizbu.

Pinda, mwanasheria na mtu aliyetumikia serikali kwa miaka mingi anajua madhara ya kujitokeza kutangaza kuwania nafasi hiyo mapema. Lakini anaweza akatumia siasa za ‘sitaki-nataka’ kama alivyofanya Warioba kwa lengo la kukwepa mashambulizi kutoka kwa wapinzani wake ndani na nje ya CCM.

Waziri Mkuu, Pinda anajua kilichotokea kwa mtangulizi wake, Edward Lowasa. Hivi sasa ana kazi ya ziada siyo ya kujinadi, bali kujisafisha kwa kashfa iliyomkumba ya kufanikisha kampeni isiyo na uwezo wa Richmond kupewa zabuni ya kufua umeme wa dharura mwaka 2006.

Bunge liliunda kamati maalum ya kuchunguza kashfa hiyo na ripoti ilimshona sawasawa Lowasaa ambaye mwaka 2008 alipima tuhuma dhidi yake akajiuzulu. Rais Jakaya Kikwete akamteua Pinda.

Waziri mkuu kwa Tanzania na Waziri kiongozi upande wa Zanzibar ni nafasi ya mtendaji mkuu na msimamizi mkuu wa shughuli za serikali bungeni au Baraza la Wawakilishi.

Maswali. Kwanini wote hushindwa kupanda nafasi ya juu ya kuwa rais? Kwanini si chaguo la wengi ndani ya CCM?

0789 383 979
0
No votes yet