Ninaweza kuwa rais, rangi yangu si hoja

MWALIMU Haruna Ali Suleiman (56), anataka urais wa Zanzibar. Amechukua fomu kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Huyu ni mwalimu wa kusomea na amekulia katika wizara ya elimu Zanzibar hadi sasa ambako ni waziri wa elimu na mafunzo ya amali.
Haruna ni miongoni mwa wanachama 13 wa CCM ambao tayari wamejitokeza katika kinyang’anyiro cha urais Oktoba mwaka huu.
Kama kigezo cha kupata mgombea kitazingatia uwezo wa kiutawala, kurejesha umoja na mshikamano na kusimamia misingi ya serikali ya umoja wa kitaifa, basi Haruna Ali Suleimani anasema anazo sifa za kufikiriwa na kuteuliwa kuwa mgombea urais Zanzibar.
Katika mahojiano yake na MwanaHALISI wiki hii, nyumbani kwake Makunduchi, Unguja, Haruna anasema, “Nipimwe kwa yale niliyoyatenda na kuyasimamia. Ni mengi na ndio ushahidi mwanana.”
Anasema, “Nisipimwe kwa rangi yangu au asili ya wazazi wangu. Nipimwe kwa yale niliyoyatenda na kuyasimamia tangu nikiwa mwalimu, naibu mkurugenzi, naibu katibu mkuu na sasa waziri. Huko ndiko kuangaliwe.”
Akiongea kwa upole, lakini kwa sauti ya kufundisha na kujiamini, Haruna anasema, “Mimi ni Mzanzibari. Ni Mtanzania. Nimezaliwa hapa na nimekulia hapa. Hata masomo yangu nimeyapata hapa. ”
Anahoji, “Kosa langu ni kuzaliwa hivi? Ni kosa mimi kuwa mhindi? Nifanyeje sasa, maana sina uwezo wa kujibadilisha. Nisichaguliwe au kupitishwa kwa sababu ya asili yangu? Mimi ni mwana Afro Shirazi – chama cha Afro Shirazi Party (ASP) kilichoasisi Mapinduzi ya Zanzibar.”
Anasema, “Nadhani niangaliwe kwa mengine. Je, mimi ni Mtanzania na nina sifa za kuwa rais? Je, yale niliyokabidhiwa niliyatenda na kuyasimamia kwa uadilifu au nilitenda kinyume na yale niliyotakiwa kuyafanya? Huko ndiko kuangaliwe,” anasisitiza.”
Anasema kwa maoni yake, hayo ndiyo mambo ya kuzingatia katika kutafuta rais. Si vema wanaotafuta mgombea wakajikita katika mambo yanayoenezwa na wale wanaotafuta madaraka kwa nguvu. Hakutaja ni nani hasa wanatumia nguvu.
Kauli ya Haruna kutetea utaifa wake inakuja kufuatia hoja zinazoibuliwa na baadhi ya washindani wake, kwamba hastahili kupewa nafasi hiyo kwa kuwa yeye ana asili ya Asia.
Anasema yeye anajivunia utaifa wake, si rangi yake. Ameweza kuwa mwakilishi wa Makunduchi kwa miaka 10, mbunge wa Bunge la Muungano kupitia Baraza la Wawakilishi kwa miaka mitano na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC). Yote hayo “nimeyapata si kwa sababu ya rangi yangu, bali utaifa wangu.”
Haruna anahoji, “Uhindi huu wa sasa unakuja kwa kuwa nataka urais? Siwezi kuwa mhindi leo… Baadhi yao wanaonituhumu kwa rangi, ndiyo ninaofanya kazi nao katika chama na serikali.”
Anasema aliyeondolewa Zanzibar, ni mkoloni, si yeye. “Mimi sikuwa mkoloni. Mapinduzi ya mwaka 1964, ndiyo yaliyotukomboa mimi na wazazi wangu. Hakika, anayekutukana hakuchagilii tusi,” anasisitiza.
Haruna anasema, “Huu ni wakati wa kuaminiana. Nikifa leo, nitakufa nikiwa Mzanzibari na kwenye jeneza langu itapepea bendera ya serikali yangu na ile ya chama changu.”
Ukimuondoa Haruna wengine waliojitosa katika kinyang’anyiro cha kutaka kurithi rais wa sasa Amani Abeid Karume, ni makamu wa rais wa Jamhuri, Dk. Ali Mohammed Shein, waziri kiongozi, mstaafu Dk. Mohammed Gharib Billal na waziri kiongozi wa sasa, Shamsi Vuai Nahodha.
Wengine ni naibu waziri kiongozi, Ali Juma Shamhuna, Balozi wa Tanzania nchini Italia, Ali Karume, naibu waziri wa Afrika Mashariki, Mohammed Aboud, Mohammed Raza na aliyewahi kuwa katibu mkuu, Omari Sheha.
Anasema iwapo atabahatika kupitishwa na chama chake, atasimamia yale yote yaliyotendwa na serikali zilizopita, lakini mkazo mkubwa zaidi ukiwa ni umoja na mshikamano wa taifa.
Anasema serikali atakayoiunda, itasimamia ukusanyaji wa mapato na kutumia fedha za umma kwa kile alichoita “matumizi ya lazima.”
“Nitasimamia miundombinu hasa barabara, kilimo cha kale na kile cha kisasa. Nitahakikisha serikali inaboresha huduma za afya na kuimarisha sekta ya utalii na uvuvi. Nitakuwa na serikali ndogo, lakini yenye ufanisi,” anasema.
Mbali na kujivunia utaifa wake, Haruna anajivunia kuwa miongoni mwa mawaziri wa serikali ya Karume waliotimiza wajibu wao kikamilifu.
Anasema hakuna waziri mwingine, isipokuwa yeye, aliyekaa katika wizara hiyo kwa muda wa miaka 10; akatembelea shule zote – Unguja na Pemba; akajenga ushirikiano thabiti kati ya serikali na walimu na akafanikiwa kujenga ushirikiano kati ya wizara ya elimu Zanzibar na ile ya Bara.
“Ni mimi,” anasema na kuongeza, “niliyetetea serikali na chama changu. Niliyesimama kutetea maslahi ya walimu wangu na watumishi wengine katika wizara yangu. Nimesimamia urejeshwaji wa mfumo wa elimu kwa waliokosa,” anasimulia.
Anasema, “Nimeifufua maktaba ya taifa ambayo kwa miaka mingi ilisahaulika. Nimesimamia ujenzi wa vyuo viwili vya ufundi, Unguja na Pemba.”
Anasema, hapendi kutamba, lakini serikali atakayoiunda itakuwa mfano kwa nchi nyingine duniani.
“Nikiwa waziri wa elimu na utamaduni, kabla ya wizara hizo kutenganishwa, Zanzibar ilichukua kombe la Chalenji kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati kwa vijana wa miaka 17 na uanachama katika Shirikisho la Soka la Afrika (CAF),” anatamba kwa upande wa michezo.
Anasema alitenda yote haya kwa maslahi ya nchi yake na serikali aliyokuwa akiitumikia.
Haruna anasema kisiwani Pemba, ambako kumekuwa na mivutano ya muda mrefu ya kisiasa, serikali imefanikiwa kupeleka maendeleo kwa kujenga shule mpya za sekondari na za msingi. Moja ya shule hizo imeitwa jina lake.
Huyu ni mmoja wa mawaziri wa serikali ya Rais Karume waliofanya naye kazi kwa kipindi chote cha miaka 10 mbali na kuwa mtumishi na kiongozi kwa zaidi ya miaka 35. Yote haya anayaita ushindi wa kujivunia.
Haruna aliajiriwa serikalini mwaka 1976 akiwa mwalimu wa kawaida. Alipanda kutoka ngazi moja hadi nyingine hadi kufikia alipo sasa. Amekuwa naibu katibu mkuu kutoka 1995 hadi 2000.
Anasema aliingia katika ulingo wa siasa mwaka 2000 baada ya kuombwa na wazee wa nyumbani kwao, Makunduchi kugombea uwakilishi katika jimbo hilo. Ameoa na ana watoto watano.