Njama za kuiba kura hizi hapa


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 06 October 2010

Printer-friendly version
CCM imetuhumiwa kuchakachua matokeo ya uchaguzi mkuu

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimetwishwa tuhuma nzito za kuandaa mipango ya kuchakachua matokeo ya uchaguzi mkuu ili kionekane kimeshinda, MwanaHALISI inaweza kuripoti.

Taarifa zilizosambazwa kwa maandishi katika miji ya Dar es Salaam, Arusha, Moshi na Mwanza mwishoni mwa wiki iliyopita, zinadai kuwa CCM imefanikiwa kupenyeza wachakachuaji kura katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Maandishi hayo hayana saini na yamechapishwa kwenye karatasi za ukubwa wa A4.

Madai hayo yanaihusisha pia serikali na idara ya usalama wa taifa kwa kupeleka NEC watumishi kadhaa wenye ujuzi katika mawasiliano ya kompyuta (IT) ili kufanya maandalizi ya uchakachuaji matokeo ya uchaguzi.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa NEC, Rajab Kiravu ameliambia gazeti hili kuwa hawezi kutolea tamko hoja hii kwa madai kuwa alikuwa mkutanoni.

Gazeti lilikuwa limemuuliza iwapo anajua kuwa kuna maofisa wenye utaalam wa IT waliopelekwa NEC kwa lengo la kuchakachua matokeo ya uchaguzi kwa niaba ya CCM.

Alisema, “Niko kwenye kikao. Nikitoka hapa nakwenda Airport (Uwanja wa Ndege). Nakwenda Zanzibar. Nitafute Jumatano (leo) nikitoka Zanzibar.”

Nacho Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimekiri kupelekewa makaratasi hayo, mbali na nyaraka kutoka serikalini, NEC na idara ya usalama wa taifa zinazoonyesha kuwapo kwa mpango huo.

Akiongea na gazeti hili kwa njia ya simu kutoka Mwanza, mwanasheria wa CHADEMA na wakili wa mahakama kuu, Mabere Marando, alisema chama chake kinafahamu njama hizo na kwamba kimepanga kuchukua hatua za haraka kuhakikisha hakuna kura inayoibwa.

Kupatikana kwa taarifa hizi kumekuja siku 14 tangu gazeti la serikali, Daily News kujiapiza kuwa mgombea urais kupitia CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, hatakuwa rais wa tano wa Jamhuri.

Aidha, taarifa hizi pia zinakuja siku tano tangu Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi (JW), Luteni Jenerali Abdulrahman Shimbo atangaze kuwa jeshi linaingia rasmi katika mchako wa uchaguzi mwaka huu.

Ijumaa iliyopita, Shimbo aliwaambia waandishi wa habari, Dar es Salaam, kuwa majeshi ya ulinzi yameona dalili za amani kuvunjika na kwamba sasa yanawataka wananchi na vyama vya siasa kukubali matokeo ya uchaguzi utakaofanyika mwishoni mwa mwezi huu.

Alisema vyombo vya ulinzi vitashirikiana na NEC katika kipindi chote ili kuhakikisha kuwa wadau wote wanaheshimu matokeo. 

Vyama vya siasa, vyombo vya habari, asasi za kijamii, wanaharakati na watu binafsi wamelaani gazeti la serikali kwa kutangaza mshindi kabla uchaguzi haujafanyika.

Asasi hizo pia zimelaani kitendo cha jeshi kujiingiza katika mchakato wa uchaguzi zikisema ni kutoa vitisho kwa vyama vya upinzani na wapigakura.

Wakati huohuo, MwanaHALISI lina taarifa kuwa Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (REDET) unaandaa taarifa zitakazoonyesha kuwa mgombea urais wa CCM, Jakaya Kikwete, amepata ushindi wa asilimia 80.

Taarifa zinasema vijana waliopelekwa na REDET kufanya kura ya maoni wamenyimwa madaftari ya wakazi ambamo wangeopoa mtu mmojammoja wa kuuliza.

Badala yake wanukuu maoni wamekuwa wakielekezwa kwa wajumbe wa nyumba kumi (balozi) wa CCM na mashabiki wakubwa wa chama hicho, utaratibu ambao utaonyesha kuwa wanaopenda CCM na Kikwete ni wengi.

Alipoulizwa juzi juu ya mkasa huo, juzi Jumatatu, saa 11.52 jioni, mtafiti mkuu wa REDET, Dk. Bernadetta Kiliani alijibu, “Hilo si kweli.”

Alisema, “Watafiti wetu wamepewa ushirikiano wa kutosha na sina taarifa hizo unazosema.”

Kuhusu lini REDET itatoa matokeo ya utafiti wake wa uchaguzi wa mwaka huu, Dk. Kiliani alisema, “Subirini mtaambiwa.”

Bali imefahamika kuwa ripoti ya REDET imepangwa kutolewa wiki mbili kabla ya uchaguzi mkuu wa 31 Oktoba 2010 ikionyesha mshindi kuwa Kikwete kwa asilimia 80.

Alipotakiwa kuthibitisha taarifa kuwa REDET inasemekana kuwa tayari imeandaa matokeo ambayo yatamuonyesha Kikwete kushinda kwa asilimia 80, Dk. Kiliani alikata simu.

Dk. Benson Bana, mwenyekiti mwenza wa REDET na mshauri wa siasa wa Rais Kikwete, hakupatikana kutoa maelezo zaidi.

REDET ilituma watafiti katika mikoa 10 ya Tanzania Bara, ikiwamo Dodoma, Singida, Mtwara, Kilimanjaro, Mbeya, Iringa na Dar es Salaam.

Watafiti waliotumwa katika baadhi ya mikoa, walipewa maelekezo ya kukutana na watendaji wa vijiji, kata na mitaa ambapo kwa utaratibu wa awali walikuwa wakutane na wananchi kwa kutumia daftari la wakazi.

Habari zinasema REDET imekuwa na mawasiliano na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, juu ya mipango hiyo ili CCM ionekana inakubalika.

Hata hivyo, MwanaHALISI lina taarifa kwamba baadhi ya watafiti tayari wameripoti kwa Dk. Kiliani kulalamika kukutanishwa na mabalozi wa shina, lakini akaagiza kuwa watafiti wakubaliane na maelekezo yote wanayopewa na wahusika.

“Hawa REDET wametumwa kumfayia kazi Kikwete; ndiyo maagizo waliyopewa. Maana kila unapopita, unaambiwa hakuna daftari la wakazi, wakati serikali imetumia daftari hili katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka jana,” anasema mmoja wa watafiti waliotumwa na REDET.

Anasema, “Tumeripoti jambo hili kwa mkubwa wetu, Dk. Kiliani, lakini hakuna hatua zilizochuliwa, badala yake anasema tuendelee na kazi,”

“Haya yote yanalenga kuhalalisha matokeo yatakaoipendelea CCM,” anasema ofisa mmoja wa serikali ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini.

Asasi nyingine ambayo inashughulikia utafiti wa kura za maoni nchini ni Synovet ambayo hivi karibuni ilikana kufanya utafiti wowote juu ya uchaguzi wa rais.

Synovate ilikuwa inapinga kauli ya Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA, Freeman Mbowe aliyesema asasi hiyo ilificha matokeo ya utafiti yaliyotoa ushindi wa asilimia 45 kwa chama hicho na mgombea wake wa urais, Dk. Slaa, huku Kikwete akipata asilimia 41.

Mbowe alisema Synovate iliamua kuchukua uamuzi huo kutokana na kile alichoita, “kutumiwa na CCM.”

Siku moja baada ya taarifa hiyo kutolewa, Synovate ilikana kuficha matokeo, ikisema katika utafiti uliofanyika, hakukuwa na swali lililolenga kujua mgombea gani wa urais anayefaa kuchaguliwa.

Hata hivyo, MwanaHALISI limeona baadhi ya maswali ambayo watafiti wa Synovate walipewa. Miongoni mwake lilikuwa lililouliza: “Mgombea gani wa urais unamuona anafaa?”

Katika karatasi ya utafiti, Synovate waliweka majina ya wagombea 10 na kuuliza, “Nani ungependa zaidi kumpigia kura kuwa rais katika uchaguzi utakaofanyika mwezi wa kumi?”

Waliotajwa katika fomu ya dodoso, kwa mpangilio wa Synovate ni: Profesa Ibrahim Lipumba, Hashimu Rugwe, Mutamwega Mugahywa, Christopher Mtikila, Juma Ali Hatibu, Willibrod Slaa, Jakaya Kikwete, Paulo Kyara, Kuga Mzirai na Fahmy Nassoro Duvutwa.

Swali hilo lipo katika jalada Na. GPO 6, ukurasa wa 21 wa dodoso za utafiti Na. 42175 ya Septemba 2010.

MwanaHALISI ina mawasiliano kati Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Salva Rweyemamu na mwenyekiti wa kampeni za CCM, Abdurahman Kinana na January Makamba ambaye ni msaidizi wa rais juu ya nia yao ya kutumia Synovet kuwapa taarifa za uchaguzi.

Rweyemamu, katika andishi lake la 21 Juni 2010 ambalo lilinakiliwa kwa Kinana na January, anaelekeza kutumika kwa kampuni ya Synovate katika kampeni za CCM. Katika andishi jingine anasema wanaweza kutumia hata “kampuni nyingine.” Hakuitaja.

Alipoulizwa Rweyemamu kuhusiana kushiriki kwake katika mkakati wa kupika matokeo alisema hawezi kuzungumzia “kwa sasa,” na kusema “Mimi niko mbali.”

Alimtaka mwandishi kuwasiliana na Premi Kibanga ambaye ni mwandishi wa habari msaidizi wa rais.

Katika mawasiliano mengine yanayohusu kutumiwa kwa makampuni ya kitafiti, Rweyemamu anaadika kwa Kinana na January na kupeleka nakala yake kwa Thobias Makoba, Amina Lukanza, Patricia Michael, Chia Ngahyoma, Rashid Shamte na Maryam Nnauye akisema, “…tutakieni kila la kheri…”

Mtoa taarifa wa MwanaHALISI anasema kazi ya kuchakachua matokeo itafanywa kwa ustadi mkubwa kwa ushirikiano na kitengo cha IT katika ofisi isiyorasmi ya CCM iliyopo Na. 175, Mtaa wa Undali, Upanga, Dar es Salaam.

Ni katika ofisi hii, mtoto wa Kikwete, Miraji Jakaya Kikwete, ameweka marafiki zake wakiwamo wataalamu wa IT ambao alipata kusoma nao huko Bangalore, nchini India. Orodha ya majina ya watalaamu hao tunayo.

Inadaiwa kuwa ikulu inatumia Sh. 46 milioni kila siku kugharimia kundi la wataalam wa IT. Wenye mkoba wa kulipa wataalmu hao wametajwa kuwa ni Rweyemamu na Miraji.

Mtoa taarifa anasema wahusika wanahisi taarifa hizi zaweza kuvuja na kusababisha CHADEMA na vyama vingine kuandamana kupinga matokeo.

Hiki ndicho wachunguzi wa mambo wanaona ni uhalalishaji wa jeshi na vyombo vingine vya ulinzi kutangaza kujiingiza katika mchakato wa uchaguzi mwaka huu.

Mjumbe wa NEC-CCM ambaye hakutaka jina lake litajwe, amesema uchakachuaji wa kura unaotarajiwa “utafanana ule ambao CCM ilitumia katika chaguzi ndogo za Busanda na Biharamulo.

Mpango wa kutumia jeshi kudhibiti wapinzani uliwahi kutumiwa na rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe ambaye alitumia kitengo chake cha usalama wa taifa (CIO) na jeshi kushughulikia mpinzani wake mkuu wa kisiasa, Morgan Tsvangirai.

“Mazingira ya sasa yanaonyesha kuwa Kikwete anataka kutumia dola kama alivyofanya Mugabe, ingawa kuna baadhi ya mbinu naambiwa usalama hawaziamini kama zinaweza kumsaidia,” ameeleza M-NEC.

Gazeti liliwasiliana na Kinana kutaka kujua kama kweli chama anachopigia debe kimekuwa na “mikakati ya kimamluki.”

Kinana amesema hayo ni madai mazito ambayo alikuwa hajawahi kuyasikia. Amesema, “Sinazo taarifa hizo. Nasikia kutoka kwako. Naiheshimu Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Inafanya kazi zake kitalaamu zaidi. Inazingatia sheria na taratibu, hivyo sidhani kama wanaweza kuingia kwenye hayo unayonieleza.”

Kinana alisema utaratibu wa kuhesabu kura vituoni ni makini na kwamba kuna utaratibu wa mtu ambaye hakuridhika kwenda mahakamani.

“Mimi naona hizo ni kelele za vyama na wagombea wanaoona wazi kwamba wanashindwa. Wanaanza kutunga uwongo ili matokeo yakija ionekane yamepikwa,” amesema Kinana.

Alipobanwa kuhusu mpango wa REDET kutaka kutoa tathimini ya mwenendo wa uchaguzi ambako kwa mujibu wa uchunguzi wa MwanaHALISI, inaonyesha kuwa CCM itaongoza alijibu, “Hiyo sijui.”

Kwa upande wa Katibu Mkuu wa CCM, Yusufu Makamba, “Kuhusu hilo la kuchakachua matokeo, niseme ukweli, mimi ndiye katibu mkuu, hatujatuma watu na wala sina kauli zaidi ya hiyo.”

Lakini mwandishi alipotaka kujua kauli ya CCM juu ya jeshi kutoa tamko kali na kama hiyo siyo mwanzo wa jeshi kuchukua madaraka, Makamba alisema, “Nawapongeza.”

“Nchi haiwezi kuchukuliwa na jeshi kama unavyosema. Hilo halipo, bali nawapongeza kwa sababu wanataka uchaguzi ulio huru na haki. Jeshi haliwezi kwa sababu vyama vimeweka wagombea urais – CCM, CHADEMA, APPT, CUF sasa tuache siasa ifanye kazi.”

Kuhusu taarifa kwamba hata REDET imekuwa na mpango wa kutoa taarifa yenye maelekezo ya kuipamba CCM, Makamba alijibu, “Hilo nalo sijui.”

Naye Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Saidi Mwema alipotakuwa kusema kama ni kweli serikali imeagiza silaha msimu huu, hakuwa wazi.

Alisema, “Tatizo la watu wengi ni kwamba wanafikiri mambo ya usalama ni one-time event (tukio la mara moja tu), hii si kweli. Uchaguzi unafanyika mara moja lakini usalama ni jambo la kila siku.

“Hivyo vifaa unavyosema vimenunuliwa, havitatupwa baada ya uchaguzi huu. Vitaendelea kutumika miaka mingi ijayo kwa faida ya nchi yetu na watu hawatakiwi kutishwa na hilo,” alisema.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: