NSSF na ‘karata tatu’ kwa fedha za wafanyakazi


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 25 January 2012

Printer-friendly version
Gumzo la Wiki

SHIRIKA la Hifadhi ya Jamii (NSSF), kwa mara nyingine tena, limejitumbukiza kwenye mchezo wa karata tatu. Hakika, haliwezi kupata mavuno linayotarajia. Linaweza kuishia katika kulalama chini kwa chini na kisha kupoteza amana za wateja wake.

Wanaoufahamu mchezo wa karata tatu, wanasema wazi kuwa mchezo huu haumaliziki salama. Pale wachezeshaji wa mchezo wanapoona wanazidiwa kete na kutaka kuliwa, hutafuta mbinu, ikiwamo kuanzisha ugomvi ili kulazimisha ushindi na wakati mwingine hukimbia na fedha.

Wiki mbili zilizopita, NSSF ilijifunga kwenye mkataba wa mabilioni ya shilingi wa ujenzi wa daraja la Kigamboni, jijini Dar es Salaam. Mkataba wa ujenzi wa daraja hilo, utagharimu kiasi cha Sh. 214.6 bilioni. Kati ya fedha hizo, serikali imejifunga kutoa asilimia 40 na NSSF watawekeza asilimia 60.

Akizungumza kwenye hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa daraja hilo, Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli alisema, daraja litakalojengwa litahusisha ujenzi wa mita 680 kwenye ujenzi wa daraja la Kigamboni; njia sita za lami kwa umbali wa kilomita 1.0 upande wa Kurasini; na njia sita za lami kwa umbali wa kilomita 1.5 upande wa Kigamboni.

Alisema kwa upande wa kusini, daraja hilo litaungana na barabara ya Mandela kuelekea Tazara wakati upande mwingine litaungana na barabara ya Kurasini kuelekea Kamata. Njia zote hizo mbili zitafanyiwa matengenezo ili kupunguza msongamano wa magari.

Hii si mara ya kwanza kwa shirika hili kujiingiza kwenye michezo ya karata tatu. Katika maeneo mengi ambako NSSF imewekeza fedha nyingi, hasa kule ambako imeshirikiana na serikali, shirika hili limeishia kupoteza fedha zake.

Kwa mfano, shirika hili limeweka dola za Marekani 7.2 milioni (karibu Sh. 8.4 bilioni) kwenye mradi wa mkaa wa mawe wa Kiwira, lakini wapi! Hakuna kilichopatikana. Fedha zilitolewa kwa kampuni ya Kiwira Coal Mines Limited.

Ndani ya mkopo huu kuliwekwa sharti lililotaka mkopaji kurejesha mkopo wake miezi 6 baada ya mkopo kutolewa. Mkopo ulitolewa mwaka 2004. Lakini ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za  Serikali (CAG) inasema hadi 30 Novemba 2009, shirika hilo lilikuwa halijarejeshewa fedha zake.

Lakini si hivyo tu. Kifungu cha 10.5 cha mkataba kati ya Kiwira Coal Mines Limited na NSSF kinasema, iwapo mkopaji atashindwa kurejesha mkopo wake, serikali ndiyo itakayowajibika kurejesha mkopo huo kwa asilimia 100.

Kwanza, wakuu wa NSSF wanafahamu mchakato wa uuzaji wa mgodi wa Kiwira; uazishwaji wa makampuni yaliyomilikishwa mgodi huo ya Tanpower Resources Ltd., Dev Consult International Ltd., Universal Technologies Ltd., Choice Industries Ltd., Forsnik Enterprises Limited na ANBEM Limited.

Wanafahamu wamiliki wa makampuni haya ni akina nani; wameuziwa asilimia ngapi ya hisa; wanashikilia nafasi gani serikalini na hisa zao kila mmoja ni ngapi.

Wala wakuu wa NSSF hawawezi kusema kuwa hawakufahamu kama Kiwira Coal Mines Ltd., ilikuwa inamilikiwa na nani; ilimiliki kiasi gani cha hisa na serikali ilikuwa inamiliki asilimia ngapi.

Hawawezi kukana kufahamu kwa kuwa, nyaraka kutoka Wakala wa Usajili wa Makampuni na Biashara (BRELA), zinaonyesha kampuni ya Tanpower Resources Ltd., iliyosajiliwa 29 Desemba 2004 na kupewa cheti cha usajili Na. 51080, inamilikiwa na Daniel Yona, Evans Mapundi, Joe Mbuna na Nicholas Mkapa.

Wakati Yona, Mapundi, Mbuna na Nicholas Mkapa, walikuwa wanamiliki kampuni hiyo pia kupitia kampuni ya Tanpower Resources Ltd., Mkapa na mkewe, Anne Mkapa walikuwa wanamiliki kampuni ya Kiwira kupitia kampuni yao ya ANBEM.

Ndani ya kampuni hiyo, serikali ilikuwa inamiliki asilimia 15 na makampuni ya ANBEN na washirika wake wengine ikiwamo Tanpower Resources Ltd., walikuwa wanamiliki asilimia 85 ya hisa.

Pili, serikali ambayo ilidhamini mkopo huu ilikuwa inamiliki asilimia 15 tu ya hisa za mgodi wa Kiwira Coal Mines Ltd. Hii ina maana kwamba NSSF walikubali kutoa fedha za wavujajasho kwa manufaa binafsi ya kikundi fulani cha watu.

Tatu, kigezo kilichotumiwa na NSSF kutoa mkopo kwa kampuni ya Kiwira ni dhamana iliyowekwa na serikali na mkataba kati ya Tanpower Resources Limited na shirika la umeme la taifa (Tanesco) wa  8 Juni 2005 unaoipa mamlaka kampuni hiyo kuuza umeme wake kwa Tanesco.

Lakini ni mkataba huu, ambao NSSF waliutumia kama kigezo cha kutoa mkopo, unaoifunga Tanesco – shirika la umma – kulipa kiasi cha dola za Marekani 271 millioni (karibu Sh. 300 milioni kila siku), kama malipo ya kuweka mitambo – Capacity Charge ya mitambo ya Kiwira.

Kiasi hiki cha fedha ni nje ya malipo ya fedha zinazotumiwa kununulia umeme. Fedha ambazo Kiwira ilikubaliwa kulipwa, ni karibu mara mbili ya fedha ambayo Tanesco wanalipa makampuni ya Richmond/Dowans.

Je, katika mazingira haya, waliokabidhiwa kusimamia NSSF watasema nini? Watawezaje kukwepa shutuma, lawama na tuhuma kuwa walinufaika binafsi? Kama hawakunufaika binafsi, kwa nini walitoa fedha kwa watu waliokuwa na maslahi binafsi na waliolenga kuangamiza taifa?

Hii ni kwa sababu, fedha ambazo NSSF wametoa kwa makampuni haya, ni michango ya wafanyakazi wa Tanzania. Serikali iliyodhamini mkopo kwa asilimia 100, ni serikali ya Tanzania, ambayo mapato yake yanatokana na kodi za wananchi wakiwamo wanachama wa shirika hilo.

Kama hapa hakuna maslahi binafsi, kwa nini shirika limetoa mkopo ambao unaangamiza wanachama wenyewe – kutokana na Tanesco kulazimika kupandisha bei ya umeme?

Aidha, NSSF waliwekeza mabilioni ya shilingi wilayani Mwanga, mkoani Kilimanjaro wakati Cleopa David Msuya alipokuwa waziri mkuu. Huko shirika lilijenga jengo la kitegauchumi.

Taarifa zinasema jengo lililojengwa kwa thamani ya mabilioni ya shilingi, miaka 20 baadaye limeuzwa kwa bei ya kutupa ya Sh. 50 milioni. Aliyeuziwa anatajwa kuwa mfanyakazi mmoja wa NSSF ambaye siku moja baada ya kukabidhiwa, aliliuza kwa zaidi ya Sh. 800 milioni.

Ni NSSF iliyojenga nyumba 252 mkoani Dodoma kwa ajili ya watumishi wa serikali wanaohamia huko, kati ya mwaka 1991 na 1993. Leo hii, haijulikani nyumba hizo zinatumiwa na nani na kwa matumizi gani?

Kama hiyo haitoshi, NSSF iliweka fedha kwenye kiwanda cha sukari cha Kagera. Mkopo huu haukurudi, badala yake inaelezwa shirika limeamua kununua hisa kwenye kampuni hiyo.

Vilevile, uongozi wa NSSF umetoa mamilioni ya shilingi kwa kampuni ya Katani Ltd., ambazo hadi sasa hazijarudishwa.

Ripoti ya hesabu za shirika la magazeti ya serikali (TSN) inaonyesha NSSF waliuza jengo lao lililokuwa makao yake makuu ya Temeke kwa Sh. 1.2 bilioni kwa kile walichoita, “hawahitaji ofisi ya aina hiyo Temeke.”

Nyaraka zinaoenyesha hadi 30 Desemba 2011, TSN hawajaweza kumaliza deni la nyumba hiyo. Majuzi, wakuu wa shirika hilo walitangaza zabuni ya kununua nyumba itakayotumika kwa ajili ya ofisi yake ya Temeke.  

Katika wilaya ya Ilala, NSSF wana jengo karibu na hospitali ya Amana; lakini hawaitumii, badala yake wameamua kupanga ili kuweka ofisi zake za Ilala kwa mtu binafsi na kulipa mamilioni ya shilingi kwa mwezi.

Kuna mengi yanayofahamika na ambayo bado yanastahili kufanyiwa uchunguzi na kuwekwa wazi.

Lakini jambo moja ni wazi. Hatua ya NSSF kujitumbukiza katika miradi ya aina hii, baadhi ikiwa ya kifisadi na isiyo na tija kwa wanachama wake, kumetokana na serikali kushindwa kutekeleza miradi ya maendeleo iliyoahidi wakati wa kampeni na kushindwa kusimamia fedha za umma.

Popote pale ambako serikali imeshindwa kutekeleza wajibu wake wa kupeleka miradi mikubwa ya maendeleo, hutumia NSSF kuwekeza au kuahidi kuwekeza.

Ukiacha hilo, kuna hili pia. Kwa nini serikali imeamua kutumia mabilioni yote hayo ya shilingi kwa ajili ya ujenzi wa daraja, badala ya kutumia fedha hizo kuimarisha reli ya kati?

Je, watawala hawafahamu umuhimu wa reli hiyo kwa uchumi wa taifa? Hawafahamu kuwa reli inatumiwa na watu wengi zaidi kuliko daraja? Wanafahamu kuimarishwa kwa reli kungesaidia kuzifanya barabara ambazo zinajengwa kwa mabilioni ya shilingi kudumu kwa miaka mingi kwa kuwa mizigo mikubwa itapita kwa njia ya reli?

Serikali haifahamu kufufua reli kungesaidia kupunguza gharama za usafishaji, hasa mafuta? Mazao ya biashara na yale ya kilimo yangeweza kusombwa kutoka vijijini kwa bei rahisi? Haifahamu kuwa kuimashwa kwa reli kungesaidia kuondoa migogoro kati ya serikali na wafanyakazi wa shirika la reli la taifa (TRC)? (TRL)
Sasa kama yote haya inayafahamu, kwa nini NSSF imechagua kuendeleza migogoro na malumbano na wafanyakazi; kuhatarisha usalama wake iwapo mifuko hii itakamuliwa hadi kushindwa kulipa wanachama wake?

Kwa nini NSSF imeamua kuendelea kuwekeza katika mradi wa mashaka? Je, mradi uliobuniwa ukigeuka kero kwa wananchi, hasa wale wa kipato cha chini, pale wahusika watakapoamua kutoza nauli kwa watumia daraja, mfuko huu utajificha wapi?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: