Nyalandu atapasuka msamba

HUU ni mwaka wa vioja na mbwembwe. Watanzania wajiandae kuona mengi; kila aina ya mbwembwe za kisiasa za kujikweza kwa nia moja tu, kujijenga kisiasa.
Wiki imeanza kwa moja ya tambo hizo. Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Lazaro Nyalandu, Jumapili iliyopita aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kusema kwamba hayumo katika makundi ya vigogo ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaotajwa kukujipanga kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Aliwataja vigogo wanaotajwa kuwania kurithi kiti cha Rais Jakaya Kikwete kuwa ni pamoja na Mbunge wa Monduli (CCM), Edward Lowassa; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta.
Nyalandu anadai kuwa alisukumwa kueleza msimamo wake kuhusu mbio za urais kutokana na madai ambayo yamekuwa yakitolewa dhidi yake kupitia vyombo vya habari kuwa ama anasuka mipango ya kugombea urais au yumo chini ya moja ya makundi ya wanaotajwa kuwa na nia ya kugombea urais.
Mbunge huyo kijana anasema kwa namna yoyote ile, yeye si mgombea wa urais wa Tanzania . Alipiga hatua moja mbele na kusema hayuko chini ya kundi lolote kati ya aliyoyataja kuwa yanatajwatajwa kujipanga kugombea urais wa Tanzania mwaka 2015.
Nyalandu bado ni kinda katika siasa za mapambano na kuparurana za CCM. Mbali na nafasi ya kisiasa ya ubunge na unaibu waziri nyingine aliyonayo ni ujumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Singida.
Nyalandu pamoja na kujaribu kukimbiza ubawa wake katika rafu na mpambano usio na huruma wa kuwania urais, bado alionyesha jinsi alivyo na mahusiano mazuri na hao aliojitenga nao.
Akimzungumzia Lowassa alisema: “…ninamheshimu, ninamheshimu sana (Lowassa) na ni mara nyingi niseme tukiwa Dodoma nakunywa naye chai. Mi naendaga (naenda) nyumbani kwake. Na kuna kipindi nimeshawahi kuambiwa na baadhi ya watu tulionekana Monduli, kwa hiyo, moja kwa moja uko kwenye hilo kundi la mzee wa Monduli. Nilicheka sana .”
Kuhusu Sitta alisema, “Huyu ni ‘mentor’ (mwalimu). Ni mtu, ambaye kwanza ananishauri vitu vingi. Ni rafiki yangu hata kama akinisikia. Sidhani kama kuna siku itapita sijaenda kumwona mzee Sitta. Kama hatujaonana kesho yake tutaonana, tutazungumza, tunaenda kwenye maeneo mengi pamoja, jambo lipo tunashauriana.”
Kwa upande wa Membe alikuwa na haya: “Sasa turudi kwa marafiki zangu wanaojulikana wa kawaida, Bernard Membe. Ni rafiki yangu mzuri sana . Tumeanza naye Bunge mwaka 2000. Unajua siamini kwamba mwaka 2000 ni karibu miaka 12 iliyopita. Maana yake ni kama jana tu. Tukiwa 'ma-back bencher', Kamati ya Mambo ya Nje wote. Sisi ni marafiki, yaani ni marafiki. Kwanza nyumbani tunakaa jirani. Jioni lazima tuzungumze. Kwa simu lazima tuongee. Nikitaka 'kubipu' ugali nyumbani kwake sipigi hodi. Ni marafiki wa kiasi hicho. Kwa hiyo, mtu anayejisikia kunihusisha na lile kundi kama lipo, off course wamesema sana .”
Nyalandu ana haki ya kusema hicho alichosema. Ni haki yake. Lakini katika ulimwengu wa siasa hakuna kitu chochote kinachotokea kwa bahati mbaya kwa wanasiasa aina ya Nyalandu. Kila kitu kinapangwa, kwa nini aseme sasa na aseme nini.
Kivipi? Kwanza ameingia katika mtego wa kutaja makada waandamizi wa chama chake na serikali ambao wanataka urais. Hata kama yeye si mwasisi wake, kitendo tu cha kusema kuwa anafungamaishwa nao na kuwataja kwa majina, kwa maneno mengine naye ameshiriki kuwaambia wananchi kwamba wapo watu wanaopiga ‘jaramba’ kutafuta kiti cha urais.
Kwa hiyo, Nyalandu sasa anaingia kwenye rekodi ya viongozi wa serikali ya awamu ya nne wanaojadili suala la urais wakati bosi wake bado ana miaka minne ya kuwatumikia wananchi. Kama ilikuwa ni kwa bahati mbaya, basi Nyalandu ajue kuwa amechochea moto uliokuwa unawaka kwa maana hiyo utaongeza kasi ya kuwaka.
Hata hivyo, kwa upande mwingine, kwa kuzingatia mbinu za kisiasa hasa katika ulimwengu wa sasa ambao habari nyingi hutengenezwa na ‘ma-spin doctors’, Nyalandu naye amejitengenezea habari yake kwa nia ya kupata manufaa makubwa ya kisiasa pia.
Nyalandu anawakana akina Lowassa, Membe na Sitta, lakini anathibitisha kuwa yeye na wote hao ni damu damu. Anajifungamanisha zaidi nao; anawataka wote kwa kuwa hana hakika ajiegemeze wapi.
Kwa lugha ya kiuchumi ametenganisha mayai yake katika makapu matatu tofauti ili lolote likitokea abakie na akiba. Amejiwekea akiba, hawakatai watu hawa, ila anawasifu na kuonyesha kimsingi hana tatizo nao. Kwa maana hiyo kama angekuwa hana shida nao hakukuwa na sababu yoyote basi ya kimsingi ya kufanya mkutano na waandishi wa habari na kujaribu kujitenga nao wakati alichofanya ni kuthibitisha alivyo karibu na makada hao.
Kubwa zaidi ya yote, Nyalandu anajijua kuwa yeye si jabali ndani ya CCM, si jabali ndani ya mkoa wa Singida, wala si jabali kwa maana ya mwanasiasa mwenye mikakati na mbinu ya kuunganisha makundi na hivyo kusaidia kukusanya kura kama suala ni kupiga kampeni kwa wajumbe wa vikao vya maamuzi vya CCM.
Nyalandu analijua hili vizuri, lakini kama mwanasiasa yeyote yule angetamani sana awe na nguvu hizo. Kwa maana hiyo, anachojaribu kufanya kwa sasa ni kujaribu kujijenga kisiasa ili kuwa na nguvu za kukusanya kura na pengine kuwa nguzo ya kisiasa siku za usoni.
Ndiyo maana nilisema hapo juu kwamba huu ni mwaka wa vioja, mbwembwe na tambo. Hivi si kwa bahati mbaya ni mikakati ya kisiasa.
Huu ni mwaka wa uchaguzi ndani ya CCM, wanachaguana kuanzia ngazi ya shina hadi taifa, watachaguana kwa hila, inda na hata kwa fedha. Nguvu nyingi zitatumika kwa kuwa ni kwa kujipanga vizuri tu nafasi ya kupatikana kwa mgombea wa CCM wa urais 2015 itakuwa neema kwa waliojinyakulia nafasi muhimu ndani ya chama.
Katika nafasi za kisiasa mbali ya kuwa Naibu Waziri na Mbunge, nafasi nyingine ya uhakika ndani ya chama (kisiasa) aliyonayo ni mjumbe wa kamati ya siasa ya mkoa wa Singida. Sasa utokaji huu wa sasa juu ya Lowassa, Membe na Sitta unalenga kumsaidia kisiasa zaidi au vipi? Jibu ni moja tu ndiyo.
Ni ndiyo kwa sababu kuanzia sasa iwe rasmi au vinginevyo, iwe chini kwa chini au wazi, kinachoitesa CCM kuelekea mwaka wa uchaguzi ni kiti cha mgombea urais hapo 2015. Hayuko mwanasiasa yeyote makini anayeweza kupuuza ukweli huo, ndiyo maana Nyalandu amebuni mkakati wake, kuuma na kupuliza; anatamani kula keki yake lakini bado ibaki mkononi.