Nyerere atakumbukwa, wengine watapuuzwa!


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 15 June 2011

Printer-friendly version

NDANI ya mitandao ya mawasiliano mbalimbali kumeibuka wimbi la watu wanaomshabulia Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na yale aliyotuachia.

Katika baadhi ya maandiko, waliopandikizwa kumchafua Nyerere wanamtuhumu kuwa alikuwa dikteta na wengine wamempachika jina la “Baba hambiliki.” Baadhi ya tuhuma zinaonekana ni za kupikwa na hazina mashiko.

Kwa mfano, nimeona baadhi ya watu wakimtuhumu Nyerere kwa kukosekana kwa katiba mpya na wengine wakisema wakati wa utawala wake ameshindwa kuleta mawasiliano ya intaneti na yale ya simu za mkononi.

Hata hivyo, jambo moja ni wazi: Mashambulizi dhidi ya Nyerere hayajaanza leo na wala hayatarajiwi kukoma leo. Ni kwa sababu, walioandaliwa kumchafua Nyerere wamelenga kuficha udhaifu wao wa uongozi.

Zipo taarifa zinazoweza kuthibitishwa kuwa mashambulizi haya yamebuniwa vizuri na yanatekelezwa na baadhi ya watu waliopo madarakani.

Ni baada ya kugundua kuwa hawawezi kuongoza na kutawala wakiwa chini ya mwavuli wa uongozi wa Nyerere.

Bali, njia pekee ambayo wangeweza kulifuta jina la Nyerere ni kama wao wangeweza kutawala vizuri zaidi, kujenga umoja wetu zaidi na kutupa nafasi ya kuthaminiwa na kutambuliwa utu wetu kama alivyofanya Nyerere ambaye alisema mwanadamu ndiye lengo na shabaha la maendeleo yote katika taifa.

Wanataka Nyerere achukiwe kwa mambo yanayotokea sasa nchini, ili wao wapate nafafsi ya kuonekana kuwa viongozi wazuri kuliko yeye. Wamekosea.

Nimekaa na kuangalia jinsi ambavyo historia ya taifa inapotoshwa na yale ambayo Nyerere alisimamia.

Nakumbuka wakati wa kifo chake, ni magazeti machache sana ya Marekani na Uingereza yaliyomuita Nyerere dikteta. Ninayo orodha ya vyombo karibu vyote vilivyoripoti kifo cha Nyerere kuanzia yale ya kiingereza hadi kiswahili.

Wala hakukuwepo Mtanzania aliyesema “dikteta kafa.” Sijawahi pia kusikia kulikuwepo sherehe mitaani kufuatia kifo cha Nyerere. Yawezekana walikuwepo watu mmoja mmoja walioshangilia pengine kwa sababu zao binafsi, lakini sidhani kama wangethubutu kufanya hivyo hadharani!

Lakini kuanzia kuelekea uchaguzi mkuu wa 2005 na hadi sasa kauli za kumlaumu Nyerere zinazidi kupata sauti, si kwa sababu zina mapya ya kusema, bali kwa sababu hazina kingine cha kusema kuelezea ubovu wa utawala wao na kutimiza malengo yao ya baadaye.

Tunawasikia baadhi yao wakimlamu Nyerere kuwa alikuwa mdini; lakini watu hao hao hawawezi kuuona udini uliyopo leo hii ndani ya taifa hili.

Wengine wameanza kumuita Nyerere mkabila – ati kwa sababu alizuia watu wa kabila fulani wasije kuwa marais. Lakini wakabila waliopewa vyeo vya kila aina na wanajulikana na hawaguswi!

Wale waliodhaifu wa kufikiri au kutafuta ushahidi, baadhi yao wameanza kuamini kuwa Nyerere alikuwa mkabila na mdini. Hili si kweli. Nyerere alizuia genge la watu wasiokuwa waadilifu kuwa viongozo.

Mashambulizi dhidi ya Mwalimu Nyerere yamefikia mahali yamevuta hata watu dalili ya usomi. Hata hivyo, sitoshangaa muda si mrefu hawa hawa walioanza kumuita Nyerere dikteta, wataanza kuitana wao kwa wao kutokana na kushindwa kujilinganisha na Nyerere.

Nyerere alikuwa na uwezo wa kusikiliza hoja, kuichambua na hata kuikataa hoja hiyo kwa hoja yenye nguvu. Ushahidi upo. Hatua yake hiyo, imewafanya baadhi yao hadi leo kumuita “haambiliki.”

Lakini ukiwauliza mlimuambia nini mpaka mnasema haambiliki? Jibu watakwambia Edwin Mtei alimshauri juu ya kufufua uchumi, lakini hakumsikiliza. Watu hawawaulizi mbona Mtei yupo kwanini hasikilizwi sasa? Hawana jibu.

Karibu mambo yote ambayo Mtei aliyasema yumkini yapo yaliyofanyika, lakini mbona watu hawajaridhika na kushukuru au hata kumpa nishani ya asante?

Ni kwa sababu, tatizo lao ni Nyerere. Baadhi yao aliwazuia kuwa viongozi wakuu wan chi na wengine wanaendelea kuteswa na mzimu wake kwa kushindwa kumsikiliza.

Hakuna mashaka kwamba Nyerere anasimama kama kipimo kisichofikiwa na viongozi uchwara waliopoteza maono ya uongozi na ambao hawana uwezo wa kuongoza watu isipokuwa kwa vitisho, ulaghai na kuzuga.

Bahati njema ni kwamba, jaribio hili la kumshambulia Nyerere na yale aliyotuachia kama mbinu ya kuficha mapungufu yaliyopo ya baadhi ya viongozi wa sasa na wale wajao, litashindwa kama ambavyo yameshindwa mengine.

Watanzania wanajua tofauti ya uongozi na ulaghai; wanajua tofauti ya ushawishi na vitisho; wanajua tofauti ya kupendwa na kulazimisha kupendwa.

Kama Nyerere alikuwa dikteta, tena dikteta aliyeiharibu nchi (mtu mmoja amesema ‘beyond repair’) basi hawa waliopo sasa ni lazima tuwape ushujaa.

Kama alikuwa kiongozi mbaya na aliyewatesa watu wake na kusababisha njaa na matatizo mbalimbali, basi hawa wa leo lazima waimbiwe nyimbo za tuzo kwani chini ya uongozi wao kuna lundo la televisheni, kompyuta na simu za kila aina.

Kama Nyerere alikuwa kiongozi mbaya kwa taifa letu ambaye hakuwajali wananchi wake na alitumia nafasi yake kujinufaisha binafsi na kupora utajiri wa nchi hii kwa ajili ya familia yake na yeye mwenyewe, basi hawa waliopo sasa ni lazima tuwape tuzo ya uzalendo kwa jinsi ambavyo hawajinufaishi wao wenyewe, na wanavyolinda raslimali zetu.

Kama Mwalimu alitumia nafasi yake kuruhusu ndege za kigeni kuja nchini na kutua katika nchi yetu –tena za kijeshi – kwenda hadi mbugani, kuchukua wanyama wakiwemo twiga mithiri ya kuokota korosho, kusafirisha na kuwapeleka nje ya nchi, basi hawa wa leo wapewe pongezi kwa jinsi vyombo vyao vya usalama na jeshi la ulinzi wa Tanzania (JWTZ) vinavyofanya kazi kwa ufanisi kulinda maliasili yetu na jinsi ambavyo chini yao hata kware hawezi kuibwa bila wao kujua!

Lazima nikiri mimi ni mpenzi wa Nyerere; kama alikuwa dikteta natamani hawa wa leo wajaribu kidogo tu kufanana naye katika udikteta wake ili tuone kama na wao hawatapendwa na kuliliwa siku wakiondoka. Vinginevyo, wengine hawatoliliwa siku wakitutoka. Watajiuliza kwanini wakati mimi sikuwa dikteta?

Nyerere anabakia kuwa alama ya kiongozi aliyelipenda taifa lake na watu wake na ambaye hakuwa tayari kusaliti wananchi wake kwa kipande cha dhahabu. Alikuwa kipimo cha uongozi kwa wakati wake na hadi sasa. Hakuwa mbinafsi. Alipenda watu wake na taifa lake; kwa sababu hiyo wananchi nao walimpenda.

Hawa wengine na mashabiki wao sijui kama tunawapenda kweli au tumejikuta tunalazimishwa kusema tunawapenda. Maana tukisema tunawachukia na wakageuka kuwa madikteta wa kweli ndipo tutajua Nyerere hakuwa hata kwa umbali karibu na udikteta - japo angetaka angekuwa kama Mobutu Seseko! 

Natoa wito kwa wote wanaoitakia mema taifa hili, waache kutumiwa na watu wenye malengo binafsi. Badala yake wakishiriki katika kumuenzi Nyerere.

mwanakijiji@jamiiforums.com
0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: