Opulukwa: Nipo vitani Meatu, nitashinda


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 21 December 2011

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii

MBUNGE wa jimbo la Meatu, Meshack Opulukwa anapiga mayowe. Kwa miezi miwili hakuna anayemsikiliza. Amekuwa akihangaika kutafuta ufumbuzi baada ya serikali ya mkoa kuamuru operesheni ya kuhamisha kwa nguvu makazi ya watu katika kijiji cha Mwangudo, ndani ya jimbo analoliwakilisha.

Uhamishaji huo umefanywa kwa sababu ya kinachoelezwa wananchi “wanaishi ndani ya hifadhi ya jamii ya Makao.” Matokeo ya operesheni hiyo ni kuteketezwa kwa moto zaidi ya nyumba 1,000 za wananchi na mamia ya watu kuumia. Baadhi wamelazwa Hospitali ya Wilaya.

Opulukwa amesema katika mahojiano na gazeti hili yaliyofanyika wiki iliyopita jijini Dar es Salaam, kwamba watu wanatuhumiwa na serikali kuwa mstari wa mbele kupinga operesheni hiyo.

Mbunge huyo mwenye umri wa miaka 44, anayetoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), hajatetereshwa kimsimamo na operesheni hiyo.

Akiwa bungeni mjini Dodoma Novemba 15, alilitolea taarifa tukio hilo kwa kiongozi aliyesimamia vikao vya siku hiyo vya bunge, Jenista Mhagama, akitaka bunge litoe nafasi ya kujadiliwa kutokana na umuhimu wake.

“Unajua, suala hili nililiombea mwongozo kwa spika kutaka atoe nafasi ya kulijadili bungeni kwa kuwa ni la dharura… wananchi wamejeruhiwa kutokana na moto na vipigo vya polisi. Kanuni 47 na 48 za bunge zinaruhusu mbunge kutoa hoja ya kutaka jambo la dharura lililotokea lijadiliwe bungeni,” anasema.

“Nilipata taarifa kutoka jimboni kwamba Mkuu wa Mkoa aliagiza uongozi wa wilaya kuchoma nyumba za wananchi waliodai wamekaidi amri halali ya serikali. Nikaambiwa nyumba 600 hadi 1,000 zilishateketezwa moto,” anasema.

Akimnukuu Mhagama, ambaye ni mbunge wa Peramiho, mkoani Ruvuma, Opulukwa anasema aliona uzito wa suala hilo na kumwelekeza akamwarifu Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye kwa mamlaka yake, anaweza kutoa agizo haraka kwa uongozi wa mkoa.

“Siku ileile nilimuona waziri mkuu. Nakumbuka mheshimiwa Pinda alimwagiza Mkuu wa Mkoa kusitisha mara moja operesheni hiyo na iundwe tume ya kuchunguza kiini chake.”

Lakini, anasikitika hakuna kilichofanyika. “Naona waziri mkuu anapuuzwa maana agizo lake halikutekelezwa. Mimi ni mbunge, ninapotoa kilio cha wakazi wa jimbo langu natarajia hatua zichukuliwe.

“Waziri mkuu alitoa agizo lakini linaishia hewani. Viongozi wanampuuza waziri mkuu, sasa hii ni hatari lakini ipo siku watajuta,” Opulukwa analalamika.

Opulukwa akaamua kukimbilia jimboni ambako wananchi waliohamishwa kwa nguvu kutoka kwenye makazi yao, wanalalamika kupewa mbegu mbovu za pamba.

Anasema sasa ametambua serikali huwa ndio kikwazo cha maendeleo ya wananchi. “Haiwezekani viongozi wadharau wananchi. Naona haya ni miongoni mwa changamoto nzito mbele yangu katika kuhamasisha maendeleo jimboni,” anasema.

“Jimboni kunafanyika mambo ya ajabu. Serikali inaleta mbegu mbovu za pamba na viongozi hawajali. Hata kama mtu si bwana shamba unagundua haraka mbegu hazifai. Ajabu, wananchi wanasema waziwazi ‘mheshimiwa tunafanyiwa hivi kwa sababu tumekuchagua wewe mbunge wa upinzani.”

“Najua nipo vitani na nitashinda,” anasema Opulukwa huku akitaja mipango ya kuharakisha maendeleo jimboni kama alivyoahidi wakati wa kampeni.

Anasema amechukua ‘wazo’ la baba yake, Jeremiah Opulukwa (marehemu), kwa kuandaa mfuko maalum wa fedha utakaotumika kutatua shida za watu katika harakati za kujiimarisha kiuchumi na kijamii.

Kupitia mfuko alioupa jina la The Opulukwa Foundation, anasema amebuni programu inayolenga kuwahamasisha wananchi kushiriki shughuli za maendeleo na watapatiwa mikopo kutoka mfuko huo ili watimize ndoto zao.

Elimu kwa vijana itatiliwa mkazo sana, anasema, na kuongeza kwa wale wanaomaliza elimu ya msingi, watasaidiwa watakapoingia sekondari ili kuwajenga kuingia ngazi ya chuo kikuu. “Kila mmoja atasaidiwa anapopamudu kufika,” anasema.

Mfuko utakapoanza utagharimia wanafunzi hadi watakapohitimu masomo yao bila kujali watakuwa wamefikia ngazi gani – kidato cha tano, sita au chuo kikuu.

Anasema hataki kufanya hayo peke yake. Atashirikisha idara zinazohusika serikalini, halmashauri ikiwa mojawapo. “Halmashauri ya Wilaya itasimamia upatikanaji wa wanafunzi watakaokuja kusaidiwa na mfuko kufikia malengo yao kielimu,” anasema.

Kwa watu wakubwa wanaojishughulisha na miradi midogo ya kiuchumi wakiwemo kinamama, vijana, wazee waliounda vikundi, Opulukwa anasema mfuko huo utawapatia mikopo yenye masharti nafuu.

Tangu alipochaguliwa, Opulukwa amekuwa akihimiza wananchi kuunda vikundi na kuanzisha miradi ya kujitegemea kama vile ushoni, uvuvi, matoroli ya kisasa na biashara ndogo. “Miradi kama hii itanufaika na fedha za mfuko tunaouanzisha,” anasema.

Anasema lengo jingine la mfuko ni kununua gari litakalotumika kufuatilia ng'ombe wanaoibwa kwa wafugaji wa jimboni kwangu. Hayo ni matatizo sugu jimboni kwake.

Opulukwa ambaye ameweka makao ya jimbo kijijini kwao Mwanhuzi-Meatu, anasema pia anahitaji gari la kubebea wagonjwa ili kuwasaidia kufika hospitali kwa haraka.

Wananchi wa Meatu walianza kumfuatilia mwaka 2000 alipoingia kwenye siasa. Aligombea ubunge kuwakilisha chama cha United Democratic Party (UDP). Alishindwa kwa kura 400 na Jeremiah Mulyambate, aliyewakilisha Chama Cha Mapinduzi (CCM). Alipata kura 10,500 dhidi ya 10,900 za Mulyambate.

Ingawa alishindwa, anasema matokeo hayo yalimtia moyo sana kwamba kumbe anaweza kupambana katika uwanja wa siasa.

Alijenga mtandao ili kunyaka ushindi katika kinyang’anyiro cha ubunge 2005. Hakufua dafu tena. Akaamua kufuata kaulimbiu ya “Ukishindwa kupambana nao, ungana nao.” Alirejea kundini CCM. “Niliona vyama vya upinzani vilikuwa vimepoteza mwelekeo.”

Hata hivyo, uamuzi huo haukudumu. Kabla ya kura za maoni ndani ya CCM za kutafuta wagombea, alijiunga na CHADEMA.

Opulukwa aliishinda CCM kwa tofauti ya kura 1,026. Alipata kura 13,850 dhidi ya 12,824 za Salum Khamis wa CCM. “Siri moja tu ya ushindi, wananchi waliamini katika haki na uhuru wa kuamua na kunichagua kama alama ya mabadiliko.”

Anasifia mafanikio aliyopata kwamba wananchi wameanza kunufaika na kufahamu elimu ya sheria na katiba, suala alilolihimiza sana wakati wa kampeni.

Opulukwa alizaliwa 27 Julai, 1967. Alipata elimu ya msingi Balili-Bunda na sekondari hatua ya awali katika shule ya Bupandagila (1988) wilayani Bariadi. Alijiendeleza hatua ya juu ya sekondari katika shule ya Geita High School (1991).

Aliingia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam 1993-1996 na kupata Shahada ya Kwanza ya Sayansi ya Jamii (Ardhi na Mazingira) mwaka 1996. Aliajiriwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kazi ya meneja wa mradi wa Mpango wa Uzazi Salama hadi Januari 1997. Baadaye aliajiriwa na Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH).

Agosti 1998, alikwenda nchini Japan kusomea usimamizi na utunzaji wa mikoko katika kituo cha Okinawa. Aliporudi nchini, alijiunga na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kusomea usimamizi wa maliasili na kilimo endelevu. Alihitimu mwaka 2000 na kurudi kazini COSTECH.

Mwaka 2001 alisomea uongozi katika taaluma (Leadership and Professional Development) katika Chuo Kikuu cha Purdue, Indiana Marekani. Mwaka 2002 alijiunga na Chuo Kikuu cha Hartford, hukohuko Marekani kusomea Shahada ya Juu (PhD) kuhusu usimamizi wa wanyama. Shughuli za siasa zimesababisha aahirishe masomo hadi baadaye.

0
Your rating: None Average: 1 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: