MHARIRI mwanzilishi wa gazeti hili, Aristariko Konga, amefariki dunia juzi Jumatatu katika hospitali ya jeshi Lugalo, jijini Dar es Salaam, alikolazwa wiki mbili zilizopita.
Msiba wa marehemu Konga uko nyumbani kwake Ubungo Kibo, jirani na baa ya Mpembene ambako mipango ya mazishi inafanywa.
Katika maisha yake ya uandishi wa habari, Konga alifanyia kazi katika vyombo vingi kikiwamo cha serikali - Idara ya Habari (MAELEZO), alikoanzia.
Yafuatayo ni maelezo ya wanahabari mbalimbali waliomfahamu na kufanya naye kazi kwa muda mrefu, kwa nyakati mbalimbali.
Saed Kubenea, Mkurugenzi Mtendaji wa Hali Halisi Publishers Limited (HHPL), wachapishaji wa magazeti ya MwanaHALISI na MSETO anasema:
Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kuondokewa na mwenzetu Aristariko Konga ambaye tulimfahamu na kumpenda.
Nilianza kufahamiana na Konga mwaka 2001 wakati huo akiwa Mhariri wa gazeti la Mtanzania Jumapili, mimi nikiwa mwandishi hapo na hivyo nikiripoti kwake.
Namfahamu Konga kama mchapakazi ambaye hata katika hali yake ya ugonjwa bado alikuwa akija kazini kufanya kazi.
Yeye ndiye aliyekuwa mhariri wa kwanza wa magazeti yetu. Nakumbuka kipindi hicho nilipokuwa nampigia simu usiku wa manane kumweleza kuhusu habari ambayo tulipaswa kuijadili, kesho yake alifika ofisini saa moja asubuhi.
Salva Rweyemamu, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu (aliwahi kuwa Mkurugenzi Habari Corporation)
Ni pigo kubwa sana kwenye taaluma ya habari. Konga alikuwa hagombani na mtu. Alifanya kazi yake vizuri.
Namkumbuka sana alipokuja kujiunga kwetu Habari Corporation Ltd (HCL) mwaka 1996. Aliondoka na kurudi mwaka 1998 na kisha kuondoka tena. Aliamua kurudi Habari Corporation mwaka 2001.
Tulithamini sana mchango wake kama mwanataaluma.
Ansbert Ngurumo, mchambuzi wa habari na Naibu Mhariri Mtendaji wa Free Media
Nimemfahamu Konga tangu mwaka 1997 akiwa Habari Corporation. Alikuwa mwandishi asiyechoka hadi akamilishe jukumu alilokabidhiwa. Hakuwa mtu wa majungu, na hakuwa na makuu. Alikuwa na uwezo wa kuchangamana na kila kundi; na alijawa na uso wa tabasamu. Tabia yake hii ilimrahisihia kazi ya kuhoji vyanzo vya habari, na ilimfanya kuwa mwanga kwa waandishi wachanga. Mungu amjalie pumziko la milele!
Jabir Idrissa (Mhariri wa sasa wa MwanaHALISI)
Nimemfahamu Konga tangu mwaka 1989 tukiwa wanafunzi katika Chuo cha Uandishi wa Habari Tanzania (TSJ) wakati huo kikiwa Shariff Shamba, Ilala.
Alikuwa ni mpole sana. Alikuwa muwazi, mkweli na muungwana kiasi cha kuwa rahisi kwa mtu yeyote kufanya naye urafiki. Nilikuwa karibu naye sana pamoja na Florian Ndyesumbilai (aliyepo Mwananchi), hata tulikuwa tunaambatana Uwanja wa Taifa kutazama mechi.
Konga alikuwa mchapa kazi mzuri na mzingatiaji mkubwa wa maadili ya uandishi wa habari.
Nilichokuja kubaini baada ya mwaka 2000, muda mrefu tangu tulipoachana chuoni mwaka 1991, ni kwamba upole wake ulikuwa umeandamana na tabia ya usiri.
Isingekuwa usiri wake huo, huenda sisi tuliokuwa karibu naye tungeweza kumsaidia mapema zaidi katika ugonjwa wake. Nitamkumbuka sana.
Alfred Lucas, Mhariri wa gazeti la MSETO, gazeti dada la MwanaHALISI.
Nimemfahamu Aristariko Konga tangu mwaka 1999 wakati nikiwa nimetoka shule na kuanza kazi ya uandishi katika iliyokuwa kampuni ya Habari Corporation Limited (HCL).
Konga alinipokea na kunisaidia. Zaidi ya uandishi wa habari, kwangu alikuwa mwalimu mzuri kwa waandishi chipukizi.
Nakumbuka neno lake la mwisho kwangu lilikuwa: “Naomba Mungu anisamehe na ninyi mnisamehe kwa usumbufu wowote ninaowasababishia.”
Absalom Kibanda, Mhariri Mtendaji wa Free Media Limited na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri
Konga atakumbukwa kwa kutokuwa na makuu. Alikuwa na uwezo mkubwa wa kutenda kazi; na alikuwa mhariri makini.
Ndimara Tegambwage, Mshauri wa Taaluma wa kampuni ya HHPL.
Konga ameishi kipindi chake na amefanya kipande chake cha kazi. Laiti kila mmoja angefanya kazi yake hadi siku chache kabla ya kuaga dunia!
Ni mmoja wa waandishi wachache nchini walioamini kwamba maadili ya uandishi hayatungwi na serikali wala wanasiasa wenye uchoyo wa kuandikwa kwa mapambo; bali wanataaluma wenyewe.
Danny Mwakiteleko, Naibu Mhariri Mtendaji, New Habari (2006) Ltd.
Msiba wa Aristariko Konga umenigusa sana. Kusema kweli ninakosa maneno ya kueleza namna ninavyojisikia.
Nilikutana na Konga wakati iliyokuwa kampuni ya Habari Corporation Limited ilipoanzisha gazeti la MTANZANIA.
Yeye na Revocatus Makaranga ndio waliokuwa walimu wangu katika fani hii wakati huo. Wao ndio walionielekeza pa kwenda wakati wa kutafuta habari.
Nitammisi sana Konga kusema kweli. Alikuwa mwanataaluma mahiri na nilimheshimu sana.
Jesse Kwayu, Mhariri Mtendaji, Nipashe
Kifo cha Aristariko Konga ni pigo kubwa katika tasnia ya habari hapa nchini. Huyu hakuwa mwandishi wa habari wa kawaida, alikuwa mpiganaji.
Alikuwa na uzoefu mkubwa wa kazi yake. Zaidi ya kwamba alisomea kazi hiyo, Konga alijijengea uzoefu mkubwa kwa kufanya kazi katika vyombo vingi vya binafsi nchini.
Katika mwaka huu wa uchaguzi, waandishi wa aina ya Konga ni muhimu sana katika kutoa maelekezo kwa vijana wanaochipukia katika fani hii.

Pole kwa Watanzania wote kumpoteza mtu muhimu kama huyu, pole pia kwa uongozi wa Mwanahalisi kuondokewa na mwanataaluma mwenzao.
Hakika nafasi yake kuzibika ni vigumu hasa kipindi hiki ambapo wanataaluma wanaochipukia wameweka pembeni maadili ya taaluma.
Mungu ailaze mahali pema roho ya ngugu yetu Konga.