Pinda, Waziri Mkuu muungwana au dhaifu


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 08 December 2010

Printer-friendly version
Tafakuri
Waziri Mkuu Mizengo Pinda

UNAPOZUNGUMZA viongozi wakuu wa kitaifa nchini, unakusudia Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu kwa upande wa utawala, lakini pia yumo Jaji Mkuu kwa upande wa Mahakama na Spika wa Bunge kwa upande wa Bunge.

Ndio kundi la viongozi wanaotambuliwa kikatiba kama viongozi wa kitaifa ambao majukumu yamefafanuliwa kama ni mkataba wa wananchi wa vile wanavyotaka kuendesha mambo yao.

Hivi karibuni, Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliripotiwa gazetini kuwa amekataa kutumia gari jipya aina ya Toyota Land Cruiser VX V8 alilonunuliwa na serikali kwa sababu alilonalo bado ni zuri na akaagiza gari hilo wapewe watumishi wengine.

Tukio hilo lilitokea kabla ya uchaguzi mkuu uliomrudisha katika wadhifa huo baada ya kuteuliwa tena, kufanyika.

Pinda tangu alipoteuliwa kwa mara ya kwanza Februari 2008 amekuwa na kampeni za kutaka serikali iachane na tabia ya kununua magari ya kifahari, maarufu kama mashangingi – mlolongo wa magari ya 4X4 kama vile Nissan Patrol, Toyota Land Cruiser za msururu wa VX, GX, Parado na mengine kama Mitsubishi Pajero na Isuzu Tropper.

Magari haya yanapigiwa kelele kwa sababu moja tu: Katika uchumi wetu dhaifu kuyatumia ni kubebesha wananchi mzigo mkubwa wa gharama utakaoathiri utoaji wa huduma kwa maeneo mengine muhimu zaidi kwa watu.

Kwa mfano, kama gharama ya kujenga darasa lenye sakafu, paa, samani ndani yake na kuta zilizopakwa rangi inaweza kufikia Sh. milioni saba, fedha za shangingi moja tu linalouzwa hadi Sh. 250 milioni, kutegemea na vikorombezo vyake, zinaweza kujenga madarasa 36. Ni shule yenye mikondo minne na ofisi za walimu.

Thamani hiyo anatembea nayo kiongozi mmoja wa serikali, kama waziri hivi ambaye mara nyingi anakaa madarakani kwa miaka mitano. Ukimuuliza muda huo amefanya nini anatafuta la kusema.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika Ibara ya 52(1), inataja kazi za Waziri Mkuu kuwa atakuwa na madaraka juu ya usimamizi, utekelezaji wa siku hadi siku wa kazi na shughuli za Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Maana yake usimamizi huu ni lazima wakati wote uzingatie maslahi ya wananchi. Wengi katika nchi waonekane wakinufaika na maamuzi ya watawala. Hili limekuwa ndio kilio cha Waziri Mkuu Pinda kwa muda mrefu.

Kwa mfano, alipokutana na wahariri mara ya mwisho jijini Dar es Salaam, Pinda alieleza ugumu anaokutana nao katika kufanikisha dhamira yake hiyo.

Anasema hata mkurugenzi wa halmashauri au mwenyekiti wa halmashauri naye anataka kutembelea VX V8, bila ya kujali gharama yake kubwa.

Wananachi waliamini Pinda kwa kauli zake alikuwa amekuja na mwarobani wa kukomesha ulevi wa magari ya anasa serikalini. Anasa hii ni kubwa na ni ulevi kweli kweli.

Jaribu kufikiria kila mkurugenzi wa serikali bajeti yake ya mafuta ya gari kwa wiki ni lita 200. Kwa mwezi hizo ni lita 800, awe anakaa karibu na ofisi yake au mbali.

Haya ni matumizi ambayo Pinda anayajua kama kiongozi mkuu mtendaji na msimamizi wa shughuli za serikali; mwenye wajibu wa kuhakikisha kila agizo analotoa Rais linatekelezwa.

Katiba ya Tanzania Ibara ya 52(3) inasema: “Katika utekelezaji wa madaraka yake, Waziri Mkuu atatekeleza au kusababisha utekelezaji wa jambo lolote au mambo yoyote ambayo Rais ataagiza kwamba yatekelezwe.”

 

Madaraka haya yakiunganishwa na yale ya ibara ya 52(1) yanafanya madaraka ya Pinda, huyu Waziri Mkuu, kuwa makubwa kiasi cha kuweza kusaidia kuliondoa taifa katika ulevi wa matumizi ya anasa kila kukicha.

Nashangaa kwamba Pinda anafikia hatua ya kukataa gari, lakini analikubali litumiwe serikalini. Hatari iliyoje?

Haijulikani kwa kukataa kwake gari hili amelisaidiaje taifa dhidi ya ulevi wa kupenda anasa, kwa sababu mwisho wa yote, gari hilo limo serikalini, litatumiwa, gharama za kuliendesha ni zilezile iwapo angelitumia Waziri Mkuu.

Nataka kuonyesha uamuzi wa Pinda wa kukataa gari ghali, usivyo na mantiki anaporidhi gari hilo kutumiwa na ofisa mwingine wa serikali ambayo ana madaraka makubwa kikatiba.

Hajatumia mamlaka hayo kuipunguzia serikali mzigo. Hajasalimisha mapato ya walipa kodi fukara wa Tanzania; na hajaonyesha kweli yeye ni mtoto wa mkulima.

Kila nimapomsikiliza Pinda kuzungumza kama mtu asiye nguvu zozote napata shida maana najua fika kwa aina ya watumishi wa serikali tulionao, hakutakuja mabadiliko kimatumizi.

Pinda anataka na kutamani sana kufuata urasimu wa kiserikali ambao umejaa upotezaji muda na mianya ya matumizi mabaya ya raslimali za serikali.

Kwa mfano, haijulikani inakuaje hadi gari la Waziri Mkuu liagiziwe Japan, linalipiwa, linafika Dar es Salaam halafu aliyeagiziwa halihitaji. Uagizaji wa gari kama huu ni maamuzi mabovu kiuchumi.

Uamuzi wa Pinda unaonyesha wazi kuwa serikalini kinachotakiwa ni huruma za kiongozi kama yeye; kila mtumishi wa umma awe na huruma, aone aah, hili halifai. Akatae safari hii au semina ile, aache posho ile au masurufu haya kwa sababu si vizuri -huruma!

Hakuna sheria na kanuni zinazoonyesha nani afanye nini na afanye vipi, na endapo atafanya ndivyo sivyo nini kitafuata. Hakuna.

Inawezekana Pinda hataki makuu, na kama anavyorejea kusema yu mtoto wa mkulima anayeona huruma kwa namna ‘mijitu’ inavyokula bila kunawa, inavyofisidi fedha za umma, ilivyokaa mkao wa kujinufaisha. Hawa posho nono zao, huduma bora wao, na kila kitu chema wao; hata kama kiasi kidogo kingetosha.

Hawajali kwamba ni vizuri fedha ndogo zilizopo zinufaishe wananchi kwa kupelekwa kule kunako tija nao. Zipo huduma zinazohitaji halan fedha ili kuhudumia wananchi kwa ufanisi.

Hakuna maji safi na salama, hakuna umeme, hakuna huduma bora za afya, hakuna barabara nzuri, hakuna masoko ya mazao, hakuna ulinzi madhubuti. Haya yanahitaji fedha kuyatimiza.

Zinatapanywa kwa viongozi kupenda anasa.

Si kweli kwamba serikalini watumishi ‘walafi’ hawawezi kudhibitiwa; si kweli kwamba Pinda hana nguvu hizo. Anazo kwa mujibu wa Katiba. Labda tu kama anajua anachokihofia?

Pengine ni wakati sasa Pinda aamue kubaki mpole na muungwana na hivyo kunyamaza au kuchangamka kwa kuwabana wabadhirifu. Hawezi kubeba yote. Awe mtoto wa mkulima lakini anaendekeza matanuzi serikalini. Haiwezekani.

Hana sababu ya kuogopa mijitu isiyoonesha kujali tatizo la umasikini. Katika mazingira hayo, naogopa kusema kwamba Pinda si muungwana ila kiongozi dhaifu wa kukabiliana na watumishi wanaotafuna kodi za wananchi.

Utendaji wake utapimwa kwa matendo yake siyo kwa kauli zake. Pinda anaapaswa kubadilika.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: