NINAKUANDIKIA Mama Salma Kikwete. Kwanza, nakusalimu na kukutakia shughuli na afya njema. Pili, nakupa pole kwa ziara yako ya wilaya ya Tarime
, mkoani Mara ulikokwenda kuwapigia magoti wananchi wa huko na kuwataka waache kuchinjana.
Bali hapa kuna kitu kimoja. Hawa watu hawachinjani kutokana na roho mbaya au imani za ushirikina. Wanachinjana kutokana na “ukapa.”
Bila kubadili aina ya uchumi wao watauana sana hata uwapigie magoti hadi yachubuke.
Hata hivyo, sikushangaa. Huu ndio ukweli wa maisha wanayoishi watu tulioahidi kupeleka Kanaani lakini wakajikuta wakizidi kutokomea Misri. Maana wamepigika kwelikweli ingawa sisi tunaotanua hatutaki kukubaliana na hili.
Hawa kwao kupata riziki ni lazima mtu avunje sheria. Huenda hii inatokana na wakubwa kujisahau na kutumia vibaya kama tulivyoshuhudia juzi kwenye sakata la Kagoda na Richmond.
Katika hili wakubwa wasio na roho na wenye roho mbaya na uchu wa fisi, waliamua kuua kashfa hizi ili kuwanusuru wenzao.
Sikupenda kuandika waraka huu. Nimelazimika kutokana na mapenzi yangu kwa taifa na hasa shughuli unazofanya ingawa haziwafurahishi wengine.
Maana kuna wanaosema eti umeaanza kumpigia kampeni mumeo hata kabla ya kipenga cha kufanya hivyo kupulizwa jambo ambalo nalipinga.
Watu hawa wasio na adabu wanahoji ni kwanini wewe, mumeo hata mwanae Ridhiwani Kikwete, muonekane sasa mikoani mkitoa misaada na nasaha wakati miaka minne iliyopita hamkufanya hivyo?
Wengine wanasema eti ni rushwa. Tangu lini wazito kama nyinyi mkatoa rushwa? Hayo ni maswali yao na roho zao mbaya.
Wapo wanaohoji bajeti ya ziara zako na kudai ziara zinahusisha misururu mirefu ya mashangingi; hata ya serikali.
Eti wanasema kufanya hivyo ni kuchafua mazingira na kuwaongezea mzigo walipa kodi na kujipachika madaraka usiyo kuwa nayo kikatiba.
Wengine wanasema eti ni matumizi mabaya ya ofisi ya mumeo kwa vile walimchagua yeye na kumwapisha yeye peke yake.
Hawa wanakosa hoja na hawana adabu. Wengine wanadai eti unatumia hata ndege ya mkuu wa nchi iliyonunuliwa kwa mabilioni ya shilingi na rais mstaafu Benjamin Mkapa.
Lakini mimi nakutetea kwamba hata kama unatumia, lakini unastahili. Wanaodai hivyo, ni wapinzani waliofilisika.
Mama, kusema ukweli hawa wanaokuandama wananiudhi kiasi cha kutamani kumtoa mtu roho kama siyo kuogopa kufungwa. Kwani wanahoji vitu visivyo na maana.
Eti wanauliza ni kwanini mlianzisha NGO ya WAMA (Wanawake na Maendeleo) baada ya mumeo kuwa rais na si kabla? Hawajui kama ungeianzisha kabla isingepata wafadhili wa maana?
Hawa naona hawana akili. Hivi hawaoni WAMA ilivyoleta maendeleo kwa wanawake wa Tanzania? Hawajui kuwa kulala watano kwenye kitanda kimoja wakati wa kujifungua pale Amana, Mwananyamala na Temeke sasa ni historia?
Hawajui hata wizi na kubadilishiwa watoto umepungua ukiachia mbali uhaba wa madawa kutokana na juhudi za WAMA?
Eti wanahoji ni kwanini wafadhili wako na matumizi na mapato ya ofisi yako hayafanyiwi ukaguzi wa hesabu na taarifa kuwekwa wazi.
Wanasema eti wengi wanaoifadhili NGO yako walikuwa wafadhili wa EOTF (Fursa Sawa kwa Wote) ya Anna Mkapa. Sasa hilo linawahusu nini?
Eti wanasema wanachangia “madaraka” si wewe. Hivi hawa wana akili kweli? Inakuwaje hawakuamini wewe mke wa kiongozi wao? Isitoshe, shughuli zako zinawahusu nini kama si wivu wa kipuuzi?
Wengine eti wanauliza ni kwanini kila shughuli ya WAMA inasimamiwa nawe na si wasaidizi wako? Kwani umewambia kuwa umechoka kiasi cha kuhitaji mtu mwingine kusimamia shughuli za asasi yako?
Kimbelembele. Nongwa. Umbeya. Kwani wanajua siri ya kuanzisha NGO hii? Si nao waanzishe kama zitapata wafadhili? Nani anaweza kuchangia, kwa mfano, NGO za watu wasiofahamika malengo yao?
Ninachokiona mimi ni hawa wabongo kukosa kazi ya kufanya kama ilivyosema serikali, kwamba “takribani nusu ya watu wanakula mara moja kwa siku.” Hii ndiyo maana wanahoji kila kitu.
Kwa vile wanaona wewe uko karibu na rais, au tuseme kweli uko kwa rais, wanadhani misafara yako ni sehemu ya haya matumizi, wakati si kweli.
Eti wanasema kuwa mke wa baba wa taifa Mama Maria Nyerere hakutenda kazi zake kama wewe. Mlinganisho huu unakujaje?
Lakini wakumbuke kitu kimoja. Zama hizi si zile za Nyerere. Sasa mambo yamebadilika sana. Kile kilichoitwa na Nyerere “siasa ya ujamaa na kujitegemea,” sasa hakijengwi tena. Bali sasa, kuna soko huria la kila kitu, ikiwamo siasa.
Na isitoshe wakati ule ufisadi ulipigwa vita kwa vitendo badala ya maneno matamu. Hivi sasa ufisadi ni sehemu ya maisha; si kwa viongozi pekee, bali hata kwa wananchi mmojammoja.
Hii ndiyo maana watu wana ufisadi wa kuhoji kazi zako tukufu. Isitoshe, Nyerere alikuwa akipoteza muda mwingi kwenye “maadili” badala ya “dili” kama ilivyo kwa marais waliofuata.
Pia wanapaswa kufahamu kuwa wakati wa Nyerere wanawake hawakuwa na matatizo mengi kama sasa kutokana na mambo kubadilika hasa baada ya mafisadi kukomba kila kitu.
Hivyo, kwa hali hii ambapo ubangaizaji ni lazima, sharti kuwepo pia NGO za wakubwa na wadogo; ndani na hata nje ya ikulu.
Hizi zitawasemea wanyonge na akina mama kutokana na wizara yao kushindwa kutekeleza ahadi zake kutokana na kushikiliwa na wanasiasa wakiwamo wasiomtakia mema mzee.
Mama naomba niishie hapa. Naogopa kukuchosha wakati una kibarua kizima cha kuzunguka nchi. Nakutakia afya njema na hawa wanaotishia misafara yako Mungu atawapeperusha.