Polisi wanaua, viongozi washerehekea


Paschally Mayega's picture

Na Paschally Mayega - Imechapwa 07 December 2011

Printer-friendly version

SIMANZI. Festo Andrea na mdogo wake Sumbuko wa kijiji cha Rungwempya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, mchana wa saa nane, walifanyiwa unyama.

Polisi wanane, wenye wajibu wa kulinda usalama, amani na haki za kuishi za vijana hao, waliwafungulia kutoka chumba walichokuwa wamefungiwa. Kilichofuata ni mateso yasiyomithilika.

Polisi hao waliwavua nguo zote vijana wale, wakaanza kuwapa kipigo kwa kutumia vitako vya bunduki, chupa za bia, na mbaya zaidi, wakawaingiza vijiti kwenye sehemu zao za haja kubwa hadharani, huku wananchi wakishuhudia pamoja na baba yao mzazi.

Polisi walipojiridhisha kwa unyama huo, waliwalaza ndani ya gari kifudifudi kisha wakawakandamiza kwa magunia manne ya mkaa juu ya migongo yao na kuondoka nao kuelekea Kasulu mjini.

Habari kama hizi za kuumiza, kuhuzunisha, kusikitisha na kufedhehesha sana zilisikika sana enzi za utawala wa Makaburu, Afrika Kusini.

Huko polisi walikuwa wakiwatesa, waliwaua kinyama watu weusi hasa wapigania uhuru ili wasitishe harakati za kusaka uhuru. Kwa kweli, tulishasahau habari hizi tangu siasa za ubaguzi wa rangi zilipokoma mwaka 1994 na shujaa Nelson Mandela kuwa rais wa kwanza mweusi.

Miaka 17 baadaye, polisi wa Tanzania wanatukumbusha unyama ule. Maskini, Festo Andrea alipoteza maisha kutokana na mateso hayo ya polisi huku mdogo wake, Sumbuko akivunda gerezani.

Daktari Said aliyechunguza mwili wa marehemu alisema Festo alikufa kutokana na kipigo kilichosababisha kupasuka bandama, michubuko usoni iliyosababisha kuvuja damu nyingi na jeraha kubwa sehemu ya kichwani. Hii inathibitisha jinsi marehemu Festo alivyouawa kinyama na polisi wa serikali.

Keshokutwa Watanganyika  wanaombwa kujitokeza kwa wingi kwenye kilele cha sherehe za Tanganyika au Tanzania Bara kutimiza miaka 50 ya kuwa huru.

Ni uhuru upi unaoweza kusherehekewa katika hali ya kinyama kama hii? Uongozi unaoheshimu maadili ungejiuzulu kutokana na makosa yaliyofanywa na watendaji walio chini yao.

Huko Rungwempya walienda kwa amri yao wenyewe? Hakuna kiongozi ambaye ameonyesha kuguswa na tukio la kusikitisha kama hili. Kuwaambia watu hawa hawa washerekee kwa sababu wamekuwa huru kwa miaka 50 sasa ni zaidi ya kuwatukana.

Waachieni viongozi wenu washerehekee uhuru wao na ninyi endeleeni na kuhangaika kwenu! Wote kuanzia Kamanda wa Polisi wa Wilaya (OCD) mpaka Waziri wa Mambo ya Ndani wote bado wapo ofisini kama vile hakuna tukio kubwa la kusikitisha lililotokea katika nchi!

Waziri mwenye dhamana, hata kauli tu ya mdomoni kulaani kitendo hiki hatoi? Bora kuku kuuawa kwake huchinjwa mara moja yakaisha. Hateswi kama hivi.

Afisa Mtendaji wa kijiji cha Rungwempya, Mosi Kilenge ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama amenukuliwa akisema amesikitishwa na kifo hicho.

“Festo alikuwa mchapakazi, hakuwa mlevi, hakuwa jambazi,” anasema Mzee Samba, baba mzazi wa Festo.

“Kitendo cha polisi kuwaingiza vijiti sehemu zao za haja kubwa watoto wangu wakiwa uchi wa mnyama na mimi nikishuhudia, kwa macho yangu, inanisikitisha sana. Tangu nizaliwe sijawahi kuona polisi wakifanya unyama wa aina hii. Naiomba serikali imwachie mtoto wangu Sumbuko anayeendelea kuteseka gerezani bila kosa lolote ili arudi alione kaburi la kaka yake kabla majani hayajaota.”

Keshokutwa wakati viongozi watakapokuwa katika majukwaa wakitazama magwaride na mbwembwe nyingi, ninyi pazeni sauti zenu, muwalilie huruma, wawaonyeshe uhuru wenu!

Hivi watu wangapi wanateseka magerezani kwa kesi za kubambikiwa na polisi? Wangapi wamekufa wakiwa wanaisadia polisi?

Unyama huu wa polisi, unakumbusha tukio la mwaka 2006 ambapo polisi wa serikali waliwateka vijana wanne wafanyabiashara ya madini wa Mahenge na dereva teksi mmoja eneo la Sinza, Dar es Salaam, wakawapeleka katika msitu wa Pande na kuwamiminia risasi visogoni bila hatia yoyote. Damu hii kwa hakika haitapotea bure!

Mahakama ilipopewa jukumu kuwatendea haki vijana wale, ikawaachia huru polisi wote waliohusika kuteka, kuwapeleka msitu wa Pande, kufyatua risasi, kurejesha maiti mochwari ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Eti ikadai si wauaji na wala hawakula njama za kuua; vijana wale walisifia wenyewe.

Yako wapi masikio ya serikali ya watu? Mtu atakuwa na furaha gani ya kufanya sherehe wakati vilio vya watu vimetamalaki nchi nzima?

Viongozi wetu wako radhi kutumia mabilion ya shilingi kufurahisha nafsi zao na familia zao kwa halaiki ya siku moja ya watoto wadogo huku madege ya kivita yakipita angani kwa sekunde chache, lakini hawajali maisha ya watu wao yanayopotea hospitalini kwa kukosekana dawa!

Wala viongozi hawa hawajali elimu duni inayotolewa kwa watoto wetu, wakiwa katika mavumbi kwa kukosa madawati na mahali pengine hakuna majengo. Bila kujali vijana wetu wanaonyanyasika kwa mikopo ya elimu ya juu.

Wafanyakazi wa chini wamepigika. Vijana hawana ajira nao hawaijui kesho yao. Wamachinga wanapigwa na kunyang’anywa hata kile kidogo walichonacho. Fahari ya fala isiwavunje moyo kwakuwa sasa Mungu amesikia kilio chenu!

Ole wao watu hao waliowafikisha hapo! Siku itafika jua litakapozuiwa kutoka mpaka nchi itakaporudishwa kwa Wananchi!

Nawahurumia trafiki wa Mbagala Rangitatu kwenye msongamano mkubwa wa magari. Mvua yao, jua kali lao. Nao wanashinda wakitafuna mavumbi ya barabara inayojengwa. Polisi wema wapo wengi lakini wanyama wachache wanalichafua jeshi zima.

Zamani siku kama ya keshokutwa tungeimba kwa furaha, uhuru na kazi, uhuru na umoja, uhuru na maendeleo! Leo kazi, umoja na maendeleo viko wapi? Vimekwenda. Tumebaki kulia na maisha magumu, dhuluma na uporwaji wa maliasili zetu na wageni kwa msaada wa viongozi wetu.

Tumekuwa kama watoto wa marehemu. Tunalia ngoa ganjoni tutasikiwa na nani? Basi na tuitazame milima, msaada wetu utatoka wapi?

0713334239, ngowe2996@yahoo.com
0
No votes yet