Posho: Unafiki au uzalendo?


Jacob Daffi's picture

Na Jacob Daffi - Imechapwa 14 December 2011

Printer-friendly version

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kinaendelea kujitundika msalabani. Ni kutokana na hatua yake ya kupinga nyongeza ya posho zilizopangwa kulipwa kwa wabunge wa Bunge la Muungano.

Taarifa ya Sektarieti ya Kamati Kuu (CC) ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho iliyotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, wiki iliyopita, inasema pamoja na mambo mengine, nyongeza mpya posho inayofikia Sh. 200,000 kutoka Sh. 70,000 ya awali, inayolipwa kwa wabunge wa Bunge hilo, “ni kinyume na maslahi ya umma.”

Nape anasema ni makosa kwa uongozi wa Bunge kuongeza posho hizo kwa kisingizio cha kupanda kwa gharama za maisha kwani ugumu wa maisha kwa sasa uko kila mahali nchini.

“Tunaamini busara itatumika kuachana na jambo hili, kwani kuendelea nalo kunaweza kutafsiriwa ni kuwasaliti watendaji katika sekta nyingine, wakiwamo walimu, askari, madaktari na wengineo,” imeeleza taarifa ya Nape kwa vyombo vya habari.

Alifika mbali zaidi kwa kumtaka Rais Jakaya Kikwete kutosaini waraka unaohalalisha kuwepo kwa nyongeza hiyo ya posho, akisema kisingizio cha kupanda kwa gharama za maisha kisitumiwe kuhalalisha utafunaji huo wa fedha za umma.

Badala yake hatua ya viongozi wa chama hicho kujitumbukiza katika mjadala wa posho, imekuja siku chache baada ya wanaharakati, viongozi wa kidini na baadhi ya vyombo vya habari kupinga ongezeko hilo la posho kama lilivyotolewa na Spika wa Bunge la Jamhuri, Anne Makinda.

Akitangaza uamuzi wa kupandisha posho za wabunge kutoka Sh. 70,000 hadi Sh. 200,000 kama posho ya kikao kwa siku, Makinda alisema ongezeko hilo limetokana na kupanda kwa gharama za maisha mjini Dodoma.

Hakuna mashaka kwamba uamuzi huo wa CCM, wa kuungana na wanaharakati na hasa viongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kupinga nyongeza hiyo ya posho, kunakidhoofisha chama hicho, badala ya kukiokoa. Sababu ni nyingi.

Kwanza, ni CCM na serikali yake iliyogeuza Bunge mradi wa kuchumia tumbo badala ya kuwa chombo cha uwakilishi.

Kwenye Bunge la Tisa, viongozi wakuu wa chama hicho, akiwamo Rais Kikwete mwenyewe, walikuwa mstari wa mbele kupinga mapendekezo ya Dk. Willibrod Slaa ambaye wakati huo alikuwa mbunge wa Karatu, mkoani Arusha, kupunguza posho za wabunge, hasa posho ya vikao.

Dk. Slaa alisema posho na marupurupu wanayolipwa wabunge ni makubwa mno; hayafanani na hali ya umasikini walionao wananchi waliowengi.

Wakati Dk Slaa akilaani jambo hilo, CCM na makada wake karibu wote walisimama pamoja, huku wakisisitiza kwamba ni vema wabunge wakalipwa vizuri ili kuwawezesha kufanya kazi zao. Walimkebehi Dk. Slaa kwa kusema, ni mroho wa madaraka anayetumia mwamvuli wa posho kujitafutia umaarufu.

Hata katika Bunge hili la sasa, serikali ya CCM kupitia kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda imepinga mara kadhaa mapendekezo ya CHADEMA kutaka kufutwa kwa posho za vikao kwa wabunge, badala yake fedha hizo zielekezwe kwenye miradi ya maendeleo, hasa umeme, elimu na afya.

Pili, suala la nyongeza ya posho kwa wabunge imejadiliwa na kupitishwa kwenye vikao halali vya Bunge, kikao cha kamati ya uongozi na kile cha kamati ya utumishi. Kwenye kikao cha kamati ya uongozi, kuna viongozi mbalimbali waandamizi wa chama hicho. Baadhi yao, wapo wajumbe wa Kamati Kuu (CC) na wengine ni watendaji wakubwa serikalini.

Miongoni mwa viongozi hao, ni Spika Makinda na Waziri Mkuu, Pinda. Makinda ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Bunge, chombo kikuu kinachosimamia shughuli za kila siku za Bunge, wakati Pinda anaingia kwenye chombo hicho kwa nafasi yake ya kuwa mkuu wa shughuli za serikali bungeni.

Wengine ambao ni wajumbe wa CC, ni Katibu wa NEC, Siasa na Mahusiano ya Kimataifa, January Makamba, ambaye anaingia kwenye chombo hicho cha Bunge kwa wadhifa wake wa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Nishati na Madini.

Katika orodha hiyo, yumo pia Dk. Abdallah Kigoda, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Fedha na Uchumi. Mwingine ni Jenista Mhagama, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Maendeleo ya Jamii. Jenista ni mjumbe wa CC kutokana na nafasi yake ya kuwa Katibu wa Kamati ya Wabunge wa CCM.

Hivyo basi, haiwezekani viongozi hawa wakapitisha uamuzi huo bungeni, kisha wakaupinga nje ya Bunge. Bila shaka kufanya hivyo, kutakuwa ni kusaidia upinzani ambao wanajulikana tangu mapema msimamo wao kuhusiana na jambo hilo.

Tatu, baadhi ya wajumbe wa sektarieti ya CCM waliojitokeza kupinga posho hizo, hawana mamlaka ya kutenda walichokieleza. Mfano hai, ni Makamba, Nape na John Chiligati, ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara).

Ifahamike kwamba January Makamba, kwa nafasi yake ndani ya CCM analipiwa na chama chake gharama zote za maisha anapokuwa Dodoma. Hapa haijalishi anafanya kazi za Bunge Au za CCM. Anapewa gari, nyumba, mafuta, dereva na analipwa posho ya kujikimu na chama chake hicho.

Taarifa zinasema kwa kila siku ambayo Makamba na wenzake hao –Chiligati na Mwiguru Mchemba, ambaye ni katibu wa uchumi – wanapokuwa nje ya Dar es Salaam, wanalipwa na chama chao posho ya kujikimu ya kati ya Sh. 140,000 na Sh. 180,000 kwa siku.

Kiasi kama hicho ndicho pia anacholipwa Nape anapofanya ziara ya kikazi mikoani. Hata hivyo, pamoja na kugharamiwa na ofisi yake safari zake mikoani, kila mkoa anakokwenda kiongozi huyo, viongozi wa chama chake kwenye mikoa husika hulazimika kumhudumia na kulipia gharama za safari yake.

Je, katika mazingira haya, uko wapi uadilifu wa Nape na viongozi wenzake wanaopinga nyongeza hiyo ya posho kwa wabunge?

Kutokana na hali hiyo, uamuzi wa chama hicho kupinga nyongeza ya posho utakuwa umefanywa kwa kukurupuka baada ya kupima hasira za wananchi dhidi ya serikali yake; hiyo haiwezi kuiondoa CCM katika lawama, tuhuma na shutuma za kupanda kwa posho hizo na ugumu wa maisha walionao wananchi.

Busara ya kawaida ingewaongoza CCM kuliacha suala hilo ndani ya utaratibu wa Bunge na ndani ya mamlaka ya rais, ambaye pia ndiye mwenyekiti wa chama hicho, badala ya kujiingiza kichwakichwa.

Kitendo cha CCM kutunisha misuli leo na kudai kwamba nyongeza ya posho hiyo “ni kinyume na maslahi ya umma,” ni usanii na unafiki mkubwa. CCM gani hiyo ya kujali maslahi ya umma wakati imekuwa mshirika mkuu wa mafisadi na vibaraka wao? Yuko wapi anayeweza kusema, “CCM inapenda wananchi kuliko wale wanaohasidi nchini?”

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: