PPF yanufaisha SACCOS kwa mikopo


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 15 June 2011

Printer-friendly version

MFUKO wa Jamii wa PPF umeinua juu bango kubwa la ushahidi wa mafanikio yake na yale ya  wanachama wake.

Mwanachama ana mafao yake kutoka kwenye mfuko. Haya ni kwa mujibu wa haki yake kisheria. Pili, ananufaika na mikopo kutoka mfuko huu wa pensheni pale anapokuwa mwanachama wa SACCOS iliyochukua mkopo PPF.

Ni utaratibu huu ambao baadhi ya walionufaika nao wanaita, “Mafao Mara Mbili.”

Shahidi wa 31 katika kutangaza mafanikio ya  utaratibu huu ni Alaf SACCOS Limited. Juzi, Jumatatu SACCOS hiyo ilipata mkopo wa Sh. 950 milioni.

Ukiwa mwanachama wa PPF na huku ukawa mwanachama wa SACCOS ya wanachama wa PPF, basi unakuwa na “Mafao Mara Mbili” yanayotokana na kile wanachama wanaita, “Mpango Mapacha.” Huku ndiko kunufaika mara mbili.

Sasa Alaf SACCOS Limited ya jijini Dar es Salaam ndiyo imekuwa SACCOS ya 31 nchi nzima kupokea mkopo wa PPF.

Kwa wale wanaofahamu kuwapo mpango huu na waliowahi kunufaika nao, wanafurahi kuona wenzao nao wanapata. Wale waliofahamu muda mrefu, wako katika maandalizi ya kukidhi masharti ya kupata mkopo.

Lakini hali yaweza kuwa tofauti kwa wale wasiojua mpango huu wakati wao ni wanachama tu wa PPF. Hao wanaweza kufikiri kuwa hii ni “bahatinasibu.” Sivyo!

Ni matokeo ya maandalizi na kukidhi matakwa ya mkopo. SACCOS ambayo wanachama wake ni wanachama wa PPF na wanachangia mfuko huo – siyo uanachama wa jina tu – ina sifa za kuzingatia kabla ya kukopeshwa.

Ili uwe na SACCOS sharti uwe umesajiliwa kwa mujibu wa sheria na kanuni za ushirika nchini. Uhalali huo kisheria, uanachama wako katika SACCOS na uanachama wako hai katika PPF, vinakuweka wewe, na wenzako, karibu na mkopo wa Mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma.

Kuna sifa nyingine. SACCOS yako iwe na umri usiopungua miaka mitatu; yenye hitoria ya utendaji bora, vitabu vya hesabu vinavyokaguliwa na vilivyo “safi” kwa maana ya kuthibitishwa na mkaguzi mwenye sifa kitaaluma.

Ukiwa na haya yote, tayari unakuwa karibu na “Mpango Mapacha.” Kuna sifa nyingine ambayo unapaswa kuwa nayo pia.

Pale ambako kuna SACCOS ambamo wewe ni mwanachama, pasiwe miongoni mwa kampuni au mashirika ya serikali yaliyoko kwenye mpango wa kubinafsishwa. Basi!

Kwa sifa hizi, kila mwenye nia atakubali kuwa hakuna masharti magumu; bali kuna maelekezo yanayozingatia taratibu mwafaka za kulinda fedha za wanachama na Mfuko.

SACCOS ni utaratibu wa “kuweka na kukopa” kwa wanachama wake. Kwa hivyo, SACCOS ni benki za wanachama.

Unaweka ili kujenga mtaji; unakopa ili kukidhi mahitaji ya shughuli zako – ikiwa ni pamoja na kuzalisha ili uweze kurejesha mkopo na kujenga mtaji au kukuza benki yako.

SACCOS ni benki za wanachama zinazoendeshwa kwa riba nafuu kulingana na uwezo wa wanachama wake. Hili la riba nafuu linazingatiwa pia na PPF katika mikopo yake kwa SACCOS.

Hii ndiyo maana tangu kuzinduliwa kwa mpango wa kukopesha, mwaka 2004, PPF imevuta SACCOS 31 sasa na kutoa mikopo ya thamani ya Sh. 28.6 bilioni.

Masharti nafuu ambayo PPF inatoa kwa SACCOS, siyo tu ni mwafaka na mepesi, bali pia yanachochea SACCOS kujichunguza, kijiimarisha na kujiweka katika mazingira bora ya utawala kifedha ili ziweze kufaulu kukopa.

PPF haitozi SACCOS gharama za kuwasilisha maombi ya mkopo. Haitozi kiwango chochote kwa kulinda heshima ya ahadi (commitment fee) ya kuchukua mkopo. Haitozi gharama zozote kwa kushughulikia maombi ya SACCOS.

Lakini watoa mikopo wengine nchini hutoza gharama zote hizo na hata riba ya kati ya asilimia 18 na 25 kwa mwaka. Riba kubwa, kwa viwango vyovyote vile.

Kana kwamba huo si mzigo mkubwa, watoa mikopo hao hutaka fedha zao zirejeshwe kati ya mwaka mmoja na miaka mitatu. Ni mzigo mwingine mkubwa.

SACCOS zilizokopa PPF zinachekelea. Zinatozwa riba nafuu ya asilimia 12 kwa mwaka; na mkopo unarudishwa katika miaka mitatu hadi mitano. Tayari waliokopa wanasema, “Hii ni bwerere!”

Kwa hiyo, chini ya Mpango Mapacha wa mikopo kwa SACCOS, utakuta riba nafuu, muda mrefu wa kurejesha mkopo, makato madogo kwenye mshahara au mapato yako; na uhuru wa kufikiri na kutenda bila msongamano wa mawazo ya kulipa haraka au woga wa kufilisiwa.

Meneja Mahusiano wa PPF, Lulu Mengele anasema  SACCOS nyingi zimeelewa umuhimu wa mpango wa mkopo na kwamba vikao vya kukabidhi hundi kwa SACCOS zilizotimiza masharti vitakuwa vikisikika mara kwa mara.

Anasema waliopata mikopo ndio mabalozi wa wanachama wa SACCOS zenye mafanikio na kwamba mafanikio yao ni kichocheo kwa wale ambao hawajafikisha umri wa kukopa au wanaojiandaa kukopa.

“Kwa vyovyote vile, PPF inajivunia kuwa sehemu ya wanachama wake wanaonufaika na mikopo nafuu iliyolenga kuboresha maisha yao na jamii kwa upana wake,” amesema Mengele.

PPF ndio mfuko wa jamii peke yake nchini unaotoa mikopo kwa SACCOS za wanachama wake zilizoanzishwa maeneo ya kazi. Baada ya Alaf SACCOS Limited, nani?

0
Your rating: None Average: 4 (1 vote)