Profesa Mtulia: Elimu ni changamoto kubwa Rufiji


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 21 July 2009

Printer-friendly version
Ana kwa Ana

NI hazina. Ni lulu. Si mwingine, bali ni Profesa Idrissa Ali Mtulia, mbunge wa Rufiji, mkoani Pwani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Profesa Mtulia, ni mmoja wa wabunge wachache kutoka kundi la wabunge wa mkoa huo, waliobahatika kupata elimu ya juu na kuitumia elimu yao kwa manufaa ya wananchi.

Ndani na nje ya Bunge, Profesa Mtulia hachoki kuzungumzia matatizo ya wananchi wa jimbo lake na mkoa wa Pwani kwa jumla.

Hiki ni kipindi cha kwanza cha ubunge kwa Profesa Mtulia, lakini utadhani amekaa bungeni kwa miaka 20 kutokana na uzito wa hoja anazozijenga.

Katika mahojiano na MwanaHALISI majuzi, mjini Dodoma, Profesa Mtulia, pamoja na mambo mengine, anasema, "wananchi wa mkoa wa Pwani wako nyuma kimaendeleo. Ni wachache waliobahatika kupata elimu, ukilinganisha na wananchi wa mikoa mingine."

Profesa Mtulia aliyefanya kazi serikalini kwa miaka mingi, hadi kufikia ngazi ya katibu mkuu wa wizara ya afya kutoka mwaka 1995 hadi 2001, anasema anatamani kugombea tena ubunge, lakini "maamuzi ya mwisho yatakuwa ya wananchi."

Anasema, "Ukiniuliza mimi, nitakwambia mara moja kwamba nitagombea tena kipindi cha pili. Lakini wenye uamuzi wa mimi kugombea, au kutogombea ni wananchi wenyewe."

Moja ya sababu kubwa ambayo inamfanya Profesa Mtulia kutamani kugombea tena ubunge jimboni kwake, ni kukosekana kwa maendeleo wilayani Rufiji na uduni wa maisha kwa wananchi wake.

Anasema, "miaka ya nyuma, Rufiji ilikuwa inajitosheleza kwa chakula na kuna wakati chakula kilikuwa kinauzwa nje ya wilaya yetu. Lakini sasa, Rufiji haijitoshelezi hata kwa chakula chake yenyewe."

Mazao ya mpunga, mahindi na mihogo, ambayo yalikuwa yakilimwa kwa wingi Rufiji, sasa yamebaki historia. Anasema, kilimo kilichokuwa kimeshamiri, hivi sasa kimeshuka kutokana na ukosefu wa zana za kisasa za kilimo.

"Udongo wa Rufiji, ni wa aina yake. Huwezi kuendesha kilimo kwa kutumia jembe la mkono au plau (jembe la kukokotwa na ng'ombe). Unaweza kuendesha kilimo Rufiji kwa kutumia trekta tu. Kukosekana kwa zana hizi za kisasa, ndiko kulikorudisha nyuma kilimo chetu," anasimulia kwa uchungu Profesa Mtulia.

Anasema mji wa Utete, ambako ndiko iliko hospitali ya wilaya na makao makuu ya wilaya ya Rufiji, ulikuwa angalau na umeme wa jenereta. Lakini hivi sasa mji wote upo gizani baada ya jenereta iliyokuwapo kuharibika.

Anasema hata barabara za uhakika za kuunganisha wilaya hiyo na wilaya nyingine zimekufa.

Hata hivyo, Profesa Mtulia anajivunia juhudi zake za kufufua umeme katika wilaya hiyo. "Mipango ya kurudisha umeme Utete imekamilika. Kuna mradi mkubwa wa umeme na tayari nyaya zimeshasambazwa katika maeneo husika," anasema.

Anasema: "Umeme huu, hautawafaa wananchi wa Utete tu, hapana. Utafika hadi Kiwanga, Chumbi, Utunge, Nyandakatundu hadi Kindwiti. Ni mradi mkubwa, na kwa hakika, wa aina yake kwa wananchi wangu."

Profesa Mtulia anasema, anataka kuiona Rufuji ikipata maendeleo makubwa. Anataka kuona Rufiji inapiga hatua za maendeleo kwa haraka, kutoka shule sifuri hadi makumi ya shule za sekondari za kidato cha kwanza hadi cha nne.

Anataka shule za sekondari za Muhoro, Utete, Ikwiriri, Nkongo, Kibiti, Rwauluke, Mahege na Kibiti, ambazo zimeishia kidato cha nne, zifikishe kidato cha sita.

"Ndoto yangu ni kuona angalau Rufiji inakuwa na shule japo mbili za kidato cha tano na sita, kabla ya mwaka 2011," anasema.

Anasema, "Mbali na kuwa hatuna shule za kidato cha tano na sita, hata hizi shule tulizonazo hazina walimu wa kutosha wa kufundisha. Kuna shule zina mwalimu mmoja tu."

Mbali na tatizo hilo, Profesa Mtulia anasema hata walimu wa kufundisha masomo ya sayansi, hawapo katika shule hizo.

Rufiji ndiyo kwanza imeanza, na hakika, utadhani ni wilaya iliyoanzishwa jana. Maendeleo yaliyokuwapo kabla na baada ya uhuru, sasa hayaonekani kutokana na viongozi waliokuwapo kushindwa kuyaendeleza.

Barabara zinazounganisha Rufiji, zilikuwa hazipitiki. Lakini angalau sasa, barabara ya Kibiti, Mkongo, Utete-Nyamwage, pamoja na kwamba haijajengwa kwa kiwango cha lami, angalau inapitika ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Hata barabara ya Ikwiriri, Mkongo, Mloka, Vikumbulu, Kisarawe, Bagamoyo-Tanga, inayoweza kupitisha magari yatokayo mikoa ya kusini kwenda Morogoro, Dodoma, Tanga, Arusha hadi nchi za Kenya, Rwanda na Burundi, iko mbioni kujengwa.

Profesa Mtulia anasema barabara hiyo, tayari imechukuliwa na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads). Kabla ya kujengwa kwa "Daraja la Mkapa," barabara ya kusini ilikuwa inapitia Utete.

Anasema, "Njia hii sasa imekufa kutokana na kuharibika kwa kivuko cha Utete. Tayari serikali imetenga fedha za kununua kivuko kipya cha Utete chenye uwezo wa kubeba abiria 200 na tani 50 za mizigo."

Barabara ya kutoka Ndundu hadi Somanga ambayo ina ukubwa wa kilomita 60 imeanza kujengwa. Profesa anasema, "barabara zilizobaki ni zile za wilaya, ambazo zitajengwa kupitia mfuko wa barabara."

Hata barabara ya Kipatimu kwenda Nyamwage, Nambunju, Muhoro hadi Ndundutawa, ambayo ina ukubwa wa kilometa 80, na ile ya Muhoro hadi Ruma, nazo zimeahidiwa kujengwa katika mwaka huu wa fedha.

Kuhusu miradi ya maji, Profesa Mtulia anasema tayari kuna mradi mkubwa wa maji unaofadhiliwa na Benki ya Dunia.

Vilevile, serikali imekarabati jengo la mkuu wa wilaya ya Rufiji ambalo lilijengwa na utawala wa Kijerumani kwa zaidi ya Sh. 400 milioni.

Wilaya ya Rufiji inaungana na wilaya ya Morogoro Vijijini, kupitia mbuga ya wanyama ya Selous na mkoa wa Lindi, kupitia wilaya za Kilwa na Liwale.

Profesa Mtulia aliwahi kuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kuanzia mwaka 2002 hadi 2007. Ameoa na ana watoto sita.

0
No votes yet