Rais ajiuzulu kwa kashfa ya elimu


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 04 April 2012

Printer-friendly version

RAIS wa Hungary, Pal Schmitt amejiuzulu urais na kitu kilichosababisha ateme madaraka yake kutokana na kashfa ya elimu yake.

Schmitt amechukua uamuzi huo siku chache tu tangu ajiapize kuwa hataweza kujiuzulu nafasi hiyo kutokana na shutuma za kuiba maandishi ya watu wengine na kuyatumika katika sehemu ya tasnifu yake ya shahada ya udaktari wa falsafa.

Wapinzani wake walitoa wito wiki iliyopitaajiuzulu mara moja kwa kashfa hiyo.

"Katika hali kama hii, wakati masuala yangu binafsi yanasababisha mgawanyiko katika nchi ninayoipenda sana badala ya kuwa kitu kimoja, naona ni wajibu wangu utumishi wangu uishie hapa na kujiuzulu,” alisema alipohutubia Bunge juzi Jumatatu.

Hata hivyo, Schmitt alisisitiza kwamba dhamiri yake iko safi akirudia kauli aliyoitoa wakati wa mahojiano na ambayo ilitangazwa Ijumaa iliyopita katika televisheni ya serikali.

Rais huyo alisema alikuwa tayari kwenda mahakamani kuthibitisha kuwa yuko sahihi.

"Niliandika tasnifu kwa kutumia elimu na weledi wangu wakati ule na wala sikukusudi kuchukua maandiko ya mtu. Hata hivyo, nitakubaliana na uamuzi wowote wa (Chuo Kikuu) Seneti kwamba kimesitisha shahada yangu ya uzamivu. Lakini hili halina uhusiano wowote na mimi kuwa rais," alisema Ijumaa.

Schmitt, bingwa wa zamani wa Olimpiki katika mchezo wa vitara, alitayarisha tasnifu yake mwaka 1992 katika Chuo Kikuu cha Elimu ya Viungo ambacho ni sehemu ya Chuo Kikuu cha Semmelweis jijini Budapest.

Lakini Januari 2012, gazeti la HVG linalotolewa kila wiki liliripoti kwamba sehemu kubwa ya tasnifu ya Schmitt ilinakiliwa.

Uchunguzi uliofanywa na chuo kikuu uligundua kwamba sehemu kubwa ya tasnifu ya rais huyo ni maandiko ya watu wengine. Kamati iliyokaa wiki iliyopita imesema zaidi ya kurasa 200 katika tasnifu hiyo yenye kurasa 215 ilionyesha “mfanano kiasi” na kazi nyingine au ilikuwa tafsiri ya moja kwa moja.

Baada ya chuo hicho kujiridhisha na uchunguzi wake, Alhamisi iliyopita kiliamua kumvua shahada hiyo.

Waziri mkuu, Viktor Orban alisema ilikuwa juu ya rais huyo kuamua cha kufanya.

"Hakuna mtu mwingine zaidi isipokuwa yeye pekee ndiye anaweza kufanya uamuzi,” alisema Orban katika mahojiano redioni Ijumaa iliyopita.

Schmitt alichaguliwa na Bunge kuwa rais kwa kipindi cha miaka mitano mwaka 2010.

Kashfa kama hii ilimkumba waziri wa ulinzi wa Ujerumani mwaka jana ambaye naye alijiuzulu.

Karl-Theodor Freiherr zu Guttenberg alijiuzulu nafasi ya siasa Machi 2011, akisema "anachukua uamuzi huo ambao natarajia hata wengine watachukua."

0
No votes yet