Rais wangu, mengine unajitakia


Paschally Mayega's picture

Na Paschally Mayega - Imechapwa 15 June 2011

Printer-friendly version

RAIS wangu Jakaya Kikwete, viongozi waliobaki na heshima yao katika jamii yetu sasa ni viongozi wa dini zetu.

Hawa ni wanadamu kama wengine, ndiyo maana baadhi yao hupatikana na makosa ya kibinadamu kama wengine. Wala hii haijawahi kuwaondolea heshima katika jamii kwa ujumla wao.

Lakini lilikuwa kosa kubwa kuwaunganisha wote kwa ujumla wao katika kufanya dhambi ya biashara ya madawa ya kulevya. Haikuonyesha kuwaondolea heshima tu katika jamii, bali pia inaonyesha udhaifu mkubwa kwa mtu aliyepewa mamlaka ya kukamata wahalifu, naye badala ya kuwakamata anaishia kuwalalamikia haohao anaoona kuwa ni wahalifu. Huku si kufaulu katika uongozi, ni kushindwa.

Rais wangu, kiongozi huzaliwa kiongozi, hatengenezwi. Vitabu na masomo ya darasani humsaidia mtu aliyezaliwa kuwa kiongozi kuwa kiongozi bora zaidi. Uprofesa au Udokta kwa kiongozi aliyejifanyisha ni sawa na shada la maua mazuri juu ya kaburi la zamani. Maua hayasaidii maiti iliyoko kaburini bali kufurahisha macho ya watu wengine kabisa wanaolitazama kaburi.

Katibu Mkuu wa Shura ya Maimamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda alisema kabla ya rais kutoa kauli hiyo aliyoiita ni ya kulalamika kwa wananchi, alitakiwa kuwakamata kwanza hao viongozi wa dini kisha auambie umma wa Watanzania kuwa nao wanajihusisha na biashara hiyo. Ponda alitoa kauli njema kabisa. Kwa nini ulalamike badala ya kuchukua hatua?

Rais wangu, ni hivi karibuni tu ulipokuwa Dodoma ukiwalalamikia wananchi kuwa mawaziri uliowateua ni wazinzi, walevi, hawaendi kwa wananchi na wanaishia ofisini kuangalia video.

Wananchi wakauliza unataka wakusaidieje? Wanayemtegemea atatue malalamiko yao na yeye anawapelekea malalamiko yake! Baba anayemwongoza mwenzake hapa nani? Kuwalalamikia wananchi ni kuwaonyesha kushindwa kwako kuwaongoza.

Rais wangu, Makamu Mwenyekiti wa CCT, Askofu Dk. Valentino Mokiwa alisema kauli ya Rais Kikwete imewasikitisha kwa kuwa amewahusisha viongozi wote wa dini jambo ambalo si zuri mbele ya jamii.

Alisema, “Rais ataje majina ni kina nani wanahusika na ndani ya saa 48 awe amewataja la sivyo itakuwa aibu zaidi kwake na serikali.”

Inasikitisha kuona mpaka wakati huu Rais ameshindwa kutaja viongozi wa dini wanaojihusisha na biashara ya madawa ya kulevya. Mtumishi wa Mungu alisema Rais akishindwa, itakuwa ni aibu kwake na kwa serikali. Na hivi ndivyo inavyokuwa. Aibu hii katika nchi mpaka lini?

Kwa kauli hii ya Rais Kikwete, Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba anahoji, kama rais anapata ujasiri wa kusema hayo, anakosaje ujasiri wa kuwakamata? Alisema serikali haiko makini katika vita dhidi ya madawa ya kulevya.

Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia amesema, “Rais ameendelea kuimba ngonjera kila siku. Leo viongozi wa dini, kesho ni wewe mwandishi, siku nyingine waganga wa kienyeji. Kama anawajua anasita nini kuwachukulia hatua?”

Baba, hawa ni viongozi wetu, wanashaka na utendaji wako. Hauwaridhishi.

Rais wangu, kauli za viongozi hawa zinakuachia hadhi gani kwa wananchi unaowaongoza? Je, hazionyeshi kuwa mbele ya wananchi tumeonyesha hatuwezi kuongoza?

Ni juu yetu viongozi kuweka wazi kwa wananchi tofauti kati ya kiongozi mweledi na kiongozi maamuma. Matendo na maneno ya viongozi wao ndiyo huwasukuma wananchi kuwaita viongozi wao weledi au maamuma.

Askofu mmoja wa Anglikana alizungumza kwa masikitiko makubwa kwamba Rais amedhalilisha na kuwakosea adabu. Alisema, “Kwa kweli Rais ametudhalilisha, hakututendea haki, ametukosea heshima kwani alichotakiwa ni kumtaja huyo anayedhani anajihusisha na biashara hiyo lakini si kutaja kwa ujumla wetu.”

Rais wangu, wakati Baba Askofu huyu analalamika zikaja habari za nguvu ‘Rais Kikwete awajibu Maaskofu kabla ya saa 48’. Tukasema ‘Safi’, Rais wetu hataki mchezo. Mawe!

Kumbe lilikuwa tamko kutoka Ikulu sijui kwa nani, kuwa wale wanaojishuku wajisalimishe badala ya kusubiri rais awataje. Tamko likasema, “Mtu akikuonya kuwa nyumbani kwako kumeonekana nyoka huanzi kwa kuuliza kama ni kweli, ni wa rangi gani….” Ikulu ya sasa ina watu wengi!

Maaskofu walichotaka kwa Rais ni majina kama anayo. Anayejishuku ajisalimishe siyo jibu. Rais ameulizwa anaitwa nani? Anayemjibia anasema Rais anakaa Ikulu.

Huyu aliyejibu amedhihirisha hakuelewa walichosema maaskofu. Lakini pia, amethibitisha kuwa hata kile ambacho Rais wake aliwaambia maaskofu, nacho hakukielewa.

Kwa kutumia mfano wake, Rais hakuwaambia maaskofu kuwa nyumbani mwao kuna nyoka. Rais aliwaambia maaskofu kuwa wao ni nyoka. Maaskofu wanakataa kuwa ni nyoka. Wanamtaka rais awataje kwa majina maaskofu ambao yeye anawajua ni nyoka.

Unapoona kufanya hivyo ni sawa na kuuliza ni wa rangi gani jua uelewa wako kwa jambo hilo ni mdogo. Ni bahati mbaya kutumia uelewa mdogo kama huo kumjibia mkuu wa nchi. Unapotosha hadhi na weledi wa Rais. Sasa wanasema Rais kaulizwa unaitwa nani, kajibu ‘nakaa Ikulu’.

Rais wangu, maaskofu waelewe kuwa waliosema “mtoto akililia wembe mpe” hawakuwa wajinga. Katika shughuli za kidini, kiongozi wa serikali inamhusu vipi? Mtu hawezi kusali mnamwita aje afanye nini? Tunaziheshimu dini zote ili tukae kwa amani basi.

Tunajua Mungu ni mmoja lakini kila mtu ana imani tofauti kulingana na dini yake. Muumini wa kweli na anayeijua vizuri dini yake anaamini dini ya haki, dini ya kweli mbele ya Mwenyezi Mungu ni ile anayoiamini. Na hii ndiyo akili ya mtu mwenye akili timamu.

Rais wetu ni muumini wa kweli wa dini yake ya Islamu. Anawapenda watu wake ndiyo maana anaheshimu dini zao, lakini hawezi kuzitumikia. Kumwita Rais wetu aende kanisani ni kumkosea kiimani. Kwa kuwa anawaheshimu mkimwita anakuja, lakini kanisani huyu si mahali pake.

Sioni kama kuna tofauti kwake akiangalia pilikapilika zinazofanywa na wanaomtawaza mtu kuwa askofu na pilikapilika anazoziona akialikwa katika filamu za Bongo. Ni mwanasiasa, kaona kapewa jukwaa kapiga siasa, kuna ubaya gani? Hapa sioni kosa la rais wangu.

Baba wakikuita tena nenda kawapige na jingine. Waliyataka wenyewe. Msituchonganishe na rais wetu bure tukadhani hawaheshimu viongozi wetu wa Kikristu.

Imeandikwa wazi kuwa, “Nyumba ya Baba yangu si pango la walanguzi”. Hivyo si vema na si haki hata kidogo nyumba ya Bwana kuingiwa na wasiomkiri Kristu Yesu kuwa ni Mwana wa Mungu.

Kuwatengea mahali na viti maalumu viongozi wa kisiasa kanisani, hakuwezi kumpendeza Mungu. Kuwatofautisha wanadamu kwa ubora ni kukosoa kazi yake! Waliofananishwa na Mungu mwanadamu asiwatofautishe!

Tel: 0713334239, ngowe2006@yahoo.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: