Regia alifanya mengi makubwa


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 18 January 2012

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii

REGIA Estelatus Mtema hatunaye; ametutoka ghafla na kuacha majonzi. Ajali mbaya aliyopata saa 5.30 hivi Jumamosi iliyopita eneo la Ruvu mkoani Pwani ndiyo imepora maisha yake. Anatarajiwa kuzikwa kwao Ifakara, Kilombero.

Wazazi wanalia, ndugu na jamaa wanalia; waliokua, kusoma, kufanya kazi naye wanasikitika. Wanasiasa hasa wanachama, wafuasi na viongozi wa chama chake – Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wanaombeleza kumpoteza mbunge huyo kijana na mpambanaji.

Regia (32) atakumbukwa kwa mengi aliyofanya. Julai 2009 alipoamua kutangaza, kupitia gazeti hili, nia yake ya kuwania ubunge katika uchaguzi mkuu mwaka 2010 Jimbo la Kilombero mkoani Morogoro, alisema kuwa anakwenda kupambana siyo kuwa msindikizaji.

“Sitagombea kwa maana ya kugombea tu. Siendi kusindikiza wengine. Nagombea ili kushinda. Mimi siko tayari kuwa msindikizaji. Ninajiamini nina uwezo mkubwa wa kufanya kazi. Tatizo kubwa lililopo ni kutokuwa na uchaguzi huru na wa haki,” alisema Regia katika mahojiano yaliyochapishwa katika toleo la Julai 8-14 2009.

Alisema, “Nimeamua kuwania ubunge ili niweze kupata fursa ya kueleza hisia zangu katika masuala ya haki kwa wenye ulemavu.”

Hii ndiyo sababu, ulipofanyika uchaguzi mkuu na hasa yalipoanza kutangazwa matokeo ya ubunge, masikio yetu yalikuwa Kilombero. Taarifa za awali zilisema binti huyo alikuwa anaelekea kunyakua kiti ikiwa hakutakuwa na mizengwe hatua za mwisho.

Lakini baada ya matokeo kucheleweshwa kutangazwa kwa siku mbili, mchezo ulikwishakamilika, Abdul Rajab Mteketa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) alitangazwa mshindi kwa kura 40,000 huku Regia akijikusanyia kura 38,550.

Regia hakukata tamaa na wala hakuona haja kupinga matokeo hayo mahakamani. Chama chake kilipompa nafasi ya kuwa mbunge wa Viti Maalum, alijua hiyo ndiyo nafasi ya kuwathibitishia wananchi wa Kilombero kwamba walikosea kumnyima kura za kutosha.

Bungeni, yeye na mbunge mwingine wa Viti Maalum kupitia CCM, Mchungaji Dk. Gertrude Lwakatare walitia fora kwa uchangiaji wao na kumfunika Mteketa. Kuna wakati watu walihoji yuko wapi Mteketa?

Kila aliposimama kuchangia bungeni ama Lwakatare au Regia alionyesha uchungu hasa namna wafugaji kutoka mikoa ya kaskazini wanavyochukua maeneo ya wenyeji-wakulima tena kwa nguvu.

Wakati Lwakatare hutumia lugha ya kichungaji kuiomba serikali iwaonee huruma wenyeji na kuwapatia ulinzi kwani kuna wakati wanacharazwa bakora na wafugaji wenye miraba minne, Mtema alifikia kutoa kauli nzito akitaka wageni hao waondoke.

Baada ya kusikiliza marudio ya vipindi vya Bunge usiku wa siku aliyotoa tamko hilo , alipotafakari ukali wa lugha aliyotumia, siku iliyofuata asubuhi Regia aliomba radhi Watanzania wote kwamba kauli yake haikuwa ya kizalendo. Wabunge na jamii walimsifu mbunge huyo kwa ujasiri aliouonyesha kuomba radhi.

Regia, aliyeuzoea ulemavu huo wa mguu wa kulia tangu akiwa na umri wa miaka saba hakuwa mwoga; mara zote amekuwa bega kwa bega na chama chake. Kwanza aliaminiwa na akateuliwa kuwa ofisa mwandamizi katika Kurugenzi ya Vijana halafu akawa ofisa mwandamizi katika Kurugenzi ya Mafunzo. Hadi anafariki dunia alikuwa mjumbe wa Kamati Kuu na Waziri Kivuli wa Kazi na Ajira.

Siku ambayo Rais Jakaya Kikwete alikwenda Dodoma kuzindua Bunge, Regia aliungana na wabunge wote wa CHADEMA kususia hotuba hiyo ya kwanza kwa mkuu wa nchi. Walitoka nje licha ya kuzomewa na wabunge wa CCM.

Kama ilivyokuwa kwa wabunge wengine wa CHADEMA, alipigania hali bora ya maisha kwa Watanzania na pale ilipolazimu kupinga jambo kwa hoja au kwa kutoka nje ya bunge au kwa kuandamana, hakuwa nyuma.

Kila alipohitajiwa na chama chake, aliitikia haraka bila kusita. Ameshiriki mandamano ya CHADEMA Kanda ya Ziwa, Nyanda za Juu Kusini katika kupigania haki za Watanzania na alishiriki sakata la kuvuliwa uanachama madiwani kusaka muafaka Arusha.

Bungeni alipigania kushushwa bei ya sukari. Hakuelewa kwa nini Kilombero, wilaya inayozalisha sukari kupitia kiwanda cha Illovo, bei ya sukari iwe juu.

Vilevile, alipigania utekelezaji wa huduma bure kwa wajawazito, watoto chini ya miaka witano, wazee na wenye ulemavu, kero ya wakulima na wafanyabiashara ya kuongezeka kwa ushuru.

Alikuwa anasomesha wanafunzi 86 shule za sekondari, na alisaidia wanafunzi 13 wa vyuo vikuu, aliezeka madarasa mawili shule ya msingi Mkula, na akawa sehemu ya kufanikisha uzinduzi wa Chuo Kikuu Kishiriki Cha Mtakatifu Fransisco.

Huduma nyingine alizotoa ni kugahrimia visima viwili vya maji,  akamhudumia baba aliyekuwa kipofu kwa miaka minane akaweza kuona tena kupitia hospitali ya CCBRT na amesaidia wagonjwa zaidi ya 42 wakapata huduma za afya na kupona.

Hakusahau vijana. Aliwasaidia jezi vijana katika kata 12 kati ya 23 za wilaya ya Kilombero, alifanikisha ligi mbili katika kata mbili – ligi za mpira wa miguu na netboli, na alifanikisha Umitashumta ngazi ya wilaya na taifa.

Waliokumbwa na mafuriko Kilombero watakumbuka mchango wake na alipofika bungeni aliishutumu serikali kwa kukawia kutoa msaada.

Wengine watakaomkumbuka ni vikundi viwili vya kina mama wajane vilivyojengewa uwezo vikaweza kujiajiri na kuendesha maisha yao wenyewe, vikundi vitano vya kina mama kuweza kujiajiri, vikundi vitatu vya wenye ulemavu kujiajiri wenyewe.

Mwamko mkubwa wa kisiasa wilayani Kilombero una mchango wake. Amefanya mikutano 20 ya hadhara ya elimu ya uraia, amelipia na kufungua ofisi za CHADEMA katika kata tano, amefungua na kuzindua matawi 13 yaliyojengewa na yenye uongozi wa kudumu na akaingiza wanachama zaidi ya 8,000.

Kazi nyingine kubwa alizoshiriki ni kutoa mafunzo ya mapungufu ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba 2011 katika mkoa wa Ruvuma na akashiriki makongamano na mikutano ya hadhara na uzinduzi wa matawi.

Regia aliyezaliwa 21 Aprili 1980 alipata ulemavu akiwa na umri wa miaka saba. Alivunjika mguu wa kulia katika kifundo wakati anacheza mpira na wenzake.

Alipolelekwa katika hospitali ya Lugalagala, Njombe, madaktari walipiga picha na haraka wakafunga bandeji ngumu (POP) bila kunyoosha mguu. Kosa hilo , ambalo lilitokana na ujuzi mdogo ndilo lilisababisha sehemu hiyo ya mguu kuoza na hatimaye kukatwa.

Regia, ambaye ni doto (kulwa ni Remija) alisoma Shule ya Msingi Mchikichini kati ya mwaka 1989 na mwaka 1995; Sekondari ya Forodhani, Dar es Salaam kati ya mwaka 1996 na mwaka 1999; Machame Wasichana kwa masomo ya kidato cha V mwaka 2000, kidato cha sita mwaka 2002.

Mwaka 2003 alijiunga na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokonne (SUA) ambako alimaliza mwaka 2006 ambako alitunukiwa shahada ya Maarifa ya Nyumbani na Lishe. Mwaka 2007 akajiunga na CHADEMA.

Mungu ailaze roho yake mahali pema. Amina.

0
Your rating: None Average: 4 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: