Reli imetelekezwa, uchumi ukala mweleka


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 16 May 2012

Printer-friendly version

KWA miaka zaidi ya 10 Tanzania imezungukwa na taswira iliyokomaa ya kudhohofika kwa njia kuu za usafirishaji za reli, meli na ndege, kana kwamba hazina umuhimu wowote katika ujenzi na ukuaji wa uchumi wa taifa.

Vituo vyote vya treni vimeota magugu. Reli imegeuka kichaka. Sababu kubwa za kudhohofika huku ni serikali  kushinikizwa na wakubwa kujitoa katika kumiliki njia kuu za usafirashaji.

Mashirika yetu ya reli, bandari na ndege yamekufa. Huu ni msiba mkubwa kwa taifa. Athari zake zinatugusa sote na utaziona kila pembe ya nchi.

Tanzania inatumia magari mengi ambayo yanatughalimu pesa nyingi za mafuta, vipuri na matairi. Matokeo yake ni mfumuko wa bei kwa sababu ya gharama kubwa za usafirishaji.

Kwa mfano mwaka 2010 mfuko wa saruji ulikuwa unauzwa Sh. 9,000 jijini Dar es Salaam lakini Mwanza ulikuwa Sh. 18,000 kutokana na gharama za usafirishaji.

Gharama za kusafirisha tani moja ya saruji ilikuwa ni Sh. 150,000 kwa gari ilhali kwa treni ilikuwa Sh. 103,663. Hapo utaona zingebaki Sh. 46,337 mfukoni mwa wananchi kwa kila tani ya saruji kama tungetumia treni au Sh. 2,316.85 kwa kila mfuko wa kilo 50. Hali iko hivyo hivyo kwa bidhaa nyingine kama mchele, mahindi, sukari na chumvi.

Kama nchi nzima tungesafirisha kwa kiwango cha chini kabisa cha tani milioni tano tu kwa treni, utapata hesabu hii: Sh. 46,337 zidisha kwa tani 5,000,000 utapata Sh.  231.685 bilioni ambazo zingebaki mfukoni mwa wananchi.

Hali hii inagusa kila sehemu ya Tanzania. Huko Muleba bei ya saruji ilikuwa ni Sh. 23,000 mpaka 25,000.

Kumbe behewa la saruji lingekuwa linafika Mwanza na kuwekwa kwenye meli ya mizigo hadi Kemondo, bila shaka unafuu wa maisha ungekuwa mkubwa kwa mkazi wa Muleba ambaye kipato chake kwa mwaka ni kati Sh. 100,000 na Sh. 150,000 kwa mujibu takwimu za serikali.

Usafiri wa treni pia ni nafuu kwa abiria. Mfano nauli ya kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza daraja la tatu ilipokuwa Sh. 19,000, nauli ya basi ilikuwa Sh. 50,000. Hii ina maana Sh. 21,000 zingebaki mfukoni mwa huyu abiria iwapo treni ingekuwa usafiri wa kuaminika na haraka.

Kama watu milioni moja wangetumia treni kwa mwaka 2010 ina maana Sh. 21 bilioni zingebaki mfukoni mwao.

Kampuni ya reli kwa sasa ilikuwa na wafanyakazi 3,220 mwaka 2010 baada ya kupunguzwa kutoka 6,500. Kama shirika la reli litasimamiwa vizuri na serikali litatoa ajira rasmi na zisizo rasmi kwa malaki ya Watanzania. Miongoni mwa ajira rasmi ni pamoja na wahandisi wa ujenzi na ukarabati wa treni na reli, madereva wa treni, mafundi katika karakana, wahudumu katika treni za abiria, wakata tiketi katika vituo na watunza takwimu za usafiraji mizigo.

Ajira nyingine zisizo rasmi ni za wapakua mizigo kwenye mabehewa na hata wafanyabiashara kama kina mama lishe na baba lishe katika vituo vya treni.

Kwa mfano, kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza kuna vituo 68, na kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma kuna vituo 85. Fikiria reli ya kwenda Mpanda na ile ya Tanga, Moshi na Arusha, ile ya Mtwara na Lindi, na TAZARA kuanzia Mbeya hadi Dar es Salaam ni watu wangapi watanufaika.

Fikiria ajira za wasomi wetu waliosomea usimamizi wa biashara, takwimu, uhasibu n.k, ambao wangepata ajira katika kila kituo cha treni. Fikiria ajira katika viwanda vitakavyokuwa vinafua chuma kwa ajili ya kutengenezea mataluma, kupasua kokoto, karakana, sementi, rangi, ufyatuaji matofari, vioo, upasuaji mbao n.k kwa ajili kujenga reli mpya na vituo vipya.

Hapo utaona kwamba katika reli kuna ajira nyingi sana rasmi zenye mafao ya uzeeni kwa vijana wetu. Ajira hizi zitaongeza mapato kwa serikali kwani wafanyakazi watakuwa wanalipa kodi. Reli itatoa chachu ya kukua kwa viwanda vya kufua chuma, kutengeneza vipuri, nk. na kuifanya Tanzania iingie tena katika mapinduzi ya viwanda na vizito.

Hili litasaidia kukuza ubunifu, uzoefu, utafiti na teknolojia nchini katika nyanja zote za viwanda vinavyogusa reli. Juu ya hayo reli ni usafiri wa uhakika wenye uwezo wa kusafirisha abira wengi zaidi ya mabasi na kwa usalama zaidi.

Nini kifanyike? Mosi, serikali imiliki shirika la reli.

Pili, serikali iunde upya shirika la reli na liwe na muundo wa kujiendesha kwa faida kwa mujibu wa kanuni za biashara na menejimenti kwa ufanisi, uaminifu, kiushindani na kutoa huduma bora za kisasa.

Tatu, serikali ijenge njia ya pili kwa reli zetu zilizopo hivi sasa ili iwe rahisi kusafirisha bidhaa na abiria kwa usalama zaidi. Ujenzi huu utanguliwe na ujenzi wa viwanda vya kufua chuma ili kuzalisha chuma cha pua ambacho hutumika katika ujenzi wa reli, kutoa ajira kwa vijana na kupunguza gharama za kuagiza vipuri na vifaa vingine nje ya nchi.

Pesa ya kujenga njia ya pili ya reli kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma inatosha kabisa kujenga kiwanda cha kufua vyuma na kubakiza mtaji wa kukiendesha kiwanda hicho. Hakuna nchi duniani imeendelea bila kuwa na viwanda vya kufua chuma. Hata historia ya mwanadamu inaonyesha mababu zetu walipiga hatua haraka za kimaendeleo pale tu walipogundua namna ya kufua chuma (nitaliongelea zaidi katika maoni yangu kuhusu viwanda vyetu).

Mkaa wa mawe na chuma huko Mchuchuma vingetusaidia sana katika hili.

Nne, serikali kupitia shirika la reli inunue treni ziendazo kwa kasi.

Tano, shirika la reli liweke utaratibu mpya wa kusafirisha abiria. Mfano kwa treni iendayo kwa kasi kutoka Mwanza hadi Dar es Salaam isimame katika vituo vikubwa tu navyo visiwe zaidi ya kumi (mfano: Morogoro, Dodoma, Singida, Tabora, Shinyanga na vituo vingine vitano muhimu hapo katikati) na itumie saa zisizozidi 24 kusafiri kati ya Dar es Salaam na Mwanza.

Pia baina ya vituo vikubwa ziwepo treni za kuhudumia vituo vidogo vidogo. Kwa mfano treni iendayo kwa kasi ikitoka Mwanza isimame Shinyanga lakini hapo katikati iwepo treni ya kuhudumia vituo vidogo vidogo kati ya Mwanza na Shinyanga.

Sita, mfumo wa mawasiliano katika treni uboreshwe ili kuepusha ajali na hasa wakati njia moja tu inatumika kabla ya kujenga njia ya pili.

Saba, serikali ijenge reli katika maeneo mengine ya nchi.

Nane, shirika la reli liwe na ufanisi katika kupakia na kupakua mizigo. Idara hii ihakikishe mizigo haipotei na inafika katika muda uliopangwa.

Tisa, tuna nchi sita jirani zinategemea bandari zetu. Reli ingeweza kuzihudumia nchi hizi kwa faida kubwa. Hivyo basi bandari ya nchi kavu kama Isaka ziingekuwa vituo kikubwa vya ajira na biashara.

Je, tunashindwa kuyafanya haya? Naamini kwa nia safi na uzalendo tunaweza. Kinyume chake ipo siku tutakuta mwekezaji ameing’oa  reli na kuuza chuma chakavu.

+447404486150
0
No votes yet