Ridhiwani amponza Bashe


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 18 August 2010

Printer-friendly version
Hussein Bashe

ITACHUKUA muda mrefu kuelewa hasa kiini cha Hussein Bashe kunyang’anywa uraia.

Wakati hati zake muhimu zinathibitisha kuwa ni raia wa Tanzania, kikao cha Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC-CCM) kilishawishiwa kuamini kuwa uraia wake “una utata.”

Bashe amekuwa mjumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana (UV-CCM) hadi “alipovuliwa uraia”, ndani ya kikao cha chama, na hivyo kupoteza nyadhifa zake zote alizokuwa akishikilia.

Tuhuma zilizomwangusha Bashe ni kama zile zilizomtikisa Rais Jakaya Kikwete mwaka 2003 akiwa waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa.

Mwaka huo, Kikwete aliwasilisha hoja ndani ya Kamati Kuu (CC) iliyokutana Zanzibar, kwamba ameanza “kuandamwa kutokana na uamuzi wake wa kutaka kugombea urais mwaka 2005.”

Kikwete aliwaambia wajumbe wa CC kwamba alikuwa anahujumiwa na baadhi ya “maadui zake;” kauli ambayo inarandana na ile ya Bashe kwamba maadui zake ndio walioanzisha tuhuma kwamba “siyo raia wa Tanzania.”

Bahati mbaya ni Kikwete ambaye anatajwa kutamka hoja “iliyommaliza Bashe kisiasa.” Hilo limetokea wakati Bashe ameshinda katika mchakato wa kura za maoni kuwania ubunge jimbo la Nzega mkoani Tabora.

Taarifa zinasema, ni Rais Kikwete ambaye hata baada ya kuonyeshwa nyaraka zote muhimu ndani ya kikao, zinazomhusu Bashe, alisema “uraia wake una utata.”

Kauli ya rais ilikuja baada ya mjadala ambao pia ulichangiwa na mjumbe Andrew Chenge aliyenukuliwa akimueleza rais kuwa “…kisheria, suala la uraia wa Bashe halina utata.”

Mchango wa Chenge ulifuatiwa na ushauri wa mwenyekiti Kikwete kwamba wajumbe waende kupata futari.

Ilikuwa baada ya kurejea ukumbini, ndipo rais anaripotiwa kusema kuwa amepata nyaraka zinazotilia shaka maelezo ya Bashe.

Kwa mujibu wa taarifa za ndani ya vikao vya CCM vilivyofanyika mjini Dodoma mwishoni mwa wiki – sekretarieti, Kamati ya Maadili na Kamati Kuu (CC), suala la uraia wa Bashe lilikwishafungwa katika mkutano wa maadili.

Kitakachoendelea kuchangia utata wa hatma ya Bashe ni marejeo ya Rais Kikwete kuwa, “… kijana mwenyewe alitusumbua sana kule Iringa….”

Mkutano wa Iringa ndio uliomlazimisha aliyekuwa mwenyekiti wa taifa wa UV-CCM, Hamadi Masauni Yusuf, kujiuzulu wadhifa wake kwa madai kuwa na nyaraka za utata kuhusu umri wake.

Hata hivyo, taarifa sahihi ni kwamba Bashe hakuwa kwenye mkutano huo, lakini alisingiziwa kutaka kumshambulia Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba aliyekwenda huko kushinikiza Masauni kujiuzulu.

Taarifa zinasema Bashe na Masauni wamekuwa wakitajwa kuwa maswahiba waliokuwa wanapambana ndani ya UV-CCM na kundi la Ridhiwani na makamu mwenyekiti wa umoja huo, Benno Malisa.

Ridhiwani ni mtoto mkubwa wa Rais Kikwete ambaye hivi karibuni alipewa kazi kuzunguka mikoa kumi kutafuta wadhamini wa baba yake katika kinyang’anyiro cha urais mwaka huu.

Bashe na wafuasi wake wanadaiwa kutaka kazi ya kutafuta wadhamini ifanywe na viongozi wa UV-CCM kama taasisi, badala ya Ridhiwani.

Taarifa zinasema kuwa ingawa UV-CCM haikupewa kazi ya kutafuta wadhamini, Ridhiwani alitumia nyenzo na rasilimali za umoja huo kufanikisha kazi ya baba yake.

Gazeti hili limefanikiwa kuona nyaraka mbalimbali zilizowasilishwa na Bashe kwenye vikao hivyo vya juu vya CCM.

Nakala ya cheti cha kuzaliwa cha Bashe chenye Na. 00089141 inaonyesha alizaliwa 26 Agosti 1978 wilayani Nzega mkoani Tabora.

Taarifa hizo za kuzaliwa kwa Bashe ziko pia kwenye pasipoti yake Na. AB 345001 iliyotolewa 18 Agosti mwaka 2009.

MwanaHALISI limefanikiwa pia kuona barua yenye Na. DN 109758/22 iliyotoka kwa Mkurugenzi wa Uhamiaji, 13 Agosti 2010, ikithibitisha kwamba Bashe ni raia wa Tanzania.

0
No votes yet