Rushwa yaweza kuleta mauti


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 02 June 2009

Printer-friendly version

SIYO rahisi kupambana na rushwa kutoka Dar es Salaam peke yake. Kunapaswa kuwa na mipango na wapambanaji kuanzia makao makuu ya nchi, miji mikuu mikoani na wilayani, vijijini hadi ngazi ya familia.

Hayo ni maoni ya Anatory Ntoole Nshoga (55) wa Kitongoji Nyakataano, Kishanje, Bukoba Vijijini.

“Rushwa ndogondogo kwa ngazi ya vijiji, ni rushwa kubwa hasa kwa vile inafanyika miongoni mwa watu masikini wasio na uwezo na ambao wanaweza kudhurika zaidi,” anasema Nshoga.

Anatoa mfano wa rushwa katika utoaji dawa inavyoweza kusababisha kifo kwa mgonjwa au mjamzito, kwa vile muhusika hana uwezo wa kupata fedha za kuhonga.

Nshoga ni mmoja wa wakulima walioshiriki Kongamano la kitaifa la kuzindua Ripoti ya Mtazamo-Rushwa na Tawi la Tanzania la asasi ya Kimataifa ya Kuendeleza Uwazi, Utawala Bora na Kupambana na Rushwa (Transparency International – TI).

Kongamano hilo lililofanyika Dar es Salaam, 8 Mei mwaka huu, liliunda kamati ya watu tisa ya kuandaa taratibu za kusajili, ndani ya miezi sita, tawi la Tanzania la TI. Kamati inaongozwa na Profesa Mwesiga Baregu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Nshoga anasema, “Tukiweza kuondoa rushwa vijijini tutakuwa tumeweza kuweka msingi imara wa utawala bora.”

Anasema, “Maendeleo hayawezi kupatikana katikati ya rushwa. Sharti vijiji viwe na viongozi bora; wanaokataa rushwa kwa kauli na vitendo na walioapa kuwatumikia wananchi bila kuwaomba au kutegemea ‘asante.’”

Kuhusu kuwepo kwake kwenye kongamano la kuasisi asasi ya kupambana na rushwa, Nshoga anasema, “Naona asasi ya ForDIA iliyoandaa kongamano imekomaa hadi kutambua umuhimu wa mapambano kuingia ngazi ya kijiji.”

Huyu ni mkulima na mfugaji aliyepata elimu ya msingi Mwemage Boys Middle School kati ya 1962 na 1968; mwenye watoto tisa aliowapata na mshirika wake Bi. Lauriana Daudi.

Nshoga amewahi kuwa mtunza kumbukumbu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili na mtumishi wa ngazi ya uinjilisti katika kanisa la Kiinjili la Kikristo Tanzania dayosisi ya Kaskazini Magharibi (ELCT/NWD), mtaa wa Kishanje.

Nshoga amehudumia jamii yake ya kijijini kwa karibu zaidi.

Amekuwa mweka hazina mradi wa ujenzi wa Ekijanjabo (Wodi ya wazazi) ya zahanati ya Kishanje na mjumbe wa Serikali ya Kijiji kupitia Tanzania Labour Party (TLP).

Aidha, Nshoga amekuwa mraghabishi wa vyama vya Saccos na mweka hazina wa Usharika (Saccos) wa Kaagya; na mwakilishi wa wakulima wa Kishanje kwenye mkutano wa Chama cha Ushirika cha Mkoa, KCU (1990) Limited.

Kuhusu matarajio yake, Nshoga anasema yuko tayari kuwa mwakilishi wa tawi la Tanzania la TI kijijini na mkoani.

Kuhusu uongozi kijijini, Nshoga anasema, “Sifa za kuongoza ninazo. Wananchi Wakipenda niwe kiongozi wao, sitawakatisha tamaa.”

0
No votes yet