Rwanda yatajwa kifo cha Prof. Mwaikusa

MAUAJI ya Profesa Jwani Timothy Mwaikusa, sasa yanahusishwa na wauaji kutoka nchi jirani, MwanaHALISI limeambiwa.
Nchi ambayo imehusishwa moja kwa moja ni Rwanda ambayo inaingia katika uchaguzi mkuu mwezi ujao.
Nchi nyingine inayotuhumiwa ni Somalia ambayo dola lake limetota na haina utawala thabiti wa kiserikali tangu kuagushwa kwa Rais Mohammed Siad Barre mwaka 1991.
Taarifa zinasema wauaji watakuwa “wametumwa na serikali ya Paul Kagame kunyamazisha wanaotetea watuhumiwa wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 katika mahakama ya kimataifa mjini Arusha.”
Siku kumi zilizopita, kikundi cha kigaidi cha Al Shaabab kutoka Somalia kilitangaza kuwa ndicho kiliangamiza roho za watu wapatao 80 mjini Kampala kwa njia ya mabomu na kudai kuwa kitaendelea kufanya hivyo katika nchi zote za Afrika zilizopeleka majeshi nchini mwao.
Lakini Balozi wa Rwanda nchini, Fatma Ndagiza amekana serikali yake kuhusika na mauaji ya Profesa Mwakusa yaliyofanywa siku mbili baada ya mwalimu huyo mahiri wa sheria kurejea Dar es Salaam akitokea Arusha.
Balozi aliulizwa iwapo amesikia taarifa zinazohusisha serikali ya Rais Kagame na mauaji hayo na kutaka kauli yake.
Balozi Ndagiza amesema mjini Dar es Salaam, “…hayo ni mambo ya uvumi tu; nayaona hayana msingi wowote na sijui walioyasema wameyapata wapi.”
Akiongea kwa Kiswahili na kwa utulivu kwa njia simu, Ndagiza alimwambia mwandishi wa habari hizi kuwa serikali yake inaheshimu haki za binadamu na haiwezi kufanya kitu kama hicho.
Alipoelezwa kuwa madai hayo yanahusishwa na Profesa Mwaikusa kutetea watuhumiwa wa mauaji ya kimbari nchini mwake, balozi alisema, “Sisi tunaheshimu watu wote wanaoshiriki katika kesi zinazohusu mauaji ya halaiki nchini Rwanda. Hatuna sababu ya kuwasumbua.”
Kuhusu taarifa hizo kuharibu hadhi ya nchi yake, Balozi Ndagiza alisema ni kweli, lakini akaongeza, “Ni vizuri watu wasubiri uchunguzi ukamilike maana haya mambo ya uvumi yaweza kuvuruga uhusiano wa nchi zetu ndugu.”
Msemaji wa serikali ya mpito mjini Mogadishu, hakuweza kupatikana kutoa maelezo yake juu ya kuhusika kwa wananchi wake katika mauaji ya Mwaikusa.
Profesa Mwaikusa aliuawa nje ya nyumba yake, Tegeta Salasala, nje ya jiji la Dar es Salaam, usiku wa Jumanne wiki iliyopita kwa kupigwa risasi. Watu wengine wawili waliuawa katika tukio hilo akiwemo jirani.
Wauaji bado hawajapatikana ingawa polisi wameeleza kuwa wanashikilia watu sita kuhusiana na mauaji hayo.
Taarifa kutoka kwa familia yake zinadai kuwa Baraka Mwaikusa, mtoto mkubwa wa profesa aliambiwa na wauaji kuwa wasingefikia hatua ya kuua baba yake kama angeacha “ukaidi wake.”
Baraka ananukuliwa akisema wauaji hao hawakuchukua chochote ndani ya chumba cha baba yake ambako aliwapeleka baada ya kumlazimisha afanye hivyo.
Uhusishwaji serikali ya Rwanda unatokana na Profesa Mwaikusa kutokea kuwa mahiri kutetea watuhumiwa wa maiaji ya kimbari katika Mahakama ya Kimataifa ya Wahalifu wa Rwanda (ICTR) iliyopo jijini Arusha.
Naye Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi (ACP) Charles Kenyela, ameiambia MwanaHALISI kuwa madai yanayohusisha serikali za nchi jirani “ni taarifa tu za kusikia.”
Alipoulizwa iwapo amesikia taarifa zinazohusisha serikali za nchi, Kamanda Kenyera alikiri kuzisikia lakini alisema, “Tunaendelea na uchunguzi; wala hatujapata uthibitisho wa taarifa hizo.”
Kenyera amesema mchakato wa upelelezi unaendelea na kwamba polisi wanahitaji kuchukua maelezo ya watu mbalimbali, kusikiliza wanafamilia na kufanya zoezi la utambuzi wa wale ambao watakuwa wamekamatwa.
“Katika hatua hii, ni vigumu kuhusisha nchi nyingine. Wananchi waamini kuwa tunafanya kazi…na sharti vyombo vya habari vichukue tahadhari katika kuripoti taarifa za matukio kama haya yanayoweza kuathiri uhusiano wa nchi husika,” ameeleza Kenyera.
Madai ya wauaji yaliyonukuliwa na mtoto wa marehemu, kwamba Profesa Mwaikusa alikuwa kaidi, yanaleta sura kuwa alikuwa hakubaliani na wenzake katika hoja fulani ndani na nje ya familia yake.
Hata hivyo, taarifa kutoka ndani ya familia ya marehemu zinakataa mtizamo huo. Hakuna hata mtu mmoja katika familia hiyo mwenye uthibitisho kuwa Profesa Mwaikusa alipata kusimulia kukabiliwa na mvutano na yeyote katika familia.
Bali kuna taarifa za ukizani kati ya serikali ya Rwanda na kinachotokea Arusha. Vyanzo vya habari ndani ya ICTR vinasema mauaji ya Profesa Mwaikusa yamekuja wakati mahakama hiyo imemruhusu afanye utafiti juu ya wazo lake la kuruhusu ushahidi dhidi ya watuhumiwa kutolewa kwenye eneo la tukio nchini Rwanda.
Aidha, Profesa Mwaikusa alikuwa amepata ushindi katika utetezi wa mfanyabiashara Yusuf Munyakazi (75), raia wa Rwanda, ambaye amehukumiwa kifungo cha miaka 25 jela kwa kosa la kushiriki mauaji ya halaiki.
Katika hili, Profesa Mwaikusa alifanikiwa kushauri mahakama kukubali kuwa mteja wake hatakuwa salama nchini Rwanda na badala yake afungiwe nchi nyingine. Sasa atafungiwa Ubelgiji.
Hatua ya ICTR kukubaliana na wakili kuwa usalama wa wateja wake nchini mwao ni mdogo, inaweka msingi wa kutowarudisha Rwanda wengine watakaotiwa hatiani.
Hatua hii pia inaiweka Rwanda pabaya kwani mahakama ya kimataifa, iliyoundwa na Umojawa Mataifa (UN), ndiyo imekubali kwamba Rwanda hakuna usalama.
Watuhumiwa wa mauaji ya halaiki wanaoshikiliwa nchini Rwanda, wanafikishwa katika mahakama zinazoitwa “Gacaca” ambazo zinaendeshwa na watu wasio na ujuzi wa sheria bali matakwa ya utawala.
Wataalamu wa sheria nchini wanazungumzia mauaji hayo kama tukio lililoshtua wengi na wapo wanaodai kuwa lina “mkono nje ya nchi.”
Profesa wa sheria Issa Shivji, amesema anaona suala hili linahusiana moja kwa moja na kesi za Rwanda na nafasi ya marehemu katika utetezi.
Shivji ambaye ni mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, amesema Profesa Mwaikusa, katika kufanya kazi yake, ametoa mchango mkubwa katika utawala wa sheria na ulinzi wa haki.
Dk. Zaveli Lwaitama wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam amesema anasikitika kukuta polisi wa Tanzania wamekimbilia kutoa jawabu kwamba ni “tukio la kijambazi” hata kabla ya kuanza kulichunguza.
Alitaka kufanywe uchunguzi wa kitaalamu ndipo serikali itoe tamko la nani hasa wamehusika kumwangamiza mtaalamu aliyetoa mchango mkubwa katika muda wake wa kuitumikia nchi.
Wakili wa mahakama kuu, Tundu Lissu, alikwenda mbali akihoji iwapo profesa bingwa wa sheria na mtu mwenye hadhi ya kimataifa kama Mwaikusa anauawa kikatili namna hiyo, “Mtanzania gani yuko salama.”
Naye wakili wa mahakama kuu, Dk. Sengondo Mvungi amesema yanayotendeka ICTR yanaiudhi serikali ya Rwanda; kwamba serikali ingetaka kila anayefikishwa pale atiwe hatiani; apate adhabu kali, hata kunyongwa.
Dk. Mvungi amesema serikali ya Rwanda imekuwa ikishangaa mawakili wa aina ya Profesa Mwaikusa wanaotetea haki na kusimamia sheria; hivyo hashangai iwapo kutakuwa na vikosi vya mauaji vinavyoelekezwa kwa watu kama hao.
Akirejea nchi za Jumuia ya Afrika Mashariki, Dk. Mvungi amesema umoja ni kitu kizuri lakini “tunaweza kuja kujuta iwapo tutaingiza inzi, nge, nyoka. Katika hali hii siyo lazima tupate neema kama tunavayofikiria. Inaweza kuwa balaa.”
Katika siku za karibuni kumekuwa na matukio ya kigaidi nchini Rwanda. Mwandishi wa habari Jean Leonard Rugambage wa gazeti la Umuvugizi la nchi hiyo alikutwa ameuawa.
Mwandishi aliuawa siku chache baada ya kuchapisha taarifa zilizodai kuwa Rais Kagame ndiye aliamuru Jenerali Kayumba Nyamwasa auawe nchini Afrika Kusini.
Jenerali Nyamwasa alipigwa risasi mbili mjini Johannesburg na kwa mshangao wa washambuliaji hakufa. Nyamwasa alikimbilia Afrika Kusini mapema mwaka huu baada ya kuacha kazi ya ubalozi wa nchi yake nchini India akidai serikali ilikuwa inapanga njama za kumuua.
Wiki iliyopita, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Chama cha upinzani cha DGPR, Andre Kagwa Rwisereka, alikutwa ameuawa kwa kukatwa kichwa, siku moja baada ya chama chake kutangaza kuwa haonekani.
Naye wakili Peter Erlinder wa Marekani aliachiliwa mwezi uliopita baada ya kuwekwa rumande kwa siku 21 nchini Rwanda kwa tuhuma za kuingilia mchakato wa mashitaka dhidi ya mpinzani wa Kagame.
Erlinder anamtetea Victoire Ingabire Umuhoza ambaye alirejea nchini Rwanda mwishoni mwa mwaka jana akiapa kumwangusha Rais Kagame katika uchaguzi wa baadaye mwezi ujao. Erlinder alikamatwa wakati akiandaa utetezi wa Ingabire.
Kukamatwa kwa Erlinder ambaye alikanusha kuhusika na mashitaka hayo, kuliamsha hasira za wanasheria kwani kundi la mawakili 30 wanaoshiriki kutetea watuhumiwa ICTR walitishia kugoma iwapo ataendelea kushikiliwa.