Samatta kutajirisha Kimbangulile


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 11 May 2011

Printer-friendly version

SAKATA la uhamisho wa mshambuliaji wa klabu ya Simba ya Dar es Salaam, Mbwana Samatta limechukua sura mpya baada ya maelezo ya wakala wa mchezaji huyo kupishana na ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Damas Ndumbaro, mwanasheria na wakala aliyefanya mipango Samatta kupata mkataba wa kuichezea klabu ya TP Mazembe ya DR Congo, anasema anatambua kisheria kuwa klabu zote ambazo mshambuliaji huyo alipitia kabla ya kuuzwa kama profeshno, zinapaswa kulipwa fidia ya mafunzo.

Lakini, wazee wenye mamlaka ya soka nchini—TFF—wanasema klabu itakayonufaika ni ile itakayoonyesha vielelezo namna walivyoandikishiana katika mkataba na klabu alikouzwa mchezaji.

“Hizi klabu zinajenga hoja ya kummiliki na nyingine zinadai fidia, lakini haya si makosa ya TFF kung’angania kwamba huyu ni mchezaji wa Simba. Makosa ni ya klabu zenyewe kwa vile hakuna nyaraka zinazoonyesha kwamba wana haki ya kummiliki au fidia kwa kuwa alipita huko kwao kama wanavyodai,” alisema ofisa habari wa TFF, Boniface Wambura.

“Makosa waliyofanya Kimbangulile au African Lyon ni sawa na waliyofanya Yanga kwa mshambuliaji wao Shaaban Nonda, ambaye alipokwenda klabu ya Vaal Professional ya Afrika Kusini waliofaidika ni wajanja wachache tu,” alisema.

Lakini Ndumbaro amesema anatambua kanuni ya FIFA inayozungumzia Hadhi na Uhamisho wa Wachezaji hasa ibara ya fidia ya mafunzo na elimu.

“Klabu hizi zote zina haki. Fedha itakayopatikana kwa mauzo ya mchezaji kwa mara ya kwanza kutoka klabu profeshno iliyomnunua itatengwa asilimia 20 ya fedha hizo kwa ajili ya fidia,” anasema.

Ndumbaro alisema asilimia tano itapewa timu ambayo imemlea na kumtunza mchezaji alipokuwa na umri wa kati ya miaka 12 hadi miaka 15 na asilimia nyingine 15 itagawanywa kwa klabu nyingine zilizomlea mchezaji hadi alipofikisha umri wa miaka 23.

Samatta ana umri wa miaka 19 na amechezea klabu za Kimbangulile (2003 – 2007), Mbagala Market (2007 – 2008), Temeke United (2008 – 2009), African Lyon (2009 – 2010) na Simba (2010 – 2011). TP Mazembe inataka kumnunua mchezaji huyo kwa kitita cha Sh. 150m.

Kwa kuzingatia maelezo ya Ndumbaro, Kimbangulile inastahili kiasi cha Sh. 7.5m ilihali klabu hizo nyingine zitagawana kiasi cha Sh. 22.5m. Asilimia 20 ya Sh. 150m ni Sh. 30m.

Pamoja na majibu mazuri ya TFF, shirikisho hilo itabidi lirejee kwenye kanuni; Ibara ya 20 kuhusu malipo ya fidia kwa mafunzo na Ibara ya 21 kuhusu utaratibu wa kukokotoa malipo ya fidia.

Kiambatanisho Na 4 kuhusu malipo ya fidia Ibara ya 1 kuhusu Malengo inasema (1) kipindi cha mafunzo na elimu kwa mchezaji ni kati ya miaka 12 na 23. Malipo ya fidia yatatolewa kwa mujibu wa sheria hadi umri wa miaka 23 lakini kwa gharama za mafunzo hadi akiwa na umri wa miaka 21, labda tu ifahamike kwamba mchezaji husika alikatisha mkataba wake na akaacha mafunzo kabla ya kufikisha umri wa miaka 21.

Katika hali ya kawaida malipo ya fidia kwa mafunzo na elimu yatatolewa hadi msimu wa mwisho anapotimiza miaka 23, lakini kiasi cha malipo kitakokotolewa kwa kuzingatia umri wake.

Kifungu cha (2) kinasema jukumu la kulipa fidia kwa mafunzo hakina mgongano wowote na jukumu la kulipa fidia kwa kuvunja mkataba.

Ibara ya 2 kuhusu malipo ya fidia ya mafunzo inasema (1) malipo ya fidia kwa mafunzo yatatolewa mara tu (i) mchezaji anaposajiliwa kwa mara ya kwanza kama profeshno; na (ii) mchezaji anapohamishiwa katika klabu ya nchi nyingine.

Kifungu cha 4 katika kiambatanisho Na 4 kuhusu gharama za mafunzo (Training Costs) kinasema (1) jinsi ya kukokotoa malipo yanayotakiwa kama gharama za mafunzo na elimu kwa mchezaji, vyama vya soka vya nchi vinatakiwa kugawa klabu katika madaraja manne kwa kuzingatia uwezo wa kifedha wa klabu kuwekeza kwenye mafunzo ya wachezaji.

Gharama za mafunzo zimepangwa kwa kila kundi na zinalingana na kiasi kinachotakiwa kufundisha mchezaji kwa mwaka mmoja na kikazidishwa kwa wastani wa siku ambazo wachezaji wametumika hadi kumpata mchezaji mmoja profeshno.

Ibara ya 5 ya kiambatanisho hicho inasema (1) kwa kawaida, kukokotoa gharama za fidia kwa mafunzo ya mchezaji katika klabu yake ya awali, ni lazima uchukue gharama zitakazotumiwa na klabu yake mpya endapo ingemjenga yenyewe.

(2) Ilivyo, mara mchezaji anaposajiliwa kama profeshno malipo ya fidia hukokotolewa kwa kuangalia gharama za mafunzo katika klabu yake mpya na zikazidishwa kwa miaka aliyopata mafunzo, kimsingi kuanzia miaka 12 hadi anapotimiza umri wa miaka 21.

(3). Ili kuhakikisha gharama za mafunzo kwa chipukizi hazipaishwi bila sababu za msingi, gharama za mafunzo kwa umri kati ya miaka 12 na 15 (misimu minne) ziko katika klabu zilizopangwa daraja la 4.

FIFA imetunga Ibara ya 6 maalum kwa ajili ya nchi za Umoja wa Ulaya (EU) na Ukanda wa Kiuchumi Ulaya (EEA). Ibara hiyo inahitaji uwepo wa mikataba inayotambulika na siyo kwa nchi za Afrika.

Kifungu cha (3) kinasema endapo klabu ya zamani ya mchezaji haina mkataba naye, haistahili malipo ya fidia labda yatolewe maelezo ya kina kuthibitisha kwamba inastahili fidia. Klabu ya zamani lazima impe mchezaji mkataba angalau siku 60 kabla ya mkataba wake wa sasa kumalizika na utakuwa na thamani sawa na mkataba wake wa sasa.

Kanuni inaonyesha kwamba malipo ya fidia ni asilimia tano kwa mchezaji mwenye umri kati ya miaka 12 na 15 na ni asilimia 10 kwa mchezaji mwenye umri kati ya miaka 16 na 21.

Nimetoa maelezo haya marefu ili kuonyesha kwamba klabu zote ambako Samatta alipita zinastahili malipo ya fidia kwa viwango ambavyo TFF inapaswa kuvijua.

brothermaps@yahoo.com
0
No votes yet