Selelii: Avua nguo Rostam, Lowassa


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 11 November 2009

Printer-friendly version
Adai Kikwete alikabidhiwa mapema ripoti ya Richmond
Asema kama kumuokoa ni yeye aliyepaswa kufanya hivyo
Mbunge wa Nzega Lucas Selelii

JUHUDI za mbunge wa Monduli, Edward Lowassa na mwenzake wa Igunga, Rostam Aziz kutaka kujivua na gome la Richmond zimezimwa, MwanaHALISI limeelezwa.

Taarifa kutoka ndani ya kikao cha kamati ya wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilichofanyika Dodoma wiki iliyopita, zinamtaja mbunge wa Nzega Lucas Selelii kuwa ndiye aliyezima ndoto za Lowassa na Rostam kujisafisha.

Inaelezwa kwamba Selii alizima ndoto za Rostam na Lowassa baada ya kuanika ushiriki mzima wa wanasiasa hao wawili katika mkataba huo.

Mkutano kati ya kamati ya wazee na wabunge ulifanyika siku tatu mfululizo katika ukumbi wa zamani wa Bunge mjini Dodoma.

Akiongea kwa kujiamini na kuchambua hoja moja baada ya nyingine, Selelii alisema Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza mkataba wa Richmond ambapo yeye alikuwa mmoja wa wajumbe wake inaoushahidi kwamba Richmond ni mali ya Rostam.

Kwa upande wa Lowassa, Selelii alisema  alibeba kampuni hiyo kwa maslahi ya binafsi ya rafiki yake huyo.

Akiongea baada ya Rostam kukana kumiliki kampuni hiyo na kutaka kuundwa kwa Tume huru kuchunguza mkataba huo, Selelii alisema “Rostam amewadanganya kwa kusema hahusiki na Richmond.”

“Huyu Rostam ndiye aliyetafuta nyumba kwa ajili ya matumizi ya ofisi ya Richmond. Ni yeye aliyelipia pango la nyumba hiyo,” alisema Selelii huku akitolea macho Rostam.

Alisema, “Kamati yetu ilihakikishiwa na mtoto wa Mucadam (Hussen Mucadam) ambaye ndiye mwenye nyumba kwamba nyumba iliyotumiwa na Richmond ilipangwa na Rostam.”

Huku wabunge na wajumbe wa kamati ya wazee wakiwa wamepigwa na butwaa, Selelii alisema “hata jopo la waadishi wa habari lililofanya kazi ya kusafisha Richmond lilitafutwa na Rostam.”

Alisema Rostam alifikia hatua ya kutumia waandishi hao wa habari mara baada ya vyombo vya habari kuanza kueleza utata wa mkataba.

“Ni huyu Rostam aliyekodisha jopo la waandishi wa habari watatu mashuhuri nchini kwa ajili ya kupoza makali. Tumezungumza na waandishi wa habari hawa mmoja baada mwingine na wote wametuthibitishia hili,” alisema Selelii.

Alitaja hata majina ya waandishi hao kuwa ni Gideon Shoo, Jimmy Mdoe na Salva Rweyemamu ambaye sasa ni mkurugenzi wa mawasiliano ya rais.

Tarehe 29 Juni 2006, serikali kupitia Shirika la Umeme la Taifa (Tanesco) ilisaini mkataba wa kufua umeme wa megawati 100 na kampuni ya Richmond Development Company (LLC) bila kwanza kuhakiki uhalali wa kampuni hiyo.

“Kama hahusiki kwa nini aliwatafuta hawa waandishi wa habari? Kwa nini aliwapa kazi,” alihoji Selelii.

Alisema mbali na waandishi wa habari na utafutaji wa nyumba, Kamati Teule iliweza kuthibitisha kwamba baada ya Richmond kuhuisha mkataba wake kwa Dowans, wafanyakazi watatu wa Caspian walionekana katika Dowans.

“Kwa maana nyingine, Dowans, Richmond na Caspian ni baba mmoja mama mmoja.”

Alisema Kamati Teule imepata ushahidi kwamba “fedha za Dowans zilihamishiwa katika akaunti ya Caspian; Rostam alikuwa akifuatilia mwenyewe fedha hizo hazina,” alisisitiza Selelii.

Mbunge mmoja wa Bunge la Muungano aliliambia MwanaHALISI kwamba wakati Selelii akieleza wajumbe taarifa hiyo, ukumbi mzima ulikuwa kimya.

“Hata sindano kama ingeanguka, ingeweza kusikika. Nakuambia yule jamaa jinsi alivyokuwa akiongea kwa upole na taratibu, kila mtu alikuwa na shauku ya kumsikiliza,” alisema.

Anasema, “Rostam alikuwa amekaa kimya. Alikuwa kama vile amelowa mvua.”

Baada ya kueleza ushiriki wa Rostam Selelii aliyeongea kwa kupanga hoja zake alirukia Makongoro Mahanga, mbunge wa Ukonga, ambaye awali alidai kuwa “ripoti ya Bunge ilikuwa feki.”

Makongoro amesema “ripoti yetu ni feki; Kamati Teule haikumshirikisha Rais Jakaya Kikwete. Haikumueleza; kama angeelezwa angemuokoa Lowassa,” alisema Selelii kwa taratibu.

Alisema madai hayo ya Mahanga hayana ukweli, na kwamba yamelenga kuhamishia tatizo kwa wengine.

Alihoji: Kama ripoti ilikuwa feki inawezekanaje rais aliyepewa taarifa hiyo kabla ya kuwasilishwa bungeni akaiamini?

Kuhusu Kamati Teule kutomshirikisha rais Kikwete, Selelii alisema kabla ya kamati kuwasilisha ripoti yake bungeni ilikabidhi ripoti kwa rais. Selelii alikuwa akijibu hoja ya Andrew Chenge na Mahanga waliotumia muda mrefu kueleza kikao juu ya kutoshirikishwa rais Kikwete.

Alisema, “Rais alikuwapo hapa Dodoma wakati mjadala wa Richmond unafukuta. Tayari alikuwa na ripoti yetu. Sasa kwa nini yeye hakumpa waziri mkuu wake,” alihoji Selelii na kuongeza, “haikuwa kazi ya kamati kumpa ripoti Lowassa.”

Alisema, Rais ana vyombo vya ulinzi na usalama. Je, kama yeye mwenye vyombo hivi hakuona kasoro, nani mwingine mwenye mamlaka ya kudai kuwa ripoti yetu ilikuwa feki,” alihoji.

Akiongea huku akionekana mwenye hasira, lakini kwa taratibu mno, Selelii alisema, “mnaleta umbeya hapa eti rais hakujua haya. Rais tulimpa ripoti hii kabla ya kuwasilisha bungeni.”

Taarifa zinasema Selelii alikiambia kikao hicho kwamba Kamati Teule imefanya kazi yake kwa kufuata misingi ya sheria.

“Duniani kote mtuhumiwa hawezi kupewa taarifa ya kilichomo katika ushahidi hadi pale suala hilo linapoingia mahakamani. Katika hili Lowassa hana wa kumlaumu,” Selelii alisisitiza.

Baada ya kumaliza kuumbua Mahanga, Selelii aligeukia Sophia Simba ambaye alituhumu Kamati Teule kuwa imemuonea Lowassa na kumvua nguo mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela na mumewe Joh Malecela.

Katika hilo, Selelii alisema, “Sophia Simba huyu ni mwenyekiti Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT). Pia ni waziri anayesimamia utawara bora,” chanzo cha habari ndani ya kamati kinanukuu Selelii.

Anasema, “aliyoyasema hapa hayakustahili kutolewa katika kikao hiki. Haya ni maneno yanayopaswa kutolewa kwenye kitchen party.  Nimemsikiliza kwa makini, mheshimiwa Simba amezungumza mambo binafsi yanayohusu mtu binafsi,” alisema.

Mbili, Selii alisema, “Sophia Simba amesema hapa kuwa Lowassa ni mwanamme namba moja. Ni mwanamme wa shoka. Akimaanisha kwamba wanaume wote akiwamo rais, waziri mkuu, wabunge na madiwani siyo kitu. Mimi sikubaliani naye. Labda kama mwanamme wa shoka katika masuala mengine,” alisema kwa kujiamini.

MwanaHALISI limefahamishwa kuwa mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge, Dk. Harrison Mwakyembe alikabidhi ripoti ya kamati yake kwa Spika wa Bunge, Samwel Sitta 31 Desemba 2007.

Mara baada ya Sitta kupokea ripoti ya Mwakyembe aliondoka nchini kwenda Uingereza kuhudhuria mkutano wa Bunge la Jumuiya ya Madola.

Taarifa zinasema mara baada ya Sitta kurejea nchini alikabidhi ripoti hiyo kwa rais Kikwete. Hiyo ilikuwa 29 Januari 2008; kabla ya Kikwete kuelekea Addis Ababa, Ethiopia kuhudhuria mkutano wa viongozi wakuu wa Afrika (AU).

Rais Kikwete alisafiri kuelekea Ethiopia 29 Januari 2007. Alirejea nchini 5 Februari 2008. Lowassa alikabidhiwa ripoti na Sitta 6 Februari 2009.

“Kwa mujibu wa kanuni za Bunge, iwapo nitakupa ripoti hii, sharti nifanye hivyo pia kwa kiongozi wa upinzani,” Sitta alinukuliwa akimueleza Lowassa.

Baada ya Sitta kumkabidhi Lowassa ripoti hiyo, alimkabidhi ripoti hiyo “Kiongozi wa Kambi ya upinzani Bungeni, Hamad Rashid Mohammed,” taarifa zinaeleza. 

Kwa upande wake, Sitta amekana kuwa Rostam aliwahi kuwasuluhisha yeye na Lowassa. “Ni uwongo mtupu. Mimi sijawahi kusuluhishwa na Lowassa. Kwanza, hatukuwa na ugomvi, sasa kwa nini tusulihishwe,” alihoji Sitta.

Alisema madai ya Rostam kwamba Sitta alitaka nyumba yenye hadhi Dar es Salaam na Urambo hayana msingi, kwa kuwa suala la makazi ya spika hupangwa na katibu mkuu kiongozi.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: