Serikali bado iko ‘chekechea’

SERIKALI ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), inaendelea kujifunza. Itaendelea kujifunza na labda bila kufuzu.
Aliyethibitisha kuwa serikali iko katika masomo yasiyoisha ni Waziri wa Miundombinu, Dk. Shukuru Kawambwa.
Akiwasilisha taarifa ya serikali bungeni wiki iliyopita, Kawambwa alisema yaliyotokea katika mkataba wa ukodoshaji kitengo cha makontena bandarini, kati ya serikali na kampuni ya TICTS na kile kilichomo katika mkataba tata wa kampuni ya Reli (TRL) ni “somo tosha kwa serikali.”
Ama CCM na serikali ni watoro – hawaingii darasani; au vichwa vyao vigumu, hivyo hawawezi kufuzu.
Kwani makosa yaleyale yanayoligharimu taifa raslimali nyingi, yanaendelea kujirudia mwaka hadi mwaka.
Kwa mfano, kauli ya Kawambwa imekuja miaka minane baada ya serikali kuingia mkenge kwa kuipa kazi ya kuongoza shirika la umeme la taifa (TANESCO) kampuni ya Net Group Solution.
Hakuna aliyesikiliza kilio cha wananchi, vyombo vya habari, wafanyakazi wa Tanesco, wasomi, hata wanasiasa waliotaka serikali kuzuia menejementi ya Net Group kukabidhiwa shirika. Serikali ilitumia mtutu wa bunduki kuingiza kampuni ofisini.
Haikuchukua muda, taarifa zikavuja kwamba wakurugenzi wanne waliokuwa wanaunda Net Group walijilipa kila mmoja mshahara wa Sh. 22 milioni hadi Sh. 25 milioni kila mwezi.
Fedha hizi zililipwa kwa kazi ambazo awali zilifanywa na wazalendo, tena kwa ufanisi mkubwa. Hakuna aliyechukua hatua. Bila shaka, serikali ilikuwa bado masomoni.
Matokeo yake, muda wote wa mkataba, Net Group ilishindwa kujenga hata njia moja mpya ya umeme. Wala haikujenga miundombinu mipya na ilishindwa kabisa kusimamia njia za umeme ilizozikuta.
Hatimaye, mkataba wa walioingizwa kwa ubabe na utawala wa Rais Benjamin Mkapa, ukadoda. Wakaondoka kwa aibu. Mara hii wakiitwa Net Group Problem, kwani hawakuwa na suluhisho.
Aidha, kauli ya Kawambwa imekuja miaka 14 tangu serikali kubinafsisha, tena kwa bei ya kutupa, Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), kampuni ya simu ya taifa (TTCL), shirika la ndege la taifa (ATC), mahoteli, viwanda, migodi, mbuga za wanyama na mashamba.
Sasa karibu mapugunfu yote yaliyomo katika mkataba kati ya serikali na TICTS ni yaleyale yaliyomo katika mikataba iliyotajwa hapo juu.
Angalia kwa mfano, mkataba kati ya serikali na TICTS. Awali mkataba huu ulikuwa wa miaka 10 – ulioanza 5 Mei 2000 na ungekoma 4 Mei 2010.
Lakini katika mazingira ambayo hayaeleweki chanzo chake, mwaka 2005 – miaka mitano kabla ya mkataba wa awali kumalizika, serikali iliongezea kampuni hiyo mkataba mwingine wa miaka 15 ambao utakoma mwaka 2025.
Ndani ya mkataba mpya na hata ule wa awali, serikali inakiri kwamba kuna vipengele ambavyo havina maslahi kwa taifa na hivyo vilitakiwa kufutwa au kurekebishwa.
Miongoni mwa vipengele hivyo, ni kukosekana kwa kifungu kinachombana mwekezaji kunyofoa vipuri kutoka kwenye mitambo ya Mamlaka ya Bandari (TPA) ambayo imekuwa ikikodishwa kwa TICTS.
Kifungu hiki kilichoachwa katika mkataba wa TICTS hakikuwamo wakati wa uuzaji wa hisa za ATC.
Katika mkataba huo, aliyeitwa mbia – shirika la ndege la Afrika Kusini – aliruhusiwa kung’oa vipuri katika karakana ya ATC na kuvisafirisha nje ya nchi.
Hatimaye karakana ya ATC ambayo ilikuwa nguzo ya taifa kwa ajili ya kujenga mafundi na marubani wenye ujuzi ilifungwa.
Ndege za ATC zilizokuwa zikifanya safari zake kupitia Dar es Salaam zililazimika kutengenezwa Afrika Kusini hata kama ndege hizo zimeharibikia nchini. Mwisho wa siku, ATC imeachwa yatima na serikali inaendelea kusema “imepata somo.”
Si hivyo tu, hata kipengele cha kulipa fidia mamlaka ya bandari pale muda wa vifaa vyake vilivyokodishwa unapomaliza hakikuwamo.
Swali: Aliyeruhusu kusainiwa mkataba mpya miaka mitano TICTS kabla ya mkataba wa awali kumalizika, amechukuliwa hatua gani?
Kama mkataba una vipengele visivyokuwa kwa maslahi kwa taifa, vilikuwa na maslahi kwa nani? Je, wahusika wamechukuliwa hatua gani? Je, serikali bado iko chekechea na hivyo haijui hatua za kuchukua?
Hata madai ya serikali kwamba iwapo ingevunja mkataba, taifa lingelazimika kulipa fidia ya Sh. 645 bilioni,” linajikita katika kilekile kinachoitwa, “serikali bado inajifunza.”
Kama miaka 50 baada ya uhuru, serikali haijui umuhimu wa kuwapo kwa kifungu kinachoruhusu kuvunjwa kwa mkataba pale mkodishaji anaposhindwa kutimiza majukumu yake, inatafuta nini madarakani?
TICTS imeshindwa kutekeleza kilichokubaliwa katika mkataba. Ndani ya bandari huduma haziendi kama ilivyotarajiwa, huku watumiaji wakubwa wa bandari wakizidi kutafuta maeneo mengine ya kupitishia mizigo yao.
Je, kama hali ni hiyo na serikali inakiri kwamba ufanisi wa kutoa mizigo umeshuka, nini kinachozuia kuvunjwa kwa mkataba? Bila shaka kama serikali ilivyosema, “bado inasoma” na haijafuzu.
Katika mazingira yaleyale ya kutohitimu, serikali imeingiza shirika la reli la taifa (TRC) kwenye mkataba wenye utata. Mkataba wa TRC uliosainiwa miaka mitano baada ya TICST kukabidhiwa bandari, umejaa mapungufu lukuki.
Kwanza, serikali inakiri kuwa mpango wa biashara wa kampuni (Busines Plan) si sehemu ya mkataba wa sasa. Pili, utaratibu wa mkodishaji kumkodisha mtu mwingine mali aliyokodishwa haukuwekwa bayana katika mkataba.
Katika hili, kuna mambo matatu muhimu ya kujadili. Kwanza, kama mpango wa biashara wa kampuni si sehemu ya mkataba, kwa nini anayejiita mwekezaji anaitumia?
Pili, kama haya si sehemu ya mkataba, nani aliyeruhusu RITES kukodisha TRC? Lakini tatu, na kubwa zaidi ni kwamba haya yalifanyika kwa bahati mbaya katika misingi ya kusoma na kujifunza au wahusika walijua wanachotenda?
Menejementi ya TRL imeshindwa kulipa mishahara ya wafanyakazi. Imeshindwa kukarabati miundombinu ya reli. Imeshindwa kulipa dola 3 milioni kwa serikali kama pango la kukodishwa.
Hata kwa yote haya, bado serikali inasema, “inataka kununua hisa za RITES” na kumbembeleza mwekezaji kuuza hisa zake.
Hicho kinachoitwa, “hisa za RITES” kinatoka wapi wakati mwekezaji ameshindwa masharti ya mkataba wa ukodishaji? Je, hili nalo linahitaji kukaa darasani kwa miaka mingine 10 au 15 kujifunza?
Kama serikali ya CCM imeshindwa kujifunza na kufuzu kwa kipindi chote hiki, ni muhimu ikakaa kando na kupisha vyama vingine.
Sasa ni wazi kuwa CCM yaweza kujifunza ikiwa nje ya madaraka; ikifuzu ndipo irejee kwenye mbio za kuwania utawala.
Vinginevyo, kwa staili hii ya uongozi, watawala kutoka chama hiki wataendelea kujifunza kila siku na huku jahazi likizidi kuzama; kwani hawafuzu.
Watu wa Visiwani wana usemi unenao, “Baharia hajifunzi jahazi kwenye upepo mkali.” Vivyohivyo CCM haiwezi kuachiwa kuendelelea kujifunza baharini wakati wa dhoruba.
Tatizo letu nini?ni elimu isiyotoshoreza matakwa ya jamii yetu au ni vichwa vibovu.Kama ni elimu yetu inawalakini tufanye nini?
Kama ni vichwa vibovu uhuru tuliomba wanini?Au ni laana kutoka kwa Mweyezi Mungu?
Au ni kutoelewa mbinu za kibepari maanake miaka mingi tulikuwa na serikali ya kijamaa?
Tuwache kuendesha nchi kishabiki turudi kwenye drawing board,uozo na ubutu wa mikataba ni nyingi kiasiinatia kichefuchefu.
Kashafa ,uzandiki,wizi,uvujaji wa mali ya umma ni kama milipuko ya volcano.
Bunge limekuwa kubwa lakini halina uhodari wa kutunga sheria.
Kila kukicha majimbo ya uchaguzi na wilaya zinaongezwa sio kumletea mwananchi maendeleo bali kumuongezea gharama za uendeshaji.Mwenye macho haambiwi tazama.Hivi huyo Baba wa Taifa mlikuwa mnamelewa au mlikuwa wavivu wa kujifunza a,e,i,o,u.
DAAAH NCHI HII NIMESHAKATA TAMAA NA NCHI HII,MAANA WATU KADRI WANAVYOELIMISHWA KUHUSU UBAYA WA CCM NDIO KWANZA WATAIPA KURA YA KISHINDO MWEZI OCTOBA,MIE NINGESHAURI VIONGOZI WA DINI WANGEENDESHA MAOMBI YA MWEZI MZIMA MUNGU ATUANGAMIZE WATANZANIA WANAFIKI WOOTE,AWABAKIZE WANAFUNZI WA VYUO VIKUU,NA WATOTO WETU WAANZE KUIJENGA TANZANIA YENYE NEEMA,LAKINI TUKITEGEMEA BALLOT BOX CCM ATATAWALA MIAKA 7000