Serikali haina hata busara ya kukopa?


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 01 February 2012

Printer-friendly version
Tafakuri

NINAKUMBUKA mwaka 1990 serikali iliwafukuza madaktari kama hawa inaovutana nao sasa. Walikuwa na madai.

Bodi ya Hospitali ya Muhimbili iliyokuwa chini ya Kitwana Kondo, ilipuuza madai hayo na kuamua madaktari wafukuzwe.

Siku moja tu baadaye, madaktari mabingwa nao wakaanza mgomo, wakaitisha mkutano na kuamua kwenda wizarani kumuona waziri wa afya.

Msafara wao ukageuka maandamano kuelekea Ikulu. Kabla ya kufika, ikajulikana Rais Ali Hassan Mwinyi hakuwepo. Maandamano yakaenda Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mashuhuda wanakumbuka vema madaktari waliokuwa wamekusanyika ukumbi mmoja eneo la Muhimbili walivyopata nguvu zaidi baada ya kuwasili kundi kubwa la wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam sehemu ya Mlimani. Wakati huo Rais wa Serikali ya wanafunzi wa Chuo Kikuu hicho akiitwa Kimaro, mwanafunzi wa shahada ya udaktari.

Baada ya wanafunzi wa Mlimani kufika Muhimbili, hali ya hewa ilibadilika na watu wakaamua kuingia mitaani.

Vyombo vya dola vilitumika kuwatoa madaktari wanafunzi Muhimbili, lakini pia vilitumwa kudhibiti wanafunzi wa kampasi ya Mlimani wasijiunge na wenzao wa Muhimbili.

Kwa bahati mbaya polisi na usalama wa taifa hao hawakufanikiwa lengo lao. Walikamata mabasi ya Chuo Kikuu yaliyokuwa yamechukuliwa na wanafunzi kwa nguvu kuwapeleka Muhimbili, lakini baadhi walifanikiwa kupenya na mabasi mengine kupitia njia za panya na wale waliozuiwa walitumia daladala hadi kufika Muhimbili.

Maandamano yalianzia Muhimbili saa nne hivi asubuhi na kufika lango kuu la kuingia kwa Waziri Mkuu yapata saa tano. Waandamanaji wakapiga kambi hapo hadi saa 11 jioni. Ndani ya ofisi hizo, waliingia wawakilishi wa madaktari miongoni mwao akiwa Profesa Shaba.

Baada ya vuta nikuvute ya zaidi ya saa saba, serikali ilitengua amri ya kuwafukuza madaktari wale, maandamano yaliyokuwa yameanzia Muhimbili yakahalalishwa na kuruhusiwa kurejea yalikotoka kwa ari kubwa.

Ni dhahiri na katika sakata hili, hata kama serikali ilikuwa imetekeleza wajibu wake kwa kufukuza madaktari wanafunzi waliokuwa wamegoma, na hata kama madaktari walikuwa wamevunja sheria, mwishowe ilishindwa. Ilichotaka zaidi ni kurudisha utulivu Muhimbili.

Tangu mgomo wa sasa wa madaktari uanze Muhimbili, nilijisemea moyoni kwamba hatua za kuwaondoa kazini na kuwarejesha wizarani hata kama zilikuwa sahihi namna gani kisheria, hazikutokana na uamuzi wa hekima na busara. Nitafafanua.

Aliyeanzisha zogo hili ni serikali. Imelianzisha kwa kushindwa kutimiza wajibu wake kwa wakati – kulipa posho za madaktari. Kwa hiyo, madaktari walipogoma, kwa hakika walipaswa kuifikisha serikali mahakamani kwa kukiuka mkataba, kimsingi mkataba ambao Mkurugenzi Mkuu wa Muhimbili aliokuwa anadai kuwa madaktari walikuwa wameuvunja, haukuwapo maana tangu awali serikali ilikuwa imeshauvunja. Kisheria haupo!

Ndiyo! Serikali ilivunja mkataba huo kwa kutotimiza wajibu wake. Tena wakati imeuvunja madaktari wanafunzi waliendelea kufanya kazi, hadi walipoona maisha yao yako hatarini kwa kuwa hawana chakula. Wakaamua kupumzika kusubiri chakula.

Umma unamfahamu Mkurugenzi Mkuu wa Muhimbili, Dk. Merina Nyelekela. Hakuna anayeweza kupinga uwezo wake wa uwajibikaji, uhodari wake na jinsi alivyojijengea sifa kwa alivyoendesha Chama cha Madaktari Wanawake (MEWATA) hasa kampeni dhidi ya saratani ya matiti. Huyu ni mtaalam wa tiba aliyepata tuzo kadhaa za kimataifa kwa uchapaji kazi, weledi na uwajibikaji uliotukuka.

Mama huyu ni mwanamke wa kwanza kuongoza Muhimbili, taasisi muhimu kwa maendeleo ya jamii na yenye changamoto nyingi na ngumu kuiongoza. Watu wengi wana imani atamudu kuiongoza kwa ufanisi.

Hata hivyo, wakati wa kushughulikia mgogoro wa madaktari wanafunzi inawezekana alishauriwa vibaya au amejikuta tu akitekeleza maamuzi ya warasimu wasiokuwa na soni wala huruma watokao makao makuu ya Wizara ya Afya. Hapa ndipo shida inapoanzia kwamba Mama huyu aliyeongoza mageuzi makubwa ya kushughulikia tatizo sugu la afya ya wanawake wenye saratani kiasi cha kuifanya serikali kujipanga upya, badala ya kuachwa aendeshe Muhimbili kiweledi, ameingizwa katika mgogoro wa kulazimishwa na madaktari. Namuonea huruma sana.

Dk. Njelekela hakuchelewesha posho za madaktari wanafunzi. Hii ni kazi ya mikono ya warasimu wa Hazina au Wizara ya Afya. Lakini zogo haliko Hazina wala wizarani, liko Muhimbili na hospitali zote za umma kwa sasa.

Nikiunganisha maamuzi ya kurejeshwa wizarani madaktari wanafunzi na wengine kupangiwa hospitali zilizowakataa na uamuzi wa juzi wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda wa kuwataka warejee kazini mara moja vinginevyo wamejifukuzisha, ni dhadhiri mgogoro sasa umepanuka na kwa kawaida kila mgogoro kati ya serikali na madaktari unapoibuka anayeshindwa ni serikali.

Kama ilivyokuwa mwaka 1990, naona historia ikijirudia kwa serikali kuvuna aibu katika mgogoro mpya na madaktari. Inawezekana watawala pale Ofisi ya Waziri Mkuu au Wizara ya Afya au Menejimenti ya Utumishi Umma wanaamini wameshika mpini na madaktari wamekamata makali. Ukweli, ni kinyume chake. Hakuna uwezekano wowote ninaoona wa kuchukua madaktari kokote ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania au hata nje kuziba nafasi za wote wanaokusudiwa kufutwa kazi. Kwa serikali kujiaminisha kuwa itawapelekesha madaktari ni kujidanganya. Na itaumbuka karibu.

Kwa miaka mingi nchi hii imekuwa mali ya wanasiasa, uzingatiaji wa weledi katika kuamua mambo ya msingi hauzingatiwi sana, ndiyo maana sasa tunaingia katika mapambano ya kitaifa ya kila kundi katika jamii kutetea maslahi yao kama kundi.

Wabunge ambao waliaminiwa kuwa watetezi wa kila sehemu ya jamii, wameshajiamulia kwamba wao wanatafuta chao, tena mapema tu. Mikopo mikubwa isiyokuwa na riba ni yao kwa gharama za walipa kodi, posho nzuri za vikao ni zao. Kimsingi, wabunge waliopaswa kubeba suala hili la madakrati ili kuiwajibisha serikali isije ikaathiri huduma za tiba, hawawezi kwa kuwa wenyewe wana mgongano wa kimaslahi na haki za makundi mengine katika jamii.

Wabunge wetu sasa wanasema waziwazi kuwa wanastahili kulipwa zaidi kwa kuwa wanagawa fedha kwa wapiga kura wao, lakini hawataki kushawishi kila kundi lilipwe vizuri ili kuwanusuru wao kuwa ATM za wapiga kura, pia hawataki kuona mifumo ikibadilika ili taifa liendeshwe kwa misingi ya usawa na haki katika kupata kipande cha keki ya taifa.

Hali hii ndiyo inayozaa mapambano ya makundi kutetea haki zao huku kila kundi likishambulia jingine kwa kulituhumu kujinufaisha au kuliona kama lisilostahili kupata hicho linachopata.

Pinda kwa maana ya kauli yake ambayo ni kama msimamo wa serikali kwa madaktari amethibitisha dhana hiyo ya makundi – kwamba nani anastahili na nani hastahili, hatoi kauli kama aliyotoa wiki iliyopita alipofanya mkutano na waandishi wa habari kuzungumzia mambo mbalimbali ya utendaji wa serikali tangu Juni mwaka jana.

Katika mkutano huo, Pinda alielekea kuhalalisha posho nono kwa wabunge na kigezo pekee alichotumia ni kwamba wanagawa fedha kwa wapigakura! Yaani nyongeza ya posho ya wabunge kutoka Sh. 70,000 hadi 200,000 kwa siku si kwa mahitaji yao, ila ya wapigakura!

Hakika unapokuwa na viongozi wenye majibu mepesi namna hii, tutarajie nini katika jambo zito kama la mgomo wa madaktari? Vifo vingi, kutaabika kwingi na mwishowe serikali kuangukia pua kwa sababu imekataa tangu awali kutawaliwa na hekima katika kushughulikia matatizo. Tusubiri tuone.

0
No votes yet