Serikali ijiangalie upya


editor's picture

Na editor - Imechapwa 25 January 2012

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

HATUAMINI kamwe kama serikali haina fedha za kuipa mahakama ili iendeshe kesi zilizofunguliwa na wabunge walioshindwa katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2010.

Hatuamini kwa sababu Idara ya Mahakama mapema kabisa ilipeleka bajeti yake serikalini kueleza mahitaji yake kifedha ili kutimiza wajibu wake muhimu na wa kipekee wa kusimamia utoaji wa haki.

Katika kesi hizo, wagombea walioshindwa wanatoka katika vyama vyote vilivyoshiriki uchaguzi. Wapo waliotoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilichotangazwa mshindi na kuunda serikali.

Wapo pia waliogombea kupitia vyama vinavyoitwa vya upinzani ambavyo wengine huviita vyama vya mageuzi.

Kama tunayo serikali makini na inayojali dhana ya utoaji wa haki, tusingesikia taarifa hizi.

Inajulikana Mahakama ni mhimili mmoja wapo wa dola kama ilivyo Serikali. Basi tulitarajia serikali ingehakikisha inaiheshimu mahakama.

Lakini pia, mbona hali halisi inaonesha nyingi ya kesi zilizokwama kuendeshwa ni zile zilizofunguliwa na wagombea wa upinzani dhidi ya wale wa CCM waliotangazwa washindi?

Baadhi ya kesi zilizofunguliwa na wagombea walioshindwa wa CCM zimekwisha, zikiwemo zilizo ngazi ya rufaa katika Mahakama ya Rufaa.

Vilevile, Watanzania wanashuhudia baadhi ya kesi za wagombea walioshindwa wa CCM zikisikilizwa kila wakati huku zile za wagombea wa upinzani zikisubiri fedha.

Kwamba imetokea tu hivyo, ni vigumu kuamini. Serikali iseme imekuaje kesi nyingine ziende vizuri, lakini nyingine zikwame?

Kwanini watu wasijenge mashaka kuwa labda ni mpango mahsusi wa serikali, ambayo inaongozwa na CCM, kuinyima Mahakama fedha kwa majimbo isiyo na maslahi nayo kama kesi zitasikilizwa na kuipatia fedha za kutosha kusikiliza kesi ambazo ina maslahi nazo.

Huu ni mfumo mbaya wa serikali kutekeleza wajibu wake wa kuongoza kwa kuheshimu misingi ya katiba inayohimiza uongozi wa haki bila upendeleo wa aina yoyote.

Kasoro hii kubwa inaendeleza mwenendo mbaya wa serikali wa kutumia vibaya fedha za umma na kulazimika kujikuta ikishutumiwa kwa kutokuwa na nidhamu katika matumizi ya fedha za umma.

Tunataka serikali ijitambue na kuacha mfumo huu. Ni vema viongozi wakabadilika na kuishi katika kuzingatia ukweli wa mambo ulivyo.

Vinginevyo, wajue Watanzania si watu wa kubezwa. Wanastahili kuheshimiwa maana siku ya mwisho ni wao wa kuamua ni vipi wanataka waongozwe.

0
No votes yet