Serikali ikiishiwa hoja, huongea kwa risasi


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 01 June 2011

Printer-friendly version

KAMA kawaida, mauaji ya raia yanayofanywa na polisi huacha maswali mengi. Utata unaoanza kuzoeleka machoni mwa raia ni vifo vya wananchi vinavyotokea mikononi mwa polisi.

Taratibu jambo huzika imani ya wananchi juu ya chombo hicho cha kulinda amani. Mwisho wa hali hiyo hapatakuwa tena na nafasi ya kuifufua imani hiyo.

Tanzania ni moja ya nchi chache za Jumuia ya Madola ambayo polisi wameruhusiwa na kuachwa wabebe silaha. Uamuzi huu nisioujua historia yake, una hatari kubwa kwa usalama na amani ya taifa na hakuna dalili kama watawala wetu wanaliona hili.

Ndani ya nchi moja kuwa na majeshi zaidi moja, yenye ruhusa ya kubeba silaha si jambo la heri hata kidogo. Hapa nchini kuna Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ, Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, si ajabu hata mgambo, wote wanabeba silaha za moto.

Yametokea mauaji ya raia huko Tarime mkoani Mara. Mwanzo tuliambiwa ni wezi wa dhahabu. Baadaye kidogo tukasikia serikali inatuma ubani kwa wafiwa. Hatimaye tukasikia mashindano ya kutengeneza majeneza kati ya serikali na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Haikuishia hapo, likafuata tukio la kuiba maiti na kuzitelekeza barabarani huku kukiwa na habari kuwa mahali pengine polisi walilazimisha mazishi ya miili ya watu waliokufa. Yaelekea kuna mengi tusiyoambiwa na hata kama tukiambiwa kwa kuchelewa, hayatakidhi haja na kiu ya watu kuhusu sakata hilo la Tarime.

Kinachoonekana wazi kuwa kilitokea na kinaendelea kusumbua vichwa vya watu, ni ukweli kuwa serikali iliishiwa hoja katika kujenga uhalali wa wawekezaji kuendelea na shughuli zao, kwa hiyo, risasi zikatumika kujibu hoja.

Hii ni kawaida kila inapotokea wakubwa wameishiwa hoja mbele ya wananchi. Hulazimika kutumia vitisho na ubabe ili kuhakikisha mawazo yao yanakubalika.

Katika mazingira ya maisha ya polisi, hili pia ni jambo la kawaida kwa sababu ndani ya kambi zao, ukuu wa mtu hujulikana kwa jinsi anavyoweza kutumia ubabe kutekeleza majukumu yake. Matumizi ya ubabe na risasi dhidi ya hoja halali za wananchi ni suala ambalo limezungumziwa na watu wengi.

Baadhi yao wemeonya juu ya uwezekano wa watu kujenga usugu wa kutojali wala kuogopa risasi au uwezekano wa kuzalisha tabaka lenye uchungu mkali unaotokana na uyatima na ujane wa kulazimishwa.

Uchungu wa namna hii huasisi visasi visivyokwisha katika jamii au kustawisha harakati za hatari katika taifa. Kutokana na mwingiliano wa mahusiano ya wananchi, kifo cha raia mmoja kinagusa pande nyingi na sekta nyingi, na kwa hiyo uchungu ule unaenea kwa kasi kila sehemu.

Kuyasema haya mbele ya watawala wa sasa ni kutafuta ubaya, lakini kwa wenye hekima, ni ushauri wa thamani sana katika kuliangalia suala hili kwa mtazamo mpya.

Matumizi ya risasi na mabomu, kwa upande mwingine, yanadumaza uwezo wa watawala kufikiri kwa kina na kutafuta suluhisho la matatizo yanayowakabili wananchi. Haihitaji shahada wala fedha za kigeni kuamua kutumia mabomu na risasi na kwa hiyo watawala wazembe na wala rushwa huonyesha hulka yao kwa kuamuru kutumia vitu hivi ili kuzuia wananchi wasihoji masuala ya msingi.

Katika tawala zinazothamini utu na uhai wa binadamu au hata kutopenda kusikia milio ya risasi, askari hupata tabu sana kuamua kufyatua risasi kwa sababu mwisho wa siku atapata tabu kujieleza alivyoitumia hiyo risasi. Na pale inapoonekana hakutumia akili sawasawa, hupata adhabu hata kama nia yake ilikuwa njema.

Matumizi mabaya ya silaha yaweza kumshusha cheo askari au kamanda wake, yaweza kumzuia asitumie silaha tena na yanaweza kumwondoa katika jeshi la polisi.

Wengi wanawashangaa Wamarekani waliposikia umma wa Wamarekani wanataka kujua kwa nini Osama Bin Laden aliuawa katika operesheni ya vikosi maalum vya makomandoo. Kwa akili za kawaida, wengi walitamani Bin Laden, akionekana popote, auawe mara moja bila kuchelewa.

Lakini katika utawala wa kweli wa sheria, hata jambazi ana haki ya kuishi au kusikilizwa. Vyombo vyetu vya usalama na dola vinakosa habari muhimu kutokana na tabia hii ya kuua watu hovyo kwa kisingizio cha kuwa ni majambazi.

Fikra nyingine ambazo zinaweza kujengeka miongoni mwa watu wa ndani na nje kuhusu matumizi ya risasi na mabomu, ni kuwa labda viongozi wa serikali hiyo wana hofu kupita kiasi. Katika hali ya kawaida, haitarajiwi serikali ilazimike kutumia risasi kujibu hoja za wapiga kura wake.

Kwanza, si sahihi kutumia risasi na mabomu kujibu hoja. Pili, serikali hulindwa na wananchi wenyewe walioichagua na kuiweka madarakani.

Lakini hapa nchini katika kipindi cha miezi sita sasa tumeshuhudia upinzani mkubwa wa wananchi dhidi ya serikali waliyoichagua na kuiweka madarakani. Hili lilitosha kuifanya serikali ikune kichwa na kujieleza vya kutosha ili kuhalalisha matumizi ya risasi badala ya hoja.

Kwa serikali makini, ingekaa na wapinzani (wito huu ulitolewa baada ya uchaguzi) wanaodaiwa kuchochea upinzani dhidi ya serikali, ili kubaini njia mwafaka ya kutumia hoja badala ya risasi. Taaluma ya utawala bora inaeleza wazi kuwa matumizi ya nguvu ya serikali dhidi ya watu wake ni dalili ya kueleza hofu kwa watu wake.

Hofu hii huwafanya polisi watumie risasi na mabomu kwa sababu wakiulizwa na serikali huiambia kuwa wamefanya hivyo ili kuiokoa na upinzani.

Kwa hili la Tarime, fikra zaidi zinajitokeza. Kwamba, askari walioua si raia wa nchi inayoitwa African Barrick Gold, bali raia wa Tanzania wanaotumiwa na mgodi kuwaua raia wenzao.

Mfumo wa uchumi na ukata wa taifa letu, umekabidhi uhai wa wananchi mikononi mwa mamluki wanaolipwa na mgodi. Hii haina tofauti na enzi za ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini (Apartheid).

Chini ya mfumo huo, askari weusi walikuwa wanatumika kuwaua weusi wenzao. Ni kwa sababu posho waliyokuwa wanalipwa ilikuwa kubwa kuliko mshahara uliokuwa unalipwa na serikali kwa askari wake.

Kuonyesha shukrani kwa wenye mgodi, askari wanatii amri kana kwamba hawana akili sawasawa. Hatari yake ni kwamba inaweza kufika siku askari hao wakaingiwa huruma, wakaungana na wanachi kupinga uonevu. Tusiruhusu kufika hapo.

Mwandishi wa makala haya, Juma Said amejitambulisha kuwa ni mtanzania anayeishi nchini Canada. Anasoma MwanaHALISI kupitia mtandao wa intaneti.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: