Serikali imejipalilia migogoro


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 08 April 2008

Printer-friendly versionSend to friend

MIEZI mitano tu tangu serikali ikabidhi Shirika la Reli nchini (TRC) kwa kampuni ya kigeni iitwayo Rite, iliyoshinda zabuni ya kuwekeza katika shirika hili lenye miundombinu ghali mno, tayari wawekezaji hao hawana uwezo wa kulipa wafanyakazi wake.

Na ukweli huu unakuja mwezi mmoja tu baada ya wawekezaji hao kusaini makubaliano na wafanyakazi, ya kuwalipa mishahara mipya inayozingatia ongezeko la kima cha chini.

Mwezi uliopita, wafanyakazi wa inayoitwa sasa kampuni ya Reli Tanzania (TRL), waliamua kugoma baada ya jitihada zao za kushinikiza menejimenti ya Rite, kuongeza mishahara, kushindwa kuzaa matunda.

Jambo la kushangaza ni kwamba makubaliano hayo yalifanywa mbele ya wawakilishi wa serikali. Masikini roho zetu Watanzania, wawekezaji wameshindwa ahadi.

Kwa sababu ya kutotimiza ahadi waliyoiweka kutokana na makubaliano waliyofikia na wafanyakazi, serikali imelazimika kubeba mzigo isioutarajia wa kuwalipa wafanyakazi hao mishahara yao.

Imelazimika kuahidi kutumia Sh. 3.6 bilioni kwa ajili ya kulipa mishahara hiyo kwa miezi mitatu ijayo, hadi Agosti kampuni ya wawekezaji itakapopata uwezo.

Haya ndio matunda ya uzembe na ufisadi. Inafahamika wazi kwamba kabla ya wawekezaji kuwasilisha maombi ya kupewa kuchukua uendeshaji wa TRC, kuliandaliwa ripoti inayoonyesha hali halisi ya kampuni.

Ni ripoti kama hii inayojenga taswira ya shirika linaloombewa uwekezaji wa kibinafsi. Inaonyesha kuwa hakukuwa na uadilifu katika kuandaa ripoti hiyo na matokeo yake, waombaji walipata matumaini ya kufanya biashara haraka.

Kwa mfano, tunaelezwa kwamba ripoti ilisema kuwa zipo injini 92 zitakazokabidhiwa kwa wawekezaji hao na kuanzia kazi haraka ili huduma za usafirishaji abiria na mizigo ziendelee.

Haikuwa. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda anawaambia wafanyakazi wa TRL kwamba zilizokabidhiwa ni injini 55 tu. Ziko wapi sasa injini 37?

Hapa kuna mambo mawili. Kwanza, ripoti imedanganya wawekezaji. Lakini pili, inaonekana kuna mpango wa kuficha ukweli ili kubeba wawekezaji.

Hii ilionekana kwenye ubinafsishaji wa kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) na hata kampuni ya gesi ya oksijeni (TOL). Mpaka sasa, serikali imepunjwa na wawekezaji kwenye fedha ilizoahidiwa kulipwa na wawekezaji.

Hali ya kampuni ya gesi inasikitisha. Tangu mwaka 1998, haijapata wawekezaji wa maana na kwa sababu hiyo, haina maendeleo yaliyotarajiwa wakati ikitangazwa kubinafsishwa. Hakuna gawio la maana hadi sasa kwa wenye hisa.

Kutokana na hali hiyo, tunaitaka serikali ichukuwe hatua madhubuti za kuhakikisha muwekezaji wa TRL anatimiza wajibu wake kama alivyoahidi katika mkataba.

Vinginevyo, serikali itarajie kuzaa migogoro mingine mikubwa TRL na mashirika mengine yaliyobinafsishwa kifisadi. Wafanyakazi wanaumia njaa wakati raslimali zao zinachezewa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: