Serikali imepata busara baada ya kuua, kujeruhi


editor's picture

Na editor - Imechapwa 22 June 2011

Printer-friendly version

BAADA ya kufanyika uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani nchi nzima Oktoba mwaka jana, uliibuka mgogoro mkubwa wa uchaguzi wa meya katika jiji la Arusha.

CCM ilifanya hila, ilikusanya madiwani wake na wa TLP wakafanya uchaguzi bila kushirikisha madiwani wa CHADEMA.

Mzozo mkubwa uliibuka kutokana na CCM kunyonga na kubaka demokrasia, haki na misingi ya utawala bora na sheria. CHADEMA wakatangaza mgogoro na serikali nchi nzima wakaandaa maandamano kupinga taratibu za uchaguzi ule, wakianzia na mkoa wa Arusha.

Ili kuzuia madhara, aliyekuwa waziri mkuu, Edward Lowassa alishauri CCM na CHADEMA wajadili suala hilo, lakini CCM walikataa. Madhara ya kukataa ushauri ule, CHADEMA waliandamana Januari 5, 2011 na serikali ikitumia ubabe kuzima maandamano yale watu watatu —Watanzania wawili na Mkenya mmoja—waliuawa.

Mbali ya vifo hivyo, wafuasi wengine wa chama hicho walijeruhiwa vibaya na wakafunguliwa kesi kwa madai walifanya maandamano yasiyo halali. Katika juhudi za kujinasua kwenye lawama serikali iliandaa vipindi vya propaganda chafu dhidi ya CHADEMA lakini haikuondoa ukweli serikali imeua watu.

CHADEMA walipata nguvu zaidi wakaendelea kufanya maandamano kulaani mauaji yale mikoa mingine. Matokeo yake chuki dhidi ya serikali imeongezeka sana.

Mfululizo wa maandamano hayo ya CHADEMA mikoani ni ushahidi kwamba ubabe na vitisho vya serikali havikusaidia.

Hatimaye, baada ya kuona giza mbele serikali imekubali ushauri wa Lowassa ikaamua kumpa kazi Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kukutana na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe kulipatia ufumbuzi.

Mwafaka umefikiwa; CCM imetoa meya huku naibu meya na mwenyekiti wa kamati ya uchumi na elimu wakitoka CHADEMA, huku TLP ikitoa mwenyekiti wa kamati ya fedha.

Tunapongeza juhudi za kumaliza uhasama kwa maslahi ya wananchi kwani ni ukweli usiopingika kwamba, lengo la vyama vyote ni kuwatumikia wananchi kujiletea maendeleo; wapunguze umaskini na kukuza uchumi.

Hata hivyo, tunasikitika kuona serikali imepata busara baada ya kuua watu wake pamoja na kuwasababishia watu wengine umajeruhi na wengine kuachwa vilema na kuwafungulia kesi.

Serikali ijue kwamba utawala wa mabavu ni chukizo, unaidhalilisha, na unaijengea uadui kwa wananchi wake. Tukio la Arusha liwe fundisho hata kwa migogoro mingine nchini.

0
No votes yet