Serikali inapokuwa na tabia ya Ndiuliza

SERIKLALI imekunja uso. Imejenga miraba – wanasema matuta au pingili – kuonyesha ukali usioweza kubishana nao.
Ninyi madaktari mnadai posho zenu? Sitaki kusikia. Kwanza bado wanafunzi tu wa mwaka wa tano. Toka hapa! Inang’aka.
Anatokea daktari mwenzao aliyepata cheo cha kiserikali. Anaahidi: Tutawalipa “kesho.” Kesho hii hapa, inaitwa leo. Hawalipwi.
Madaktari wanadai posho zao. Wapate mlo na nauli. Walipe pango kule wanakolaza mbavu; angalau wapate usingizi; wapate utulivu wa moyo na mwili ili waamke wakiwa na nguvu na utashi wa kusikiliza wagonjwa.
Wapi! Siku zinavyokwenda ndivyo serikali inaongeza matuta usoni na ndani ya kifua. Ndipo madaktari wanakunja mikono kifuani na kujisemea: Basi angalau tule ndipo twende kazini. Bado hakuna anayesikia.
Hatimaye madaktari wanalipwa posho lakini wanatawanywa – wanatolewa Muhimbili, ile hospitali kuu na chuo kikuu – na kusambazwa hospitali ndogo za jijini Dar es Salaam.
Ni kama serikali inasema hivi: Wakorofi eh?! Sasa tutaona nani ameshika mpini na nani ameshika makali. Tokeni mlikochagua kufanya kazi. Ondokeni karibu na mabingwa!
Mtindo wa serikali huo. Hadi madaktari wawe ombaomba. Lakini wakikunja mikono, serikali inasema wakorofi. Inasema siyo wazalendo. Inarefusha mjadala; inamwaga tuhuma na shutuma. Inawaambia wananchi, “…ona tuliowasomesha waje kuwatumikia; sasa wanawatelekeza!”
Kwani ni madaktari peke yao? Walimu nao wanalalamika. Wasikilize. Hawajalipwa mishahara. Wamecheleweshewa mishahara. Hawajalipwa posho ya usumbufu wakati wa kuhama. Hawajalipwa nyongeza ya mshahara. Hawajalipwa…hawajalipwa!
Muulize rais wao Gration Mukoba. Ana orodha ndefu ya madai ya walimu. Anasukumwa huku na kule. Anatuhumiwa na waathirika wa chelewachelewa ya serikali. Baadhi ya walimu wanamuuliza: Inakuwaje huyo rais mwingine anakuzidi kete?
Walimu nao wameishia kutishia kugoma.Wakifanya hivyo huambiwa wanatumiwa na vyama vya upinzani. Madai magumu; makali na ya kutisha.
Kumbe neema iko chama kilichopanga ikulu; na dhiki na malalamiko yako upinzani. Kumbe ukiwa na njaa ni mpinzani. Ukiwa na mahitaji mengine muhimu ya maisha ni mpinzani.
Pingili za serikali usoni na moyoni haziishii kwa madaktari na walimu wa shule za sekondari na msingi. Sikiliza kilio cha wanafunzi wa vyuo vikuu.
Mikopo kwa ajili ya elimu ya juu inacheleweshwa. Inatolewa kwa upendeleo. Mkondo wa kuipata ni mrefu zaidi ya ule wa kutafuta kazi. Wakitishia kugoma ili ujumbe ufike haraka, basi watakuwa wamejipalia mkaa.
Wanafunzi watalipuliwa mabomu ya kutoa machozi; watafukuzwa mithili ya swala; watapigwa virungu kama mkristo apigavyo nyoka; watawekewa askari vyuoni ili kuhakikisha hawafurukuti – vyuo vinakuwa kambi za askari.
Wanafunzi watafukuzwa kwa kutoa maoni yao kwa njia ya maandamano. Wale watakaoandamana kutetea wenzao, nao watafukuzwa. Hii ni moja ya kazi muhimu za wakuu wa vyuo: Ku-fu-ku-za.
Hiyo ndiyo sura ya mazingira ya kila mmoja anayeidai serikali. Hata wastaafu wa iliyokuwa Jumuia ya Afrika Mashariki; pamoja na umri mkubwa walionao, wamekuwa wakiswagwa kama wahalifu.
Kuna wakati walilala barabarani jijini Dar es Salaam karibu na daraja la Selander. Mara nyingine walikaa barabarani karibu na mahakama ya rufaa kusisitiza madai yao. Mara zote waliamkiwa kwa vitisho – virungu, bunduki na maji ya washawasha.
Kumbukumbu za wanaodai chao au cha jamii kukumbana na nguvu ya dola ziko hai katika maisha ya wananchi. Hata vyama vya siasa vimezuiwa mara kwa mara kufanya maandamano.
Hivi karibuni wanaharakati walizuiwa kuandamana. Walitaka kusisitiza umuhimu wa mijadala ya kutafuta “katiba mpya” na hasa kutaka dunia ijue kuwa sheria ya mkondo wa kupata katiba ni chafu, katili na isiyokubalika.
Kila watawala wanapolalamikiwa wanakuwa wepesi kukasirika; kufura kwa hasira na ghadhabu, kutafuta kujikosha na hata kusogeza lawama kwa mwingine; hata Mungu na hatimaye kutumia “bunduki kuua sisimizi.”
Serikali inafanana Yasin Kayanda. Huyu ni kijana. Ana miaka 40 – umri wa kujinadi na kujigamba.
Ana mke na watoto. Anaweza kupata mshahara wake na marupurupu mengine kama anavyostahili. Lakini akafuja kila senti.
Atasahau ana kichanga kinachohitaji maziwa – ama ya kopo au halisia yatokayo moja kwa moja kwa mama ng’ombe.
Atasahau nauli ya watoto. Hatajua kuwa chumvi au sukari imeisha nyumbani kwake. Hatakumbuka deni dukani wala mkopo wa Sh. 2,000 aliopewa na Paulina, mfanyakazi mwenzake alipokuwa amekosa nauli.
Sasa mtoto au mke wake atakapotoa taarifa, “…hakuna sukari” au “chumvi imeisha,” sikiliza majibu. Nyumba itawaka moto, “Ninyi mnatumia vibaya. Vitu vingine mnagawa au watoto wanalamba sukari.” Ukali!
Jaribu kuuliza serikali: Iko wapi bajeti iliyoidhishwa na bunge, ya matumizi nchi nzima – wizara na idara za serikali, mashirika ya umma – kwa ajili ya sherehe za kuadhimisha miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika? Wanayo? Kiasi gani?
Zilifanyika sherehe badala ya kumbukumbu. Kwa kuangalia kiasi kilichotumika katika wizara moja au idara; halafu ukajumuisha matumizi kote zilikofanyika sherehe, hutahitaji mtaalam kukueleza mabilioni ya shilingi yaliyotumika.
Sasa iulize serikali: Kwa nini hulipi posho za madaktari mpaka waingie kwenye mgomo? Kwa nini hulipi posho za walimu? Kwa nini hulipi mikopo ya wanafunzi hadi waanze kuandamana?
Uliza: Kwa nini unataka kufunga vyuo vikuu kwa kufukuza wahadhiri kwa njia ya kuwapa mishahara midogo na kusababisha wahamie nchi nyingine?
Hutapata jibu. Utakumbana na ukali wa kauli, pingili za usoni na vitisho. Bali wanaodai haki wanaweka rekodi ya watawala kuwa na tabia ya “bwana haambiliki.”
Ndiuliza ni moja ya vitabu nilivyoandika. Najua siyo kawaida kuandika kitabu na kukifanyia mapitio wewe mwenyewe.
Lakini yakitokea mazingira ambayo yanafanana na yaliyomo katika kitabu, sitasubiri kuomba ruhusa kutoka kwa yoyote ili niweze kuunganisha ya leo na yaliyomo katika kitabu.
Mhusika mkuu katika kitabu ni Ndiuliza – mdudu anayependa kula mahindi. Atasubiri mahindi yakaribie kukomaa shambani. Atajivuta taratibu hadi kwenye ndevu za hindi.
Ataguguna ganda. Atafikia hindi. Ataanza kuguguna hindi. Akinogewa atapenya gunzi. Atafyonza utomvu na kusahau kuwa humo alimo siyo kwao.
Marafiki wa Ndiuliza watamwita na kumwambia atoke haraka, lakini atajibu, “Subiri tu, nitatoka.” Atakuja mwenye shamba. Atavuna mahindi. Atayapeleka nyumbani.
Watoto watayatoa maganda. Watayaweka kwenye chungu chenye maji. Watayabandika motoni. Yatapikwa hadi yaive. Naye Ndiuliza “ataiva.” Laiti watawala wangekataa kuwa Ndiuliza – haambiliki.