Serikali inaposhindwa kutumia wazalendo wataalam


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 20 January 2010

Printer-friendly version
Profesa Mwesiga Baregu

UNAPOANZA kusoma makala hii, chukua kalamu na karatasi. Anza kuorodhesha watu unaowajua ambao ni waajiriwa serikalini lakini wana nafasi za kisiasa katika vyama vya siasa.

Zoezi hili sikukupa mimi. Amekupa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejementi ya Utumishi wa Umma. Anaitwa Hawa Ghasia.

Waziri anasema serikali imekataa ombi la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kumpa mkataba mpya Profesa Mwesiga Baregu kuendelea kufundisha chuoni hapo kwa kuwa “anajihusisha na mambo ya siasa.”

Mtaalam wa sayansi ya jamii na mahusiano ya kimataifa, Profesa Baregu amekuwa miongoni mwa walimu lulu chuoni na katika vyuo mbalimbali katika Afrika Mashariki na Kusini.

Baregu ni mtaalam pia wa menejimenti ya migogoro katika kanda ya Maziwa Makuu ya Afrika na Kusini mwa Afrika.

Alhamisi iliyopita, waziri Ghasia aliibuka na kile alichoita, “ufafanuzi wa sakata la ajira” ya Profesa Baregu. Alisema “Waraka wa Utumishi Namba 1 wa mwaka 2000” ndiyo ulitumika kumnyima ajira mwalimu huyo kipenzi cha wanafunzi na wahadhiri Mlimani.

Alisema serikali imemnyima Profesa Baregu mkataba mwingine chuoni kwa kuwa “amekosa sifa ya kuendelea na utumishi wa umma kutokana na kuwa kiongozi wa kisiasa ndani ya CHADEMA” – Chama cha Demokrasia na Maendeleo.

Aidha, waziri amemtaka Profesa Baregu kutafuta kazi nje ya nchi iwapo bado anatamani kuendelea kufundisha katika chuo kikuu. Baregu ni mjumbe wa Kamati Kuu na Baraza Kuu katika CHADEMA.

Sasa angalia wanaokuzunguka. Nani ana ajira ya serikali au kampuni au shirika lake na bado anashika nafasi ya uongozi ndani ya chama cha siasa? Orodhesha, kisha linganisha na kauli ya Hawa Ghasia. Kama waziri Ghasia siyo mwongo, basi ni msanii wa viwango vya chini kabisa.

Lakini kabla ya kuangalia hali halisi katika serikali na vyama, hebu tujadili kwa ufupi tu, usomi na siasa.

Usomi wa viwango vya Profesa Baregu siyo wa ubabaishaji; kujipendekeza ili upate fadhila au cheo serikalini; siyo ule wa kusifia na kutukuza vimbweneleni wa kisiasa ili kupata safari katika ndege moja na rais. Baregu na wasomi wa viwango vyake, wamevuka ngazi hiyo ya “hewala bwana!”

Hata darasani hafundishi ubishi wa mitaani wala kukaririsha kama wafanyavyo walimu wa watoto katika masomo ya dini. Kazi yao kubwa ni kuhakikisha wanawezesha wanafunzi kufikiri na kupata zana za kufanyia uchambuzi.

Mwanafunzi aliyeokwa kwenye meko ya aina hii siyo tegemezi tena kifikra. Anajua jinsi ya kujitafutia; kukusanya na kutumia alichopata. Upevu utokanao na maarifa yaliyopatikana kwa njia hii, huweza kuwa wa mafao kwa jamii, chuo, chama na hata mtu binafsi.

Kwa msingi huo hatutarajii msomi awe dhaifu kifikra na ajinyenyekeze na kujikomba ili apendwe au apewe nafasi ya kisiasa katika chama kikubwa au kidogo.

Uhuru alionao kifikra unaendana na uhuru wake wa kuchagua – iwe katika siasa na vyama, sera na viongozi au vionjo vingine vya binadamu, kama michezo. Hapa ni muhimu kusema kuwa mwalimu wa chuo kikuu aweza kuwa na haya yote kama raia mwingine yeyote.

Tatizo la baadhi ya watawala na watumishi wao ni woga. Wengi wanaogopa watu wenye fikra pevu, wanaojitegemea na wasiojipendekeza. Huwaona ni hatari na daima hufikiri kuwa “wanaeneza upinzani” kwa wengine.

Inapotokea mtu wa aina hiyo akawa chuo kikuu na akawa mwalimu, basi akili fupi ndani ya serikali huona kuwa uwezo wa muhusika “utapotosha” wanafunzi na hata walimu wengine.

Ni fikra finyu. Hii haina maana kwamba Profesa Baregu ndiye pekee mwenye fikra pevu. Wengine wa aina yake waweza kuwa kwenye orodha ya kung’olewa. Siyo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam peke yake bali hata vyuo vingine vya umma. Kila mmoja kwa wakati wake na kwa kadri anavyouma.

Kwa hiyo, Waraka wa serikali Na. 1 wa mwaka 2000, ni matunda ya woga na ufisadi wa kisiasa. Ulilenga kunufaisha CCM na kuhujumu vyama vingine. Waziri Ghasia, bila aibu wala chembe yoyote ya uchambuzi, ananukuu waraka huo kuhalalisha haramu ya kukosesha wanafunzi mwalimu mahiri na wanayemhitaji.

Sasa tuangalie mifano michache ifuatayo ili tuweze kuona jinsi waziri anavyoweza kutumikia maslahi finyu ya CCM au ya watu binafsi na waliochoka.

Chama Cha Mapinduzi kimetenga nafasi za ubunge kupitia vyuo vikuu kwa lengo la kuvuna wanataaluma. Huko ndiko alikopatikana Asha-Rose Migiro. Aliingia bungeni kupitia nafasi za vyuo vikuu. Bado Migiro ni mwajiriwa wa UDSM.

Je, CCM walipanga kupata msomi aliyeko mitaani? Asiye na kazi au anayeuza genge la nyanya na pilipili? Kama walipata msomi anayefundisha, tena katika chuo kikuu cha serikali, wanawezaje kuleta hoja na hata Waraka ambao unawazidi kimo? Unafiki.

Mkufunzi katika idara ya historia UDSM, Dk. Rehema Nchimbi, ni mjumbe wa NEC kupitia Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT). Huyu ni mmoja wa watumishi wa umma waliojipachika katika kwapa la CCM na wanaendelea kulindwa kwa hoja ya “huyu ni mwenzetu.” Hivi sasa, ni mkuu wa wilaya.

Hajafukuzwa kazi UDSM. Hakuandikiwa barua ya kuelezwa kuwa hatua yake ya kuwa mjumbe wa NEC inakwenda kinyume na waraka wa utumishi.

Tarimba Abas, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bahati Nasibu ya Taifa (GBT) ni diwani wa Kata ya Hananasif, Kinondoni, Dar es Salaam. Ni mtumishi wa umma ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya na Mkutano Mkuu wa wilaya. Ghasia, Waraka unasemaje?

Huyu, kama walivyo wengine, hajaulizwa; hajaguswa wala hajasakamwa kwa kujishughulisha na siasa wakati ni mtumishi wa umma. Ghasia analijua hili.

Profesa Robert Mabere, kama Profesa Baregu, amestaafu utumishi wa umma, lakini serikali imempa mkataba. Ni mhadhiri katika idara ya uchumi UDSM lakini pia ni mwenyekiti wa tawi la CCM chuoni hapo. Ghasia, Waraka unasemaje?

Elisha Kaaya ni Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC). Pamoja na kushikilia nafasi hiyo nyeti serikalini, Kaaya ni mjumbe wa NEC ya CCM. Ghasia, Waraka unasemaje?

Dk. Kakyondo ni mhadhiri katika Kitivo cha Sayansi ya Kompyuta UDSM. Taarifa zinasema Dk. Kakyondo ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Mkoa wa Tanga kutokea wilaya ya Lushoto. Hajafutwa kazi kwa kushiriki siasa. Ghasia, Waraka unasemaje?

Ole Medee, Meneja Rasilimali Watu na Utawala katika Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA). Yeye ni kamanda wa Vijana wilayani Arumeru – nafasi nyeti ya kuunda vijana-siasa wa CCM. Ghasia, Waraka unasemaje?

Dk. Sengodo Mvungi, mhadhiri mwandamizi aliyestaafu Kitivo cha Sheria UDSM, aliwahi kugombea urais kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi na bado ni mjumbe wa Kamati Kuu na mkurugenzi wa sheria wa chama hicho.

Lakini serikali imempa mkataba wa kuendelea kufundisha UDSM. Wapo wanaosema serikali inamuogopa Mvungi kwa kuwa ni mwanasheria; lakini wengine wanasema serikali “inamvutia pumzi” ili isije kutoa nafasi kwake kwenda mahakamani. Ghasia, Waraka unasemaje?

Mbali na hao, kuna wanasiasa na watumishi wengine wa umma wanaoshiriki siasa, japokuwa si kwa kugombea na kuchagua. Wanashiriki vikao vinavyofikia maamuzi na wanatetea sera na siasa za chama kilichoko madarakani.

Chukua mfano wa Mwanasheria Mkuu wa serikali (AG), Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Mkurugenzi Mkuu wa Usalama wa Taifa. Ghasia, Waraka unasemaje?

Kwa kauli ya waziri Ghasia, serikali inathibitisha kwamba haithamini wataalamu wazalendo. Anasema, “Kama Baregu anatamani kuendelea kufundisha akatafute kazi nje ya nchi.”

Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana anasema Profesa Baregu ni nguzo Afrika na duniani na kwamba kutomchukua kutanufaisha wengine. Waziri Ghasia upooo?

Serikali inakataa mzalendo kubaki chuo kikuu; badala yake inaagiza “galasa” kutoka nchi za nje. Tumelaaniwa? Rejea orodha yako ya walioajiriwa serikalini na bado wako katika vyama vya siasa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: