Serikali inateswa na ahadi zake


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 20 June 2012

Printer-friendly version

KATIKA Bajeti ya mwaka 2011/12, Serikali ilitangaza nia yake ya kupunguza makali ya maisha. Hatua mbalimbali zilichukuliwa ikiwamo kupunguza kodi na tozo kwenye mafuta ya dizeli na petroli, kuanza kutekeleza mpango wa dharura wa umeme na kutoa fedha za kununua chakula kwa Wakala wa Chakula.

Serikali ilitumia Sh. 296 bilioni na dola za Marekani 183 milioni kwenye Umeme. Vilevile Serikali ilitumia Sh. 27 bilioni kununua mahindi na kusambaza kwenye masoko.

Hata hivyo, mfumuko wa bei uliongezeka maradufu kutoka wastani wa asilimia 6.3 mwaka 2010/11 mpaka wastani wa asilimia 17.8 mwaka 2011/12. Serikali imefeli katika lengo lake la kupunguza makali ya maisha kwa wananchi.

Siyo tu kwamba Serikali imeshindwa kudhibiti upandaji holela wa gharama za maisha bali pia hatua za Serikali zimeongeza kasi ya kupanda kwa makali ya maisha.

Serikali ilitoa vibali vya kuagiza sukari bila kutoza ushuru wa forodha kiasi cha tani 200,000 ili kukabiliana na uhaba na kupanda kwa bei ya Sukari. Baada ya hatua hii bei ya sukari ilipanda kutoka Sh. 1700 mpaka Sh. 2800 kwenye maeneo mengi nchini.

Hotuba ya Waziri wa Fedha inaonesha serikali imetenga Sh. 1,383 bilioni  kwa ajili ya Usafirishaji na Uchukuzi huku kati ya hizo Wizara ya Ujenzi imechotewa Sh. 1,000 bilioni.

Hii ina maana Wizara ya Uchukuzi yenye reli, bandari, viwanja vya ndege na usafiri wa maziwa ya Tanganyika, Nyasa na Viktoria, imetengewa Sh 383 bilioni.

Kutokana na serikali kutotenga fedha za kutosha katika baadhi ya maeneo muhimu, wakati wa vikao vya kupitia mwelekeo wa bajeti ya 2012/ 2013, makadirio ya wizara kadhaa yalikataliwa na kamati za kudumu za bunge.

Wizara ambazo hazikupitishiwa makadirio ni Elimu na Mafunzo ya Ufundi; Kilimo, Ushirika na Usalama wa Chakula; na Uchukuzi. Pamoja na mazingira haya magumu Waziri wa Uchukuzi Dk. Harrison Mwakyembe alijitapa katika mkutano wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jangwani Dar es Salaam kwamba atafufua reli ya kati.

Katika Bajeti ya mwaka 2011/12 Serikali iliahidi kupunguza misamaha ya kodi mpaka kufikia asilimia 1 ya Pato la Taifa. Ahadi hii haikutekelezwa na Serikali na badala yake imerejea kuahidi tena.

Katika hotuba yake, Waziri wa Fedha amesema serikali itaendelea kufanya mapitio ya sheria mbalimbali zinazotoa misamaha ya kodi kwa lengo la kudhibiti na kupunguza misamaha hiyo. Kwa kauli hiyo, serikali haikupitia misamaha hiyo katika mwaka uliopita wa fedha.

Alipokuwa anafunga Bunge la Bajeti mwaka 2011/ 12, Waziri Mkuu alitangaza kampuni ambazo ni walipa kodi wakubwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Katika orodha ile kulikuwa na kampuni moja tu ya simu za mkononi – AirTel.

Ajabu, wakati wananchi wanataka serikali ikamue zaidi kodi kutoka kampuni za simu, inapendekeza kuongeza kodi kwa mwananchi anayetumia simu hizo. Serikali imekimbilia kukandamiza wanyonge watumiaji wa simu na kuziacha kampuni za simu zikilipa kiduchu kutoka kwenye mapato yao.

Deni la taifa. Serikali inasisitiza kwamba deni la taifa linastahmilika, lakini Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) anaonyesha mashaka makubwa sana kutokana na kasi ya kukua kwa deni hilo.

Taarifa ya CAG inaonyesha  kuwa deni la taifa linazidi kuongezeka kwa asilimia 38 kutoka Sh. 10.5 trilioni mwaka 2009/2010 hadi Sh. 14.4 trilioni mwaka 2010/2011.

Waziri wa Fedha katika hotuba yake wiki iliyopita alisema deni la taifa limefikia Sh. 20.3 trilioni mpaka ilipofika mwezi Machi mwaka 2012. Lakini taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ya Mei 2012 inaonyesha deni la taifa sasa limefikia Sh. 22 trilioni.

Wabunge wameshtuka. Christopher ole Sendeka wa Simanjiro (CCM) anataka iundwe kamati kuuchunguza mfuko wa fedha. Pendekezo la Sendeka linafanana na la kambi ya upinzani bungeni.

Kambi ya upinzani imependekeza Bunge lifanye ukaguzi maalumu kuhusu akaunti ya deni la taifa ili kubaini ukweli kuhusu ustahmilivu wa deni na mikopo ambayo Serikali inachukua. Lengo ni kujua kama mikopo inakwenda kwenye miradi ya maendeleo na kama miradi hiyo ina tija.

Mkanganyiko mwingine uko katika taarifa. Katika sura ya kwanza ya kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2011 Serikali inakiri kwamba kulikuwa na ukuaji mdogo wa pato la taifa.

Serikali ikaamua kumlaumu Mwenyezi Mungu kwa kusababisha ukuaji huo usioridhisha wa pato la taifa kwa kusema, “Kiwango kidogo cha ukuaji kilitokana na hali mbaya ya ukame iliyojitokeza katika sehemu mbalimbali nchini ambapo imeathiri sekta ya kilimo.”

Lakini katika kitabu hicho hicho, kilichoandaliwa na Serikali hiyo hiyo imeandikwa: “Mwaka 2011, uzalishaji wa mazao ya chakula hususan ngano, mihogo, maharage, ndizi na viazi uliongezeka ikilinganishwa na mwaka 2010 kutokana na hali nzuri ya hewa na mtawanyiko mzuri wa mvua kwa ustawi wa mazao.” Mkanganyiko huu ni dalili ya ukosefu wa umakini katika kuandaa taarifa muhimu za Serikali na unaitia Serikali katika aibu kubwa.

0753 626 751
0
No votes yet