Serikali itoe majibu sasa
BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilianza mkutano wake jana mjini Dodoma huku Watanzania wakiwa na mashaka juu ya hatima ya mambo muhimu ambayo serikali haijapatia majibu.
Lipo suala la hatima ya viongozi waandamizi serikalini waliohusika na mkataba wa kifisadi wa Richmond na kama ilivyothibitishwa na Kamati ya Bunge.
Lipo tatizo la usiri kuhusiana na kampuni ya Kagoda Agriculture Limited iliyoiba zaidi ya Sh. 40 bilioni kutoka Akaunti ya Madeni ya Nje, Benki Kuu.
Kuna kampuni ya RITES ya India ambayo imedhihirika kushindwa kuendesha Kampuni ya Reli Tanzania, TRL.
Miliki ya mgodi wa Kiwira ulioko Mbeya, inayohusishwa na viongozi wa juu serikalini na utata wa mkataba wa kampuni ya kupakia na kupakua makontena, TICTS.
Kuna uzembe wa kifisadi katika shirika la ndege nchini (ATCL) uliosababisha lifilisike na kufungiwa hadi serikali kulazimika kulipa Sh. 4.7 bilioni ili lianze upya.
Haya ni baadhi tu ya mambo yaliyoitia aibu kubwa serikali na taifa. Yalionyesha jinsi baadhi ya watendaji walivyotumia vibaya nafasi zao na hatimaye kuhujumu taifa.
Hujuma hii imegharimu maisha. Imesababisha mamilioni ya wananchi kukosa kazi, elimu, afya bora na huduma nyingine muhimu za kijamii.
Mabilioni ya shilingi yaliyopotea yangetumika pia kuwekeza katika miundo mbinu anuai. Yamepokonywa tu.
Serikali ina deni kubwa katika yote haya. Lakini ni vema kwamba sasa inawafahamu waliotenda hujuma. Imetoa ahadi bungeni, za kuchukulia hatua wote waliobainika kushiriki hujuma hizi.
Bali hadi mkutano huu wa bunge, haijatekeleza ahadi zake na haionekani kufanya hivyo hivi karibuni.
Sasa tunasema, utamaduni huu wa serikali kulegeza mikono na miguu, haufai wala hauisaidii kwa namna yoyote ile. Unailegeza zaidi na kuidhalilisha.
Tunataka serikali inayosimamia kauli na ahadi zake. Wananchi wataheshimu serikali inayotenda na isiyoweka mbelekoni wale ambao tayari wamebainika kuwa wahujumu uchumi.
Katika hili wananchi hawatakubaliana na serikali itakayowaeleza kwa mafumbo, mambo ambayo wanajua yalistahili kufanywa waziwazi na kwa kila mmoja kuona. Wana haki ya kuona na kujua.
Bunge ndio msimamizi wa serikali. Hapa ndipo tunahimiza wabunge, tena wote, bila kujali wanatoka chama kipi, kuwa imara katika usimamizi wa serikali na kuifanya iwajibike ipasavyo.
Tungependa mkutano wa sasa wa bunge usimalizike bila serikali kutoa majibu kwa hoja kuu tulizonukuu hapo juu na nyingine kama wabunge watakavyoona.