Serikali yaijia juu MwanaHALISI


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 16 September 2008

Printer-friendly versionSend to friend

OFISI ya Msajili wa Magazeti katika Idara ya Habari (MAELEZO) imeikomalia MwanaHALISI kwa kuandika kichwa cha habari kisemacho, “Kikwete alidanganya.”

Katika mahojiano ya takribani saa moja na mhariri wa MwanaHALISI, Jabir Idrissa katika ofisi za Maelezo, Mtaa wa Samora jijini Dar es Salaam, juzi Jumatatu, jopo la maofisa watatu wa serikali lilitaka gazeti liombe radhi kwa kuandika kichwa hicho cha habari.

“Rais alisema yale aliyopata kutoka kwenye ripoti alizopelekewa. Asingeweza kutegemea ripoti moja. Angalau mngesema rais alidanganywa, hapo ingeeleweka,” alieleza kiongozi wa jopo la maofisa hao Habib Nyundo.

Nyundo alieleza kwamba gazeti “limemvua rais heshima” mbele ya wananchi ambao walimchagua kwa zaidi ya asilimia 80.

“Hawa (asilimia 80) mnawaweka kundi gani? Na kwa sasa, kutokana na mambo makubwa aliyokwishafanya rais, idadi itakuwa imepanda. Kwa hiyo ni vizuri mkarekebishe ili kuondoa mwelekeo mbaya,” alisema Nyundo.

Maofisa wengine wa maelezo waliohudhuria mahojiano ni wanahabari Raphael Hokororo na Jovina Bujuru.

Kila utetezi uliowasilishwa na mhariri ulikataliwa na jopo, ikiwa ni pamoja na hoja kwamba kinachotofautisha pande mbili ni “ni suala la mtizamo tu bali mantiki ni ileile iliyokusudiwa.”

Mhariri alipoomba maofisa wamwandikie jinsi ambavyo wangependa taarifa irekebishwe, walikataa katakata na kushurutisha kuwa gazeti liandike, “Rais hakudanganya.”

Toleo la MwanaHALISI la Septemba 10 – 16 liliandika kichwa cha habari “Rais alidanganya” juu ya taarifa za kina juu ya uchotaji wa mabilioni ya shilingi kutoka Benki Kuu (BoT) uliofanywa na kampuni ya Kagoda Agriculture Limited.

Taarifa hiyo ilisema rais hakuwa na sababu ya kuunda Timu kuchunguza wezi wa EPA kwa kuwa tayari alikuwa na taarifa za kipi kilitokea, wapi, lini, kiasi gani kinahusika, nani walihusika katika wizi na maofisa wa BoT waliowezesha ukwapuaji.

MwanaHALISI linaheshimu maoni tofauti ya wananchi, maofisa wa Maelezo na serikali kwa ujumla. Tutaendelea kufanya hivyo.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: