Shamsi Vuai Nahodha: Sina mamalamiko


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 21 July 2010

Printer-friendly versionSend to friend
Gumzo
Apigia debe serikali ya umoja wa kitaifa
Ampamba Rais Aman Abeid Karume

WAZIRI Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Shamsi Vuai Nahodha alitaka kugombea urais Visiwani. Hakufanikiwa.

Katika mahojiano rasmi, ya kwanza na ya aina yake na chombo cha habari tangu atoke kwenye vikao vya chama chake Dodoma, anamweleza SAED KUBENEA, “Sina malalamiko.” Mahojiano hayo yalifanyika ofisini kwake, Vuga, Unguja, Ijumaa 16 Julai 2010.

Swali: Pole kwa hekaheka za kutafuta kugombea urais Zanzibar. Lakini hilo limepita. Unajisikia vipi kwa kukosa ulichotaka?

Jibu: Ni vizuri kwa maana chama kilitangaza hizo nafasi na nilifanya hivyo nikielewa kwamba kuna kupata na kukosa. Mimi nabaki na imani kwamba anayepanga jambo fulani lifanyike ni Mwenyezi Mungu. Sisi wanadamu kwa kawaida tunatamani mambo mengi, lakini mwisho yeye ndiyo huamua.

Swali: Kuna madai kuwa hukujiandaa vya kutosha na hukuwa na mtandao mkubwa na imara. Kwa nini hukujiandaa na kwa nini hukuweka mtandao Visiwani hadi Bara?

Jibu: Hizo ni hoja tu za kutaka kuhalalisha matokeo ya mambo yanavyokuja na kutoka, maana hakuna anayeweza kukwambia ujiandae miaka ishirini, thelathini au mingapi hasa? Ila muda kwangu muhimu.

Unaweza kuwa na watu makini wawili, watatu, waliojiandaa vizuri. Mimi nadhani nilijiandaa vya kutosha.

Tokea nilipoteuliwa Novemba 2000; pamoja na kwamba sikusema au sikuwa na nia ya kugombea, lakini kama mtendaji mkuu wa serikali nilifanya kazi zangu kikamilifu na zilionekana. Hayo ni maandalizi makubwa.

Labda niseme, wakati haujafika; ukifika hiyo mitandao tunayoijua na tusiyoijua, itakuwa inajiunda yenyewe wala haihitaji kuundwa na mimi.

Swali: Au uamuzi ulikuwa tayari umechukuliwa na viongozi wenu wa ngazi ya juu – Bara na Visiwani?
 
Jibu: Hayo ni madai ambayo nayaona kama ya kujifurahisha. Una uhakika gani kwamba huyu mtu unayemfanyia mipango ya awali ataendelea kuwa na afya njema na uhai? Hakika Mwenyezi Mungu anauchukua uhai kwa dakika kumi tu…

Hayo yote ni mipango ya Mungu. Ni jambo ambalo si kweli, kwamba limepangwa toka mwanzo. Hapana! Hili limetokea kwenye mchakato; watu wanafanya maamuzi, tena wanavyohisi kuliko sisi tunavyosema.

Swali: Kwa nafasi kama hizi, hivi siyo lazima kwanza kujadiliana miongoni mwenu – uongozi wa juu – ili kuepusha misuguano na kuumbuana?

Jibu: Hapana. Watu wanakuangalia na wanafanya maamuzi kama wanavyotaka. Huwezi kumlaumu au kumlazimisha. Wako watu wanaotafuta uongozi wanaangalia vitu fulani. Sasa hatujui katika mazingira hayo walitumia vigezo gani.

Swali: Nipe maoni yako: Umeridhika jinsi mchakato wa uteuzi wa mgombea urais Zanzibar ulivyoendeshwa?

Jibu: Ndiyo nimeridhika. Hakuna dosari yoyote. Kila mmoja alipata fursa ya kujieleza na sote tulipata fursa sawa.

Waliotaka kuvitumia vyombo vya habari kwa kadri walivyoweza, waliruhusiwa kufanya hivyo. Kwa jumla mchakato ulikwenda vizuri, tena vizuri sana.

Swali: Unapendekeza marekebisho yapi katika utaratibu wa sasa wa uteuzi?

Jibu: Kwa maoni yangu, hakuna ambacho kimekwenda vibaya. Hivyo, sijaona mahali popote pakubwa ambapo panahitaji marekebisho kwa hali ya sasa.

Utaratibu wa kuendesha uchaguzi umevuka hata kiwango kile cha makadirio yangu. Kwa hiyo nadhani umeendeshwa kwa asilimia mia kwa jambo hilo.

Swali: Una malalamiko yapi juu ya mchakato ulivyoendeshwa?

Jibu: Sina malalamiko. Nimeridhika na kila kitu.

Swali: Kuna taarifa kwamba baada ya wewe kubaki – miongoni mwa viongozi watatu waliokuwa wanawania kugombea urais – umeahidiwa kitu. Nani amekuahidi na ni kitu gani hicho ulichoahidiwa?

Jibu: Hapana mimi hilo sijalisikia, lakini kama watu wanakaa na kumfikiria mwenzao, pengine ni kutokana na mchango wake na kutambua uwezo wake.

Hilo ni jambo jema ambalo hata kama lisipotokea, lakini vile watu kukaa na kuwaza jambo kubwa namna hiyo, ina maana kwamba wanatambua kwamba wewe unaweza kufanya kazi hiyo.

Sasa mimi nasema, likitokea nitamshukuru Mungu; lakini hata lisipotokea, kwa ile tu kufikiriwa, inaniongezea umri na uhai.

Swali: Kuna maelezo kuwa wewe ndiye mwenye uwezo wa kusimamia utendaji wa serikali katika mazingira ya vyama viwili ikulu. Ni kweli?

Jibu: Nimepata bahati kubwa sana. Nimekutana na watu wenye fikra na maoni tofauti hata kabla sijaingia katika ulingo huu wa siasa. Lakini baadaye nilipokuwa mtu mzima mafunzo yangu yaliendelea kuwa yaleyale niliyokulia; nilibahatika kuwafahamu watu wenye fikra tofauti.

Nilijiunga na chuo cha elimu ya juu ya Diplomasia, nayo ilinipa mafunzo ya aina yake namna ya kukutana kwenye vikao tofauti na jinsi ya kupunguza migogoro.

Yote yalikuwa ni maandalizi kwa hiyo nilipoingia kwenye uongozi nikajikuta nina utaalamu wa kutosha ambao umenisaidia sana katika kujenga mahusiano na watu mbalimbali hata watu wasionipenda na tunaotofautiana kimawazo.

Sasa kama watu wanasema kwamba nina uwezo wa kufanya hivyo, inawezekana ni kwa sababu hizo nilizozieleza. Halafu nina tabia nyingine ambayo inawezekana wao hawana.

Mimi ni mwepesi wa kusahau; sina visasi. Napenda kuwaunganisha watu; ni mwanafunzi mzuri ninayapenda kujifunza haraka.

Na jingine ambalo watu wengi hawana, siwezi kuikana kweli kwa kuchelea upweke wa kitambo… maana kuna watu wengine unapotokea ukweli wanashindwa kusema ukweli kwa sababu ya kuogopa tu watu wengine watawalaumu.

Mimi niko tayari kwa jambo la msingi, na la ukweli. Sasa ukizikusanyisha hizo zote zinakupa jibu kama hivi ndivyo nilivyo.

 Swali: Je, kuna uwezekano wa MRADI wa kura za maoni inayotaka kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa kufanikiwa? Wewe una nafasi gani katika kuukamilisha?

Jibu: Jambo la msingi kwanza tujiulize, kwa nini wananchi waulizwe kama wanapenda mfumo huo.

Tumekuwa tukiangalia hali ya siasa ya Zanzibar kupitia nchi zilizofanikiwa sana kustawisha uchumi wake na kuleta maendeleo kwa wananchi wake. Kote huko kunaonyesha kwamba maendeleo hayo yamepatikana kutokana na kusimamia umoja.

Tunayo dhamana kubwa ya kuhakikisha tunawapa wananchi maendeleo wanayoyahitaji. Hilo ni swala ambalo halina uchaguzi; kila mwana-CCM ana wajibu huo.

Mimi nina matumaini kwamba kila mwananchi ambaye anaitakia mema Zanzibar atakuwa tayari kufanya maamuzi ambayo yatasaidia katika kujenga umoja. Hatuwezi kuleta maendeleo iwapo watu hawawezi kushirikiana katika shughuli za maendeleo.

Hivi vyama ni (kwa ajili ya) utaratibu; bado sote ni raia wa nchi moja. Hivyo tunao wajibu wa kuleta maendeleo katika nchi yetu. 

Kama kuna jambo lolote linaloweza kutusaidia kuwafanya Wazanzibari kuwa wamoja, wakasahau yaliyopita, ni hili (la serikali ya umojawa kitaifa).

Kwa maana hiyo basi, mimi natarajia kura hiyo itapita. Ni matumaini yangu kwamba watu wanaopenda maendeleo ya Zanzibar na wanaoitakia Zanzibar na watoto wetu mema, wataunga mkono uamuzi wowote ambao utaleta umoja na maendeleo.

Kwa hiyo labda nikae nikiwa na matumaini, ingawa siwezi kutabiri litakalotokea.

Swali: Kuna madai kuwa Rais Amani Abeid Karume hakumtaka Dk. Mohammed Gharib Bilal katika kiti cha urais visiwani na hata katika nafasi ya sasa ya mgombea mwenza wa rais Jakaya Kikwete?

Jibu: Mimi siwezi kuthibitisha hili. Sijawahi kumsikia Rais Karume kwa kipindi chote cha miaka 10, kwa tafsiri yake au kwa kauli ya mdomo, akisema jambo hilo. Hivyo siwezi kulithibitisha na wala sidhani kama lipo maana sijalisikia hata harufu yake.

Swali: Una hofu yoyote juu ya utawala wa serikali ya umoja wa kitaifa? Ni hofu ipi?

Jibu: Mimi sina hofu… Serikali ya umoja wa kitaifa, kama italeta tija kwa maana ya kustawisha maendeleo ya wananchi, hilo sina tatizo nalo.

Naamini kwamba iwapo suala hili la serikali ya umoja wa kitaifa litapita, serikali itakayoundwa itakuwa makini. Kila kiongozi atakayekuwa serikalini au katika vyama vyetu, atatanguliza uzalendo mbele.

Hivyo serikali itakayokuja, itakuwa serikali makini na yenye uwezo wa kusimamia nchi yetu; kwa sababu kila mmoja ana kipaji ambacho mwingine hana.

Kwa hiyo, unapokuwa na watu wa vyama viwili au vitatu kwenye serikali, kila mmoja anakuja na kipawa chake; anakuja na sera zake na anakuja na falsafa yake. Mkikusanya (yote hayo) pamoja mnakuwa na kitu kikubwa na kizuri. Kikubwa kinachotakiwa ni kutanguliza mbele maslahi ya watu wetu; kule kuwa tayari kuwatumikia wananchi.

Ninavyofahamu Dk. Ali Mohammed Shein ni kati ya watu makini, wenye ujuzi. Iwapo wananchi watampa ridhaa ya kuingia madarakani, basi haya atayatekeleza bila matatizo.

Huyu bwana (Dk. Shein) namfahamu sana, tulipoingia serikalini mwaka 2000 mimi nilikuwa bosi wake. Wakati huo, yeye alikuwa Waziri wa Nchi, Katiba na Utawala Bora, mimi nikiwa waziri kiongozi.

Lakini baadaye aliendelea kuwa makamu wa rais, mimi nikaendelea kuwa mtendaji wa shuguli za serikali. Tumekuwa tukikutana na tukifanya kazi kwa ukaribu mkubwa.

Kwa hiyo yeye namfahamu, naifahamu dira yake, naifahamu falsafa yake. Ndiyo maana nasema, iwapo atachaguliwa ataunda serikali itakayoipeleka nchi mahali pazuri zaidi. Hataunda serikali itakayoturudisha nyuma.

Swali: Kuna madai kuwa Zanzibar hakuna uhuru wa kutoa maoni na kumeshamiri vitisho. Hili limekua hasa baada ya serikali kufuta gazeti la DIRA. Una maoni gani kuhusu hili?

Jibu: Kila jambo lina faida na hasara yake. Maana katika nchi kuna maswala yanayovuruga umoja na mshikamano wa taifa; jambo linalovuruga umoja na maelewano lazima lipewe uzito unaostahili.

Gazeti hili (DIRA), hata uandishi wake ulikuwa unakwenda kinyume na misingi yetu. Badala ya kuleta umoja lilikuwa linachochea uhasama. Lakini hata misingi ya kulifungia ilifuata taratibu.

Serikali ilipeleka shauri Baraza la Habari Tanzania (MCT) kutafuta suluhu kwa kuelemisha wahusika namna bora ya kuendesha gazeti lao; lakini hakuna suluhu iliyopatikana.

Baadaye, sisi kama serikali, tukachukua uamuzi wa kulifuta. Lakini bado tukasema nchi yetu inafuata misingi ya demokrasia; hivyo wahusika wanaweza kupeleka suala lao mahakamani kutafuta haki.

Hawakufanya hivyo. Nadhani ni kwa sababu waliona hawana haja ya kuendelea na shauri lao. Sijui kwa nini (hawakuchukua hatua), maana bado siwezi kuwasemea. Lakini nadhani pengine waliona mazingira yenyewe yana ukweli.

Katika mazingira hayo, huwezi kusema Zanzibar hakuna uhuru kwa vyombo vya habari au uhuru wa kutoa maoni. Hapana. Uhuru upo, tena mkubwa sana. Sisi ni wapendwa wa waandishi wa habari na vyombo vyao; ndiyo maana leo unaona gazeti lako linafanya mahojiano na mmoja wa viongozi wakuu katika serikali.

Swali: Sema kidogo juu ya utawala wa Rais Karume unaoingia ukingoni. Je, umefurahia kufanya kazi naye?

Jibu: Ndiyo nimefurahi, tena sana. Tumefanya kazi yenye mafanikio makubwa. Sisemi tumefanikiwa kumaliza matatizo yote ya wananchi katika kipindi chetu cha uongozi, lakini tumefanikiwa.

Maana hakuna mwenye uwezo wa kuondoa matatizo yote katika nchi kwa wakati mmoja. Hapa tumekuta matatizo mengi.

Tumekuta mishahara serikalini shida, viinua mgongo havipatikani kwa wakati, wanaotoa huduma ndani ya serikali na taasisi zake hawalipwi ujira wao; ili mradi matatizo juu ya matatizo.

Serikali ya Rais Karume ilipoingia madarakani, ikaja na vipaumbele vyake. Ikavitekeleza. Hivi sasa, mengi kati ya hayo, yamekuwa historia. Tulitekeleza wajibu wetu, lakini kwa jumla tumefanya (pamoja) kazi nzuri.

Swali: Je, kuna wakati mlisigana? Katika yapi?

Jibu: Sikumbuki. Kwa kuwa hatukuona jambo baya likitokea kwenye jamii, tunaweza kusema halikujitokeza (la kusigana). Lingejitokeza kila mmoja angeliona; maana urafiki unapotokezewa na uadui, kila mmoja atajua.

Swali: Kuna wakati mlikwaruzana? Katika yapi?

Jibu: Nasema hakuna. Nimefanya kazi na Rais Karume kwa ushirikiano mkubwa. Nilikuwa msaidizi wake mahiri. Nilimpenda na yeye alinipenda.

Swali: Ulimpenda Rais Karume kwa kitu gani?

Jibu: Mimi labda jambo ambalo nilipenda, kwa maneno machache sana, ni hili. Wanadamu katika jamii wako wa aina mbili. Wako wanaosema wasiyoyatenda, lakini wapo wanaotenda wanayoyasema.

Rais Karume yuko katika kundi la pili. Anatenda yale anayoyasema. Si msemaji sana. Yeye anatumia maneno machache sana kujieleza, lakini vitendo ni vingi.

Jambo hilo ni zuri sana kwa kiongozi. Kiongozi anatakiwa kuwa mtu wa vitendo, si maneno. Hakuachana sana na marehemu baba yake, Mzee Abeid Amani Karume na sishangai sana kwa sababu ndiye baba yake.

Swali:  Ulimchukia kwa lipi?

Jibu: Nikiwa mkweli wa dhati, sina hata moja ambalo limefanya nimchukie.

Swali: Kama ungeteuliwa kugombea urais Zanzibar na ukagombea na kushinda; ni kitu gani hasa unaona ungeshughulikia kwanza?

Jibu: Nilitaka kujenga msingi mkubwa katika elimu. Naamini kuwa Zanzibar inaweza kuwa kituo kikuu cha mawasiliano na kompyuta. Badala watu kwenda Kenya au Uganda kujifunza, Mungu awezeshe waje Zanzibar.

Nilitaka vijana wetu lazima wawe na ujuzi na maarifa ya hali ya juu sana, na nafikiria Zanzibar siku moja iwe ni kituo mahsusi cha elimu hapa Afrika Mashariki.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: