Sheria pekee haitoshi kuokoa NSSF, PPF


Alloyce Komba's picture

Na Alloyce Komba - Imechapwa 02 June 2009

Printer-friendly version

WATAALAMU wa masuala ya mifuko ya hifadhi ya jamii na wanasheria kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) hivi sasa wanaandaa kanuni na taasisi zitakazoongoza utumiaji wa Sheria ya Mamlaka ya Mifuko ya Jamii ya Mwaka 2008.
 
Lengo la kuunda mamlaka ya mifuko ya jamii, kwa mujibu wa Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkullo, ni kudhibiti matumizi ya fedha za mifuko hiyo. Mifuko hiyo hupata fedha kutoka kwa wafanyakazi wa mashirika, serikali na makampuni binafsi kwa michango ya kujiwekea akiba ya uzeeni.
 
Kwa mujibu wa muswada huo, mamlaka itahakikisha mifuko hiyo inaendeshwa kwa ufanisi ili kuwanufaisha zaidi wanachama wake.
 
Sheria hiyo inaunda pia Mahakama ya Hifadhi ya Jamii ili kushughulikia migogoro yoyote itakayojitokeza. Mahakama hiyo itakauwa chini ya Jaji wa Mahakama Kuu.
 
Mahakama hii itakuwa ikipitia maamuzi yoyote yenye utata au mgogoro ya Mamlaka ya Mifuko ya Jamii. Itakuwa pia na uwezo wa kusikiliza rufaa za masuala ya hifadhi ya jamii kutoka katika mamlaka.
 
Mamlaka ya Hifadhi ya Mifuko ya Jamii inaundwa wakati kuna tuhuma kadhaa za ufisadi katika mifuko ya hifadhi ya jamii nchini, inayoyahusisha mashirika ya umma na hata serikali za mitaa kama vile NSSF, PPF na LAPF. Hata Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali CAG, amethibitisha kuwepo ufisadi huo.
 
Ndiyo maana sheria ya udhibiti wa fedha za mifuko hiyo zinazokatwa katika mishahara ya wanachama wake, imehakikisha mameneja au wakurugenzi hawatakuwa na uamuzi pekee yao juu ya uwekezaji kama ilivyozoeleka. Benki Kuu na Bodi ya Mamlaka ya Mifuko zitatoa vigezo vya uwekezaji pale inapobidi kufanya hivyo.
 
Taarifa ya CAG imebainisha kuwa, kwa mfano, Mamlaka ya Mfuko wa Hifadhi ya Serikali za Mitaa (LAPF) iliikopesha GK Hotels & Resorts dola 535, 000 katika mwaka wa fedha wa 2003|04, ambapo kufikia Juni 30, 2008 deni lilifikia kiasi cha dola 722, 000 wakati kampuni husika ilikuwa inadaiwa pia kodi ya kupanga katika jingo la LAPF dola milioni 1.127.
 
Imeonyesha matumizi ya fedha yasiyofaa kwa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) ambayo imekuwa ikitumia fedha za wanachama wa mfuko huo kuwalipa wafanyakazi wake bonasi eti kwa kazi nzuri wanayofanya wakati huo ni wajibu wao kwa mujibu wa ajira zao.
 
NSSF nayo imehusika katika kutoa mikopo na hata misaada ya fedha kwa watu na makampuni binafsi wakiwemo vigogo ndani ya serikali bila utaratibu wowote kwa vile hakuna sheria iliyokuwa inazuia maamuzi hayo.
 
Sheria inasema Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Mifuko hiyo itakuwa na Mwenyekiti atakayeteuliwa na rais na wajumbe wafuatao: Msajili wa Hazina, Kamishna wa Kazi, Wawakilishi wawili wa Chama cha Waajiri, Wawakilishi wawili wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi, mtaalam mmoja wa masuala ya hifadhi ya jamii na Mkurugenzi Mkuu ambaye hana kura.
 
Bodi itateua pia mwanasheria mwenye uzoefu wa sio chini ya miaka miwili ili awe Mwanasheria wa Mamlaka na Katibu. Shughuli za Mamlaka kisheria ni pamoja na kuandikisha wasimamizi au mameneja wote wa mifuko, kutembelea na kukagua mara kwa mara utendaji kazi wa mifuko hiyo ikiwemo vitabu vya mahesabu.
 
Ukiisoma sheria hiyo kwa makini pamoja na vyombo vitakavyouunda kusimamia utekelezaji wa majukumu yake, utaona ni nzuri sana kama ambavyo tunazo sheria nyingi za namna hiyo. Hii imekuwa ni mtazamo tulionao kwamba sheria yaweza kuweka mambo sawa pale yanapokwama bila kukumbuka kwamba sheria hiyo hutumika endapo waliopewa mamlaka ya kuitumia wataitekeleza.
 
Mfano ni ile Sheria ya Rushwa ya Mwaka 2007 ambayo ina vifungu vya sheria vya kudhibiti masuala mengi ya rushwa ikiwemo hata rushwa ya ngono ambayo uchunguzi na ushahidi wake huwa ni mgumu sana . Hata hivyo sheria hiyo inayompa madaraka makubwa Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, inategemea na utashi wa wanaoitumia. Wanaweza kuamua isitumike ipasavyo kwa manufaa yao au ya mtu mwingine yeyote. Yaani sheria yaweza kutumika kifisadi.
 
Hata mashitaka yakipelekwa mahakamani, ikiwemo ushahidi wa kutosha kutolewa, uamuzi wa kumtia hatiani mshitakiwa kwa ushahidi huo ni wa mahakama ambayo ndiyo yenye mamlaka pekee ya kutafsiri sheria. Inaweza kutafsiri sheria vinginevyo kwa manufaa ya mshitakiwa! Hivyo, ili sheria ifanye kazi nzuri, kunahitajika utashi wa maadili kwa wasimamiaji wa sheria hiyo.
 
Ni maoni yangu kwamba ufisadi unatokana na mmomonyoko wa maadili katika jamii yetu katika maeneo yote ya kikazi. Nimewahi kueleza katika gazeti hili kwamba kila sekta nchini imekumbwa na mmomonyoko wa maadili.
 
Hata kwenye masuala ya dini kuna matatizo kiasi cha kushangaza kama tulivyoona kwenye upatu wa DECI unaoendelea kuliza watu wengi.
 
  Kwanza , kuundwa kwa mamlaka ya kudhibiti mifuko ya hifadhi ya jamii ni kuongeza urasimu wa kusimamia masuala hayo ambapo wahusika wanaweza nao kuhongwa kwa kupewa mikopo na mifuko husika kama ambavyo imewahi kutokea ambapo Waziri Mkuu na hata Rais waliwahi kunufaika kinyemela na fedha za mifuko hiyo, ingawa baada ya kushtukiwa wakarejesha chap chap.
 
Pili, watakaoongoza mamlaka hiyo watakuwa wamepimwa vipi kimaadili kwani kama ambavyo imezoeleka ni dhahiri watakuwa ni watanzania tunaowajua tena wengi wao ni wale waliowahi kuvurunda katika maeneo mengine ingawa wa sifa nzuri za kitaaluma.
 
Nashauri watakasimamia uendeshaji wa mamlaka hiyo wapewe mafunzo kuhusu maadili na hata kupelekwa katika mafunzo zaidi nje ya nchi ili kuondokana na tabia ya kufanya kazi kwa mazoea.
 
Maana sheria haiwezi kuleta mabadiliko yoyote ya udhibiti wa ufisadi unaofanywa na mifuko ya hifadhi ya jamii. Tunahitaji watendaji wenye maadili mema. Wasioweza kushawishiwa kupinda sheria kwa manufaa yao .
 

0
No votes yet