Si kashfa ya Sophia Simba pekee...

- Ni kielelezo cha uoza wa serikali nzima
SERIKALI imeangukia pua bungeni. Ni Jumamosi iliyopita baada ya Bunge kuukataa muswada wa sheria ya usalama wa taifa ya mwaka 2009 baada ya kubainisha mapungufu mengi ambayo ni ya ukiukaji wa katiba.
Muswada uliwasilishwa bungeni na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utawala Bora, Sophia Simba. Ulilenga kundwa baraza la usalama wa taifa lenye wajumbe 20.
Watoa hoja wengi bungeni walionyesha dhahiri muswada huo ulikuwa unaingilia madaraka ya rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania ambao yameanishwa kwenye katiba ya nchi.
Wabunge kwa kutambua udhaifu wa muswada huo waliukataa kwa kauli moja hivyo kuifanya serikali kurudi mikono mitupu kotoka bungeni. Iliarifiwa kwamba hii ni mara ya pili kwa muswada huo kukataliwa na wabunge.
Kwa sura ya haraka haraka watu wanaweza kufikiri kwamba aliyeshindwa bungeni ni waziri Sophia, na wanaweza kumbebesha kila aina ya lawama. Lakini tafakari ya kina inaonyesha kwamba kilichotokea bungeni ni mwendelezo wa malalamiko ya wananchi juu ya mwenendo wa serikali ya kwa muda mrefu sasa.
Kiutaratibu, hakuna hata waziri mmoja mwenye ubavu wa kuandaa muswada wa sheria na kuuwasilisha bungeni bila kufuata mchakato uliokubalika serikalini. Kwa maana hiyo, kila muswada huanza na wizara husika kwa maana ya huu wa usalama wa taifa utakuwa umeanzia ofisi ya Simba, lakini ilipokea mapendekezo kutoka kwa vyombo vyote vya kiusalama vilivyo chini ya ofisi hiyo.
Hivyo, Sophia atakuwa amepokea mawazo kutoka Idara ya Usalama wa Taifa, Polisi, Jeshini na mawazo haya ni lazima mtiririko wake ujadiliwe kwa mapana yake na wadau wote. Hatua inayofuata ni kuandaliwa kwa waraka wa makatibu wakuu ambao huwasilishwa kwenye Baraza la Mawaziri ili kupata baraka za chombo hicho cha juu katika maamuzi ya kuendesha nchi.
Hakuna muswada unaokwenda kokote bila kikao hicho kuamua. Lakini la muhimu zaidi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ni lazima ishirikishwe tangu mwanzo ili kuhakikisha kwamba hakuna pengo lolote la kisheria linalojitokeza katika utayarishaji wa muswada husika kisha kuufikisha ngazi zote.
Kwa kifupi muswada wowote wa serikali unaowasilishwa bungeni ni matokeo ya kazi ya serikali kwa ujumla wake. Kwa hali hii kuanzia juu, yaani Rais kama mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri; mawaziri wake wote, mwanasheria mkuu, wataalam wa kutoka ofisi ya mwanasheria mkuu.
Kote huko utaalam na weledi wa kisheria unazingatiwa ili sheria itakayopelekwa bungeni isiwe inapingana na sheria nyingine za nchi, achilia mbali kukiuka katiba. Sasa kama huu ndio utaratibu, inakuwaje upungufu wa kiwango hiki ukajitokeza kwenye muswada wa Simba?
Kuna mambo mengi yanayoweza kuelezwa kama kiini cha udhaifu wote huu; kwamba ni uwezo mdogo wa wote waliohusika na mchakato? Kwamba kuna watu wana nia ovu ya kutaka kupunguza madaraka ya rais? Kwamba inawezekana madaraka makubwa yamemkifu na hivyo anatafuta njia ya kuyapunguza?
Binafsi sina jibu. Lakini naweza tu kuchambua kuwa kinachotokea kwenye miswada hakiwezi kutofautiana na kile kinachotokea kwenye mikataba yetu.
Si bahati mbaya leo hii kila mkataba tunaoingia kama taifa na hakuna mkataba wowote mkubwa ambao serikali imeingia katika miaka 15 iliyopita.
Huo ndio mwendo wa wataalam wetu, na sasa umekuwa mwendo wa watawala kwa ujumla wao, mawaziri na hata baraza la mawaziri, na kwa kweli ni uchochoro ambao umelitumbukiza taifa hili katika maafa makubwa ambayo kila siku tunashindwa kujinasua.
Hivi inawezekana vipi Rais akubali madaraka yake ya kikatiba yaguswe kirahisi namna hii kama umakini ulitawala katika kuandaa muswada wa usalama wa taifa? Na tusema mtu kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali kiongozi ambaye amekwisha kushika wadhifa wa ujaji anashindwa vipi kuona pengo kubwa namna hiyo la lisheria katika muswada husika?
Kikubwa zaidi hivi vyombo vyote vya usalama havikuona kwamba suala zima la usalama linalotakiwa kujitenga kabisa na siasa linatumbukizwa kwenye siasa tena kwa kasi kubwa? Je, wataalam wetu wa usalama waliacha wapi weledi wao kiasi cha kushindwa kumwambia Amiri Jeshi Mkuu kwamba sheria hii inavunja nguvu za amiri jeshi mkuu?
Sijui kama nina majibu ya maswali yote haya, lakini itoshe tu kusema kwamba Sophia Simba amesaidi taifa kufumbua macho na sasa litambue kwamba matatizo yetu ni makubwa kuliko tunavyoweza kufikiri.
Nakumbuka wakati wa utawala wa rais Benjamin Mkapa, mambo mawili juu ya umakini wa watawala wetu yalipata kutokea kuhusu uandishi wa taarifa, mikataba au makubaliano; Mkapa alikuwa amewataka wakuu wote wa mikoa wawasilishe kwake ripoti ya maendeleo ya mikoa yao, aliwataka kila mmoja awasilishe baada ya kuisoma ili iwe ni ripoti kweli ya mkuu wa mkoa na si ya wasaidizi wake. Wote waliwasilisha, lakini wote pia hawakuzisoma.
Walizisukuma kwa mkuu wa bila kuzisoma na bila soni. Katika kipindi hicho hicho Tanzania iliwasilisha ripoti yake juu ya mkataba wa Marekani na nchi za Afrika wa kuuza bidhaa kwenye soko la taifa hilo - AGOA. Lakini unajua nini kilitokea? Nyaraka za Tanzania hazikusomwa.
Zilisukumwa hivyo hivyo, yaani kwa uharaka, uzembe na kutokujali kwa hali ya juu kwetu, hata jina la nchi yetu lilikosewa. Yaani badala ya kusema hii ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nyaraka zilisomeka Jamhuri ya Tanzania.
Tulivuna aibu ya kutosha kwani Wamarekani walirejesha nyaraka zile na kutukumbusha pamoja na mambo mengine nchi yetu si Jamhuri ya Tanzania bali Jamhuri ya Muungano wa Tanzania .
Ukiniuliza leo hii kuhusu muswada uliomwangusha Sophia nitakuambia kwamba ni kweli ulipitia mchakato mzima wa kisheria serikalini katika kutunga sheria, lakini nitakuhakikisha kwamba wote waliokaa kwenye vikao vya kuujadili macho na akili zao hazikuwa kwenye muswada ila kwenye ‘bahasha’ wanazolipana.
Watu wetu wameamua kuwa watendakazi wa bahasha- posho- kuliko wawajibikaji wa majukumu yao . Wanakaa kama askari wa kukodiwa, hawana umakini wowote, hawaguswi na weledi tena katika kutenda, ila katika ukubwa na idadi ya bahasha, matokeo yake ni kama haya yaliyomkumba Simba.
Mimi sitashangaa kama siku moja tutasikia kwamba watawala wetu walisaini mkataba wa kuuza nchi bila kujua wakidhani wanasaini mkataba wa msaada kutoka nje.