Siasa za mapanga zinapeleka nchi kubaya


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 04 April 2012

Printer-friendly version

ALIPOTEMBELEA Ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam baada ya kuwa umelipuliwa kwa mabomu na magaidi wa Al Qaeda Agosti 1998, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Madeleine Albright alisema, “Hii si siasa, hii si dini, haya ni mauaji.”

Kauli hii mbali na kulaani tukio lile, ililenga kutenganisha uhalifu na imani au itikadi za wahusika wa uhalifu huo. Ilitaka kila mtu anayefanya uhalifu huo ahukumiwe kwa matendo yake, na si kuchukulia kuwa amefanya hivyo kutokana na kile anachokiamini.

Albright alitaka kuueleza ulimwengu kuwa mashambulizi yaliyofanywa dhidi ya maslahi ya Marekani na Tanzania na kusababisha watu 11 kufariki dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa, hayakuwa vita vya kidini wala kisiasa, na walioathirika hawakuwa walengwa na vita husika.

Mfano huu ndio unafaa kutumika katika kulaani vitendo vya uhalifu vinavyoshuhudiwa sasa katika siasa. Hakuna sababu ya kuunganisha matukio haya ya watu kukatwa mapanga na kuumizwa, na sababu za siasa.

Ni uhalifu tu si siasa. Siasa haiendeshwi kwa mapanga, kumwagiana tindikali, kuuana, kupopoana kwa mawe wala kwa vitendo vingine vya kuumizana.

Siasa inafanywa kwa kujenga hoja, utumishi uliotukuka na huduma bora kwa jamii na kufafanua utekelezaji wa ahadi kwa wananchi.

Siasa hizi za mapanga hazipeleki nchi au wananchi wake popote isipokuwa badala yake zinajenga msingi mbaya kuelekea kwenye machafuko.

Ilianza kwa kushambulia wafuasi wa vyama, mawakala na sasa inaanza kuwagusa wabunge na kuna uwezekano wa matukio haya kukua na kuwafikia viongozi wa vyama kitaifa.

Na hapo ndipo yatakapotokea machafuko kwa wafuasi kuamua kulipiza kisasi au kutetea viongozi wao.

Ukitazama matukio ya Jumapili, ya wabunge wawili wa CHADEMA, Samson Highness Kiwia wa Ilemela na Salvatory Machemuli wa Ukerewe kushambuliwa kwa mapanga, utabaini kuwa hali hii imefumbiwa macho na sasa imeanza kuwa mbaya.

Siasa zinaweza kutumika kama kisingizio lakini uhalifu ndio unatangulia. Mbunge ni kiongozi anayefahamika katika jamii, hakuna anayeweza kuaminisha watu kuwa wamemshambulia bila kumjua, na huenda kuna jambo la ziada linalohitaji kuchunguzwa.

Kiwia ameumizwa vibaya katika mashambulizi hayo, na sasa amehamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kutoka Hospitali ya Rufaa Bugando, Mwanza, na inasemekana hali yake ni mbaya.

Mbali na wabunge hao, wengine pia walishambuliwa, akiwamo Ahmed Waziri ambaye inasemekana kuwa ni kada wa UVCCM aliyekatwa na wenzake kiganja cha mkono wa kulia.

Pia wamo Haji Mkweda (21), alijeruhiwa mguu wa kulia, Judhith Madaraka (26), aliyechomwa kisu kwenye titi la kushoto na mkono wa kushoto, Ivory Mchimba (26), aliyejeruhiwa kichwani na mdomoni.

Majeruhi wote ukiondoa wabunge hao na Waziri, wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Mwanza, ya Sekou Toure.

Mkoani Mbeya nako watu wanne waliokuwa wakitoka katika kituo cha kupigia kura cha Kiwira, wamejeruhiwa kwa kukatwa mapanga katika eneo la Hilondo ambalo ni maarufu kwa machimbo ya mchanga.

Waliojeruhiwa ni John Andengenye (26), Daud Hamis (27), Jacob Kalua (30) na mwingine ambaye hakutambuliwa.

Matukio hayo yaliyoibuka wakati wa kuhitimisha kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani, ni mwendelezo wa matukio yanayotokea katika maeneo mbalimbali nchini.

Mbaya zaidi chama kinachohusishwa na matukio haya ya kihalifu ni chama tawala, CCM. Hiki ndicho kinachoimba majukwaani kuwa sera yake ni “kulinda amani ya nchi”.

Inashangaza kuona chama kikongwe kama hiki kinakuwa na kauli ambazo ni tofauti na matendo yake. Ninajiuliza bila majibu, kama matendo haya ndio kulinda amani, hali ingekuwaje kama kisingekuwa na sera hiyo?

John Mnyika, Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa CHADEMA, akilaani vitendo hivyo amesema, “CCM ni chama chenye kukumbatia matusi, mafisadi, uongo na umwagaji damu; maneno yao juu ya amani na utulivu ni ya kuficha matendo maovu ya viongozi wake.”

Anaongeza, “hakika tukio hili halitaishia kusikitika na kulaani, tutachukua hatua za ziada.”

Mbunge huyu wa Ubungo, Dar es Salaam, anasema “kadiri CCM inavyoelekea kuondoka madarakani, rangi yake halisi itajihidhirisha kuwa ni chama na serikali inayokumbatia vitisho, vurugu na umwagaji damu kama njia ya kujaribu kujiokoa na kukataliwa na umma.”

Haiingii akilini kuona matukio haya yanafanyika katika maeneo ya kampeni kama Kirumba, Kiwira, Igunga, Arumeru Mashariki ambako ulinzi umeimarishwa vya kutosha.

Idadi ya askari polisi iliongezwa, vifaa vya kupambana na wahalifu vimeongezwa, maji ya kuwasha yamepelekwa ya kutosha, mashushushu wamemwagwa kila kona, lakini bado matukio ya ovyo yanatokea na hakuna anayekamatwa haraka ili kushitakiwa.

Matukio haya hayana tofauti na vitendo vya rushwa katika maeneo kulikofanyika uchaguzi, kila “mwenye macho” anaona, hongo inagawiwa waziwazi hata mikutanoni, lakini maofisa wa Takukuru wanaishia tu kuandika ripoti badala ya kukamata wahusika.

Hii inaashiria kwamba CCM wanafanya uhalifu wa kila aina hivyo kwa kutumia au kulindwa na vyombo vya dola na vikosi vya chama chao, ili kukiwezesha kubaki madarakani kwa vurugu na umwagaji damu.

Matukio haya yanakumbusha mengine ya namna hii yaliyotokea kila kulikoendeshwa uchaguzi mdogo: Kiteto, Busanda, Biharamulo, Tarime, Igunga.

Wilayani Kiteto, mwaka 2007 mashambulizi ya aina hiyo yalifanyika ndani ya kituo cha polisi. Wahalifu walikuwa ni vijana wa kikosi cha CCM, Green Guard, kwa ushirikiano na baadhi ya polisi. Hakuna aliyekamatwa wala kufunguliwa mashtaka.

Hata pale maisha ya mtu yalipopotea, kama ilivyotokea kwa wakala wa CHADEMA, Mbwana Masudi, aliyetekwa na kuuawa Igunga, polisi hawajachukua hatua hadi leo. Wamemaliza kuwa lile ni tukio la kisiasa.

Mnyika anasema katika matukio hayo yote, polisi walifungua majalada ya uchunguzi, baadhi ya watuhumiwa walitajwa kwa majina, lakini hakuna yeyote aliyefikishwa mahakamani. Polisi wanadharau uhalifu, watakuja kushindwa kudhibiti baadaye huku wakisema wanahimiza kufuata sheria bila shuruti.

CCM kimehusishwa na mlolongo wa matukio hayo ya kihalifu. Viongozi wake wamejitia kujitenga na matukio hayo ingawa mazingira yake yanathibitisha kuhusika kwa makada wake.

Inawezekana viongozi wanakubaliana na uhalifu huo, wamewatuma wahusika au hawaguswi kwa namna yoyote na mauaji, ukatili na udhalimu unaofanyika dhidi ya binadamu.

Ifike hatua, kila mtu na hasa polisi watambue kuwa wanaohusika na vurugu hizo ni wahalifu, wauaji na wahuni wanaotumia mgongo wa siasa kujificha.

Siamini kama wakuu wa Jeshi la Polisi wakiongozwa na IGP Said Mwema wanaridhika na kukubali uhalifu huu. Lazima wahalifu watenganishwe na wanasiasa na hatua stahiki zichukuliwe dhidi yao bila kuwauliza itikadi zao.

0788 346175
0
Your rating: None Average: 4 (1 vote)