Silinde: Kijana wa CHADEMA aliyeitikisa CCM Mbozi


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 16 February 2011

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii
David Sinde, Mbunge wa Mbozi Magharibi

KATIKA kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani kulikuwa na habari nyingi kuhusu baadhi ya wagombea ‘kumwaga’ fedha ili waweze kuchaguliwa.

Habari nyingi juu ya matumizi ya fedha zilisika ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Wapo walipoteza zaidi ya Sh. 20 milioni lakini hawakupita, na waliopita katika mchujo ndani ya CCM bado walikwama walipokutana na wagombea wa upinzani.

Je, wapinzani nao walimwaga fedha ili washinde katika majimbo waliyokuwa wanawania? Mbunge wa Jimbo la Mbozi Magharibi mkoani Mbeya David Sinde, anajibu swali hilo akisema hapana.

“Watu wengi wanadhani kwamba ili uwe mbunge unahitaji kuwa na kiasi kikubwa cha fedha. Hili linaweza kuwa na ukweli lakini si mara zote,” anasema .

“Mimi kabla ya kuwania ubunge nilikuwa na Sh. 25,000 ambazo nilizitumia kama nauli kutoka Dar es Salaam kwenda Mbozi kuwania ubunge. Na leo hii mimi ni mbunge wa jimbo la Mbozi,” anasimulia Silinde, aliyepita kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Si hivyo tu, ubunge ni kama ajira ya kwanza kwa Silinde ambaye alimaliza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Julai mwaka jana. Baada ya kuhitimu alikwenda moja kwa moja kuwania ubunge jimboni kwake na akashinda.

“Nilichojifunza katika kuwania kwangu ubunge ni ukweli kuwa wananchi wanahitaji kwanza mtu anayeyajua matatizo yao na mwenye kuyaeleza katika namna ambayo wananchi wanaielewa.

“Mimi ni kijana mdogo, lakini uwezo wangu wa kujenga hoja ni mkubwa. Mimi nilikuwa nikipanda jukwaani watu wanalia machozi kwa sababu ya kile ninachokieleza na si kwa sababu ya kupewa takrima.

“Ndiyo maana fomu ya kuwania ubunge nilichangiwa na wananchi kwa sababu sikuwa na fedha na pia kila baada ya mikutano ya hadhara nilikuwa nikitembeza bakuli kwa waliohudhuria ili wanichangie na wakanichangia.

“Na leo ngoja nikwambie jambo ambalo watu wengi hawajalifahamu. Katika kipindi cha kampeni, wananchi walinichangia kiasi cha Sh. 17 milioni ili nipande ushindi.

“Mimi ni miongoni mwa wabunge wachache katika Bunge hili ambao tumeingia bungeni bila ya madeni yoyote. Sikuwahi kukopa kwa ajili ya kufanya kampeni. Isipokuwa deni langu ni kwa wananchi,” anasema.

Mbunge huyo, ambaye ni miongoni mwa wabunge vijana kabisa katika bunge la sasa linaloendelea mjini Dodoma, alizaliwa Julai 28, mwaka 1984. Anamzidi kwa miaka miwili mbunge mdogo kuliko wote katika Bunge la sasa, Felix Mkosamali wa chama cha NCCR Mageuzi mwenye umri wa miaka 24.

Silinde anasema, katika maisha yake hapa duniani, hajawahi kupata tabu kama aliyoipata wakati alipokuwa katika kampeni za kuwania kuchaguliwa kuwa mbunge katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

“Nilifahamu mapema kuwa kwa sababu mgombea wa chama tawala (Chama Cha Mapinduzi—Dk Luka Siame) alikuwa na uwezo wa kifedha na kimtandao kuliko mimi. Namna pekee ya kumshinda ilikuwa kufanya kazi ya ziada,” anasema.

“Kwa hiyo, kama yeye alikuwa akifanya mikutano miwili kwa siku, mimi nilikuwa nikifanya mikutano kati ya saba hadi nane kwa siku. Hiyo haikuwa kazi ndogo.

“Mwanzoni watu walikuwa wamenidharau sana. Kwanza nilionekana mdogo na kwa vile ndiyo kwanza nilikuwa nimetoka kwenye mitihani, nilionekana kama nimechoka. Na kwa namna nilivyo mwembamba ndiyo ikawa balaa tupu.

“Kwa hiyo ilibidi nijitume sana kuliko kawaida. Nilitumia muda wangu wote, nguvu zangu zote, uelewa wangu wote wa Mbozi na kila aina ya jitihada ili nishinde. Hiyo ndiyo iliyokuwa namna pekee kwangu ya kushinda,” anasema.

Anasema mbinu yake ya kuchangisha wananchi na kufika katika maeneo mengi kupiga kampeni ilimsaidia kwa vile ana imani wote waliomchangia fedha, ndio waliompigia kura ilipofika siku ya kuamua.

“Wakati mwananchi masikini anapokuchangia Sh. 50 thamani ya fedha hiyo ni sawa na tajiri anayekuchangia milioni moja au laki tano kwa sababu, maana yake ni kuwa wote watakupigia kura,” anaeleza.

“Ni mara chache sana mwananchi atakuchangia kwenye kampeni yako na asikupigie kura siku ya mwisho kama amejiandikisha. Kwa hiyo fedha unapata lakini muhimu zaidi unajihakikishia kura,” anasema.

Silinde anasema ushindi wa chama chake katika jimbo hilo ni jambo la kihistoria kwa vile katika kipindi cha miaka takribani 50 iliyopita, tangu Tanganyika kupata uhuru wake, Mbozi haijawahi kutawaliwa na chama cha upinzani.

Anasema Mbozi haikuwahi kuwa na mbunge wala diwani kutoka upinzani achilia mbali CHADEMA, na akasema katika baadhi ya chaguzi zilizopita tangu vyama vingi viruhusiwe, wabunge wa CCM walikuwa wakipita bila ya kupingwa.

“Kwa hiyo utaona changamoto ilikuwa kubwa sana. Ndani ya familia yangu mwenyewe nilipingwa kwa sababu ya kugombea kupitia CHADEMA. Wapo wanaoamini kuwa kuwa mpinzani ni makosa. Ushindi huu kupitia CHADEMA utasaidia sana kubadilisha watu,” anasema.

Akizungumzia kero za wananchi wa Mbozi, Silinde alisema tatizo kubwa la wananchi wake ni upatikanaji wa maji na amesema katika kipindi cha miaka yake mitano ya kwanza, hiyo ndiyo itakuwa kipaumbele chake.

Alisema wananchi wa Mbozi wamekuwa wakichangishwa na serikali ya CCM kwa kipindi cha zaidi ya miaka saba wakiahidiwa kutatuliwa kero ya maji, lakini hali inazidi kuwa mbaya.

Alisema ufisadi umekuwa tatizo kubwa; akitoa mfano wa serikali kuidhinisha kiasi cha Sh. 500 milioni kwa ajili ya miradi ya maji wilayani Mbozi lakini viongozi wakaanza kwanza kuunda Bodi ya Maji ya Wilaya, ambapo wajumbe walikuwa wakijilipa kiasi cha Sh. 600,000 kwa kikao kimoja.

“Yaani imefikia watu badala ya kutengeneza visima kwa ajili ya wananchi, viongozi wanaamua kutengeneza vitu vya kula hiyo fedha. Kwanini watu wasipate kwanza maji halafu ndiyo bodi iundwe? Haya ni baadhi ya mambo ambayo sitayakubali wakati nikiwa mbunge,” anasema.

Silinde ambaye ni mzaliwa wa Mbozi, amewaahidi wananchi wa jimbo hilo kuwa tofauti na wabunge wengine ambao huishi Dar es Salaam wakati wakiwa wabunge, yeye ataishi jimboni katika kipindi chake chote cha ubunge.

“Nimeweka utaratibu wa kuhakikisha kuwa kila mwezi ninakutana na kundi moja la jamii kama vile vijana, wazee, walemavu ili kufahamu matatizo yao na namna bora ya kuyatatua. Huu ndiyo mpango wangu ili nikienda bungeni niwe nazungumza nilichotumwa,” alisema.

Silinde hajaoa na ana shahada ya biashara (BCom) aliyoipata kwa muda wa miaka minne katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Shahada hiyo huchukua muda wa miaka mitatu lakini yeye alitumia miaka minne kwa sababu ya kusimamishwa chuo mara kwa mara kwa sababu ya harakati za kutetea maslahi ya wanafunzi.

0
Your rating: None Average: 4 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: