Simba, Yanga na ushiriki wao kuiua Taifa Stars


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 14 July 2009

Printer-friendly versionSend to friend

MEI 3 mwaka huu, Shirikisho la Soka Misri (EFF), lilipitisha uamuzi wa kuzizuia klabu za nchi hiyo kusajili makipa kutoka nje ya nchi hiyo, kuanzia msimu ujao wa ligi.

Hata wale walio na mikataba, klabu zimeagizwa kuangalia uwezekano wa kutoiongeza zaidi ya msimu wa 2009/2010.

Uamuzi huo mzito wa EFF umelenga kulinda vipaji vya ndani, hasa baada ya kuonekana klabu zikikimbilia kusajili makipa kutoka nje ya nchi, badala ya kuviendeleza vipaji vya ndani.

Aidha, imesikia kilio cha Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Misri, Hassan Shehata aliyelalamikia ukame wa makipa, kwani mara kadhaa amejikuta akipasua kichwa kupata kipa wa uhakika anapokosekana mkongwe Essam El-Hadary anayeidakia Sion ya Uswisi. El-Hadary kwa sasa ana umri wa miaka 38.

Uamuzi huo ulionekana kuwa mchungu kwa klabu kadhaa, zikiwamo Harras Hodoud, Tersana, Masry na Arab Contractors, kwani zina makipa mahiri, lakini kutoka nje ya Misri.

Kwa mfano Hodoud inayomilikiwa na Jeshi la Misri, inatamba golini na kipa wa Cameroon, Mathurin Kameni, mdogo wa Carlos Kameni anayeidakia Espanyol ya Hispania.

Ni dhahiri kwamba, uamuzi wa EFA ni mgumu, lakini unapaswa kuigwa na vyama na mashirikisho ya soka barani Afrika.

Bila shaka shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ni miongoni mwa wanaopaswa kufuata nyayo za EFA, kwa kuthubutu kutaka kulinda vipaji vya nyota wao.

TFF inastahili kuiiga EFA, si katika kuwadhibiti makipa wa kigeni, ingawa nao wameivamia kwa fujo Ligi Kuu ya Bara, bali pia kwa washambuliaji.

Hakuna asiyefahamu ukame wa mabao unaoikabili timu ya Tanzania 'Taifa Stars' inayonolewa na kocha mahiri wa Kibrazil, Marcio Maximo.

Mara kadhaa tumesikia kilio cha Maximo kuhusiana na ukame wa mabao unaotokana na safu ya washambuliaji wa Kitanzania.

Bila shaka, hili linatokana na klabu zetu kubwa kuwapapatikia washambuliaji wa kigeni ambao kwa namna moja ama nyingine, huwafumika nyota wetu.

J
iulize, ndani ya miaka miwili, nani wamekuwa nyota wa mabao katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara?

Mganda Mike Katende wa Kagera Sugar anaweza kuwa jibu jepesi. Huyu ndiye aliyewika kwa upachikaji wa mabao akiwa na Kagera Sugar mwaka 2008 na hata kutwaa kiatu cha dhahabu katika Ligi Kuu.

Na hata msimu uliofuata ulioishia karibu na nusu ya mwaka huu, Boniface Ambani wa Yanga ndiye aliyetwaa kiatu cha dhahabu si katika ligi kuu pekee, bali hata Yanga alikofuatiwa na mgeni mwingine, Bernard Mwalala.

Kwa staili hii, tutegemee kuwa na makali gani katika safu ya ushambuliaji ya Taifa Stars? Bila shaka ni madudu tu, kwani hao wanaoonekana nyota Stars, hawana bao katika klabu zao, zaidi yakuwa wapiga debe katika safu ya ushambuliaji.

Utamzungumzia Tegete, huyu anafanya nini Yanga na anapewa nafasi gani? Hakuna. Hali ipo hivyo kwa akina Mrisho Ngassa anayetamba na 'chenga twawala', Haruna Moshi `Boban' na hata Mussa Hassan `Mgosi'. Wote ni waviziaji, hakuna mshambuliaji tegemeo.

Kama hali imekuwa hivi, hakuna sababu ya kuendelea kuwakumbatia nyota wa kigeni, hasa katika safu ya ushambuliaji kama ni hawa hawa wanaoidhoofisha Taifa Stars kutokana na kuwafunika wenyeji, hivyo kuwaua kabisa katika makali ya soka?

Kinachofanyika kwa sasa hakina tofauti na kujaribu kuua taratibu safu ya ushambuliaji ya Maximo, kwani kuanzia Simba, Yanga na sasa hata African Lyon, zote zinakumbatia washambuliaji mahiri wa kigeni.

Yanga ina Steven Bengo, Jama Mba, Moses Odhiambo na Kabongo Honore, Simba ina akina Emmanuel Okwi na Hillary Echesa katika kuiongezea nguvu safu ya kiungo, na African Lyon ina Ssentongo Robert kutoka Uganda .

Tujiulize, kama klabu zetu `mfano wa kuigwa' zinaendekeza nyota wa kigeni' tutarajie nini kipya kutoka kwa Maximo, kama si kutegemea nyota wa Kitanzania ambao katika klabu zao wanakaa benchi?

Ndiyo maana nashauri kwamba, kwa staili ile ile iliyotumiwa na EFF, shirikisho letu chini ya Rais Leodegar Tenga litulize akili na kufikiria uwezekano wa kuzizuia klabu kusajili washambuliaji wa kigeni, au zipunguze idadi.

Kwa kupunguza idadi au kuzuia, italisaidia taifa kupata vipaji vipya, tena vyenye ushindani kwa safu ya Taifa Stars, badala ya kuwategemea `ma-Tx' wanaotuacha solemba linapokuja suala la kimataifa.

Ni kwa staili hii tunadhani bila TFF kuamka, kila siku tutaletewa na klabu zetu washambuliaji tishio wakaoifanya Tanzania ing'are katika medani ya kimataifa, lakini linapokuja suala la Taifa Stars, washambuliaji wetu wakibaki `butu', wasiojua pa kuanzia wala pa kumalizia. Sana sana ni mchecheto t uwanjani.

Tujiulize, kwa satili mpya ya TFF ya kuruhusu nyota kumi wa kigeni kwa kila klabu kwa msimu, huku ni kukuza soka yetu au kuua? Na Tutafakari kama kweli tunaitakia mema soka ya nchi hii.

Lakini kwa jinsi ninavyoona, mwanya huu umetumiwa vyema na klabu zenye uwezo kama Simba na Yanga, zenye tamaa ya kushinda kila taji ndani ya msimu mmoja, ingawa mwisho wa siku unageuka na kuwa kitanzi kwa Taifa Stars, kwani klabu hizi kubwa zinakosa mashambulizi yale yale ya Ligi Kuu, na badala yake washambuliaji wetu baada ya kusota benchi kwa muda mrefu, huzinduka na kujaribu kuchomoa makucha, licha ya kukosa uwezo halisi uwanjani.

Kwa staili hii, Simba na Yanga zitakuwa zinaisaidia Taifa Stars au kushiriki katika kuiua? Na Tutafakari huku nikikumbuka simu na ujumbe mfupi wa maneno kutoka kwa wasomaji mbalimbali, itoshe tu kusema kwamba nimewasoma.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: