Siri ya Zitto yafichuka


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 01 September 2009

Printer-friendly version
Zitto Kabwe

SIRI ya Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Zitto Kabwe kuondoa jina lake katika kinyang’anyiro cha uenyekiti wa chama chake imejulikana.

Taarifa zinasema Kamati ya Wazee ya CHADEMA ilikuwa inahofia Zitto angeendeleza matakwa yake, “angetokomea kisiasa.”

Naye Mwanzilishi wa CHADEMA, Edwin Mtei, akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam juzi Jumatatu alisema, “Zitto bado mchanga.”

Chanzo cha habari kimemnukuu mmoja wa wazee akisema, “Kijana huyu bado ana muda. Hana haja ya kuwa na papara. Tumemlea na bado anahitaji malezi na maelekezo; lakini angekaidi angekuwa anajitokomeza mwenyewe.”

Zitto, mbunge wa CHADEMA, Kigoma Kaskazini, alichukua fomu za kuomba kuwania uenyekiti wa chama chake ili apambane na mwenyekiti wa sasa, Freeman Mbowe.

Taarifa zinasema, Kamati tayari ililetewa “dozi” (taarifa nyingi za siri) juu ya Zitto, lakini kabla hajasomewa “mabaya” yake, walimueleza kistaarabu kwamba ni vema akaondoa jina lake.

“Alipofika ndani ya Kamati, hakushinikizwa kama inavyoelezwa. Alielezwa juu ya hali ya chama na baadaye kutakiwa kutoa kauli yake kuhusu kugombea uenyekiti au kutogombea. Alisema anaondoa jina lake,” kimeeleza chanzo cha habari.

Hata hivyo, tuhuma mbili kubwa zilikuwa zikimsubiri Zitto katika Kamati Kuu (CC) ya chama chake.

Ya kwanza ni ile ya kushambulia mwenyekiti wake, Mbowe kuwa amekuwa baba wa migogoro badala ya suluhu katika chama.

Shutuma za Zitto zilitangazwa na baadhi ya vyombo vya habari nchini na nje ya nchi, likiwamo gazeti la Mwananchi na Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Ujerumani (DW).

Zitto alinukuliwa akisema, ndani ya CHADEMA kuna harufu ya ukabila; akitoa mfano wa mchakato wa kuwapata wabunge wa Viti Maalum mwaka 2005, ambapo alisema wengi walitoka mkoa wa Kilimanjaro.

“Unajua hizi tuhuma ni nzito. Zingefikishwa CC, Zitto angejimaliza. Kwanza, ni yeye aliyekuwa Katibu wa Kamati ya kutafuta wabunge wa Viti Maalum. Sasa kuna makosa yamefanyika, na yeye ndiye mhusika mkuu. Asingeweza kukwepa,” zimeeleza taarifa za ndani ya chama.

“Zitto asingeweza kuthibitisha madai kwamba mwenyekiti anahusika. Kama kuna upendeleo, basi naye angehusishwa kwa kuhakikisha anampitisha dada yake, Mheshimiwa Mhonga Saidi,” ameeleza mtoa taarifa.

Tuhuma ya pili kubwa ilikuwa ujumbe wa simu aliomtumia Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa.

Taarifa zinasema Zitto alimweleza Dk. Slaa kuwa hana “msaada wowote katika chama;” na kwamba kama kuna kiongozi ambaye ametoa mchango mkubwa katika ujenzi wa CHADEMA, basi ni yeye na Mbowe.

“Huyu dogo, nadhani ameanza kulewa sifa. Kweli ana ubavu wa kujilinganisha na Padri huyu (Dk.Slaa)? Jambo hili lingefikishwa Kamati Kuu, hakika angekutana na cha moto,” mbunge mmoja wa CHADEMA alilimbia gazeti hili.

Imeelezwa kwamba tuhuma za Zitto ndizo zilifanya hata pendekezo lake la awali kuwa Dk. Slaa agombee uenyekiti likataliwe.

“Lakini Dk. Slaa alikataa kugombe uenyekiti, akisema hataki nafasi hiyo. Sababu kubwa ni kule kushambuliwa na Zitto. Sasa kufika hapo kukawa hakuna njia nyingine, bali Zitto kukubaliana na ushauri wa wazee wa kuondoa jina lake,” ameeleza mjumbe wa kikao cha wazee.

“Unajua wazee waliona mbali, kwamba Zitto asingweza kushinda uchaguzi. Angekuwa kama Profesa Safari (Abdallah Safari, aliyeshindwa vibaya na Profesa Lipumba katika uchaguzi wa Chama cha Wananchi (CUF), jambo ambal lingemdhoofisha,” ameeleza.

Ndani ya CHADEMA taarifa zinasema Zitto hakuwa na mtandao mkubwa ambao ungemwezesha kushinda uchaguzi. Wabunge wote kumi na moja, ukimwondoa yeye na Mhonga, hawakuwa pamoja na Zitto katika uchaguzi huo.

Nguvu kubwa ya Zitto ilionekana kutoka nje ya CHADEMA, jambo ambalo lilianza kutia mashaka baadhi ya wanachama wenzake wakiwamo viongozi wakuu.

Watu pekee wanaofahamika kuwa ni wana-CHADEMA ambao walikuwa nyuma ya Zitto, ni Mkurugenzi wa Uchaguzi, Msafiri Mtemelwa, Afisa wa Habari, Devid Kafulila na mwanachama maarufu wa Dar es Salaam, Mkumbwa Kitilya.

Mtemelwa ambaye kabla ya kujiunga na CHADEMA, alikuwa amepitia vyama mbalimbali ikiwamo CCM, NCCR- Mageuzi, Tanzania Labour Party (TLP) na CUF, ndiye aliyerudisha fomu za Zitto na meneja wake wa kampeni.

Ni Mtemelwa ambaye wakati wa mtafaruku wa uongozi ndani ya chama cha NCCR- Mageuzi, alipachikwa jina la “Black Mamba” kutokana na kuandaa makundi ya vurugu na ghasia yaliyoshabikia Agustine Mrema.

Wakati huo alikuwa mwenyekiti wa taifa wa vijana na aliapa kutetea Mrema hadi kaburini. Alikaripia na kutishia kila aliyetofautiana na Mrema.

Katika uchaguzi wa CHADEMA, Mtemelwa alibwaga katika harakati zake za kuwa mjumbe wa Baraza Kuu la Taifa kupitia mkoa wa Temeke.

Taarifa zinasema karibu viongozi wa mikoa ya Mbeya, Arusha, Kilimanjaro, Pwani, Shinyanga, Mwanza, Tanga, Ruvuma, Morogoro, Manyara, Singida na Zanzibar, bado walikuwa na imani kubwa na uongozi wa Mbowe.

“Unajua hata hoja yake ya kuondoa jina ilipofika CC, hakuna mtu aliyehoji maamuzi yake. Hapa panathibitisha kuwa wazee waliona mbali, maana kama Zitto angefika mkutano mkuu angeshindwa vibaya kwa vile hakuwa na mashiko,” anasema mwanachama mmoja wa siku nyingi wa CHADEMA.

Naye mwandishi wetu, Steve Mwasubila anaripoti kuwa Mwenyekiti mstaafu wa Chama cha CHADEMA, Edwin Mtei amewakata vijana kujihadhari na mbinu chafu za mafisadi na wala rushwa ili kulinusuru taifa.

Matei alitoa kauli hiyo juzi, Jumatatu jijini Dar es Salaam katika ufunguzi wa mkutano wa uchaguzi wa vijana wa chama hicho, ambapo aliwataka vijana kuwa imara na kuepuka mitego ya mafisadi ya kutaka kukizorotesha chama kwa kuwapaka matope viongozi wake wakuu.

Alisema wakati wote amekuwa na masikitiko kwa kuwa vitendo vya kifisadi na ulaji rushwa vimekithiri nchini, wakati watoto wa masikini wakifa kwa utapiamlo.

“Kama watoto wa masikini wanakufa kwa utapiamulo, basi hiyo ni njaa, hivyo kauli ya rais kuwa hakuna mtu atakayekufa kwa njaa ni ya kusikitisha sana,” alisema.

Alisema mara kwa mara rais amekuwa akitoa kauli zenye kuacha maswali mengi kwa Watanzania wengi walio masikini.

Aidha, Mtei aliwataka vijana kujihadhari na Idara ya Usalama wa Taifa, ambayo alisema imekuwa ikivifadhili baadhi ya vyama vya upinzani kwa maslahi ya chama tawala. Hakutaja vyama hivyo.

Alisema hali hiyo ni moja ya vituvi vinavyochangia kuua demokrasia ya kweli nchini na kuendelea kukilinda chama tawala kizidi kuteketeza raslimali za nchi.

Alisema kwa miaka 48 CCM imekuwa madarakani, imeshindwa kukidhi matarajio ya Watanzania. Alisema chama hicho kimedumaa kimawazo na kimetekwa na mafisadi, huku akiwataka wana CCM wenye kukerwa na ufisadi kujiengua katika chama na kujiunga na CHADEMA.

Wakati huohuo, Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Mbowe aliwaasa waandishi wa habari kuacha kutumiwa na baadhi ya mafisadi kwa kuwa kufanya hivyo ni sawa na kushiriki “kuibaka nchi.”

Akizungumzia kuenguliwa kwa Zitto katika kuwania nafasi ya uwenyekiti, Mbowe alisema maneno yasiyostahili na yenye kuonyesha kuwepo kwa mgogoro ndani ya CHADEMA, yamekuwa yakikuzwa na vyombo vya habari wakati hali ndani ya chama hicho ni utulivu.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: