Sitta amtikisa Kikwete


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 17 November 2010

Printer-friendly version
Aliyekuwa spika wa Bunge la Jamhuri, Samwel Sitta

HATUA ya kumuengua aliyekuwa spika wa Bunge la Jamhuri, Samwel Sitta kwenye kinyang’anyiro cha uspika, ililenga kusafishia njia aliyekuwa waziri mkuu, Edward Lowassa, MwanaHALISI limeelezwa.

Taarifa kutoka ndani ya kikao cha Kamati Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilichofikia uamuzi wa kumuengua Sitta, zinasema mpango huo ulisukwa na kutekelezwa kwa ustadi mkubwa na mbunge wa Igunga, Rostam Aziz.

Lowassa anayekabiliwa na lundo la tuhuma za ufisadi anatafuta kila upenyo kuhakikisha anapata nafasi ya kushika utawala mwaka 2015.

Mjumbe mmoja wa CC aliyekuwa katika kikao kilichomuengua Sitta, na hakupenda kutajwa gazetini, amesema mkakati huo uliandaliwa na kutekelezwa na viongozi waandamizi ndani ya chama hicho.

Aliwataja viongozi hao kuwa Rostam Aziz, Edward Lowassa, Andrew Chenge na Yusuf Makamba ambaye ni katibu mkuu wa chama hicho. 

Kilichofanyika ndani ya kikao kilikuwa mwendelezo wa kile ambacho Chenge alifanya siku chache kabla ya uchaguzi wa spika.

Mjumbe huyo wa kamati kuu aliitisha mkutano wa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kutumia muda mwingi kumlaumu, kumlaani, kumshutumu na kumtuhumu Sitta kwa kile alichoita kuleta mgawanyiko katika chama na kudharalilisha serikali wakati akiwa spika (2005 – 2010).

Gazeti hili limefahamishwa kuwa aliyekuwa wa kwanza kushambulia Sitta alikuwa Haji Omari Kheri, mjumbe wa CC kutoka Zanzibar.

Kheri amenukuliwa na mtoa taarifa akimtuhumu Sitta kuwa ni mbinafsi na anayeendesha Bunge kibabe.

Mjadala juu ya Sitta uliibuka baada ya sektarieti ya chama hicho kupeleka katika mkutano wa CC majina matatu ya wagombea nafasi hiyo. Wagombea ambao majina yao yalipelekwa CC, ni Sitta, Anna Makinda na Anna Abdallah. 

Ni katika kujadili majina hayo matatu, ndipo Kheri aliibuka. Akiwa mzungumzaji wa kwanza katika kikao hicho, Kheri alisema, “Bwana huyu amejaa ubinafsi.”

Akiongea kwa ukali na msisitizo ambao haujulikani chanzo chake kwa kuwa Kheri hajawahi kuwa mbunge, wala kufanya kazi na Sitta bungeni alisisitiza, “Mwenyekiti, Sitta hatufai… Ni mbinafsi na amejaa ubinafsi.” 

Kauli ya Kheri iliungwa mkono na Spika wa Baraza la wawakilishi la Zanzibar, Pandu Ameir Kificho ambaye alimtuhumu Sitta kuwa ameligawa bunge na chama chake.

Kificho amenukuliwa akisema “mwenzetu” ameendesha bunge vibaya. Hakuleta umoja wala hakusimamia maslahi ya chama na kwamba Sitta ameleta madhara makubwa katika chama na bunge.

Taarifa zinaeleza alikuwa ni mwenyekiti wa kamati ya kampeni ya CCM, Abdulrahaman Kinana aliyetaka wajumbe kuachana na porojo kwamba Sitta amevuruga bunge. Alipendekeza Sitta aruhusiwe kutetea kiti chake.

Alisema, “Ukweli unabaki palepale, kwamba Samwel Sitta amelijengea heshima Bunge, chama chetu na yeye binafsi. Ametupa sisi na chama chetu heshima ya hali ya juu sana.”

Alisema, “Kama tunataka kumpa (uspika) mwanamke basi tumpe. Lakini bado nasisitiza, kwamba Samwel amefanya kazi na ametujengea heshima, na mimi binafsi sioni sababu ya kumuengua,” amenukuliwa Kinana akisema.

Lakini kauli ya Kinana ilizimwa mara moja na sauti ya Makamba iliyonukuliwa ikisema, “…naona huyu Kinana anamsifia sana Sitta. Kwani yeye hana kasoro?”

Akiongea kwa sauti ya juu, Makamba alisema, “…mbona Kinana hasemi mabaya ya Sitta? Kwani hana kasoro? Ndiyo tukubaliane basi kuwa Sitta anaweza kuwa na sifa, lakini kasoro zake mbona hazisemwi,” alihoji Makamba.

Naye Sophia Simba, kama ilivyokuwa kwa wajumbe waliotangulia, Kificho na Kheri, aliibuka na lundo la shutuma dhidi ya Sitta. Alisema kiongozi huyo alikuwa ameligeuza bunge kuwa kama chombo chake binafsi.

“Sitta ametugawa bungeni. Anajigamba na kujisifia. Kumpitisha tena kuwania nafasi hii, ni kujitafutia matatizo zaidi,” alinukuliwa Simba akisema.

Mara baada ya kumaliza kumshambulia Sitta, ndipo Simba akapendekeza kuwa CC ipitishe wagombea wanawake ili kuwezesha nafasi hiyo kushikiliwa kwa mara ya kwanza na mwanamke.

Hata hivyo, msimamo wa Simba ulipingwa na baadhi ya wajumbe kama vile, Kinana, Benard Membe na John Malecela. Viongozi hao waliendelea kusisitiza kuwa ni muhimu Sitta kupewa fursa ya kutetea nafasi yake.

Mjumbe mwingine aliyemtetea Sitta ni mkurugenzi wa Sera, Habari na Uenezi wa CCM, John Chiligati. Hoja ya kuwekwa spika mwanamke iliungwa mkono na viongozi wakuu wa nchi, akiwamo Rais Kikwete na rais mstaafu Ali Hassani Mwinyi.

Akiongea kwa sauti ya upole na iliyojaa diplomasia, Membe alinukuliwa akisema, “Chama chetu kiko hatarini iwapo baadhi ya viongozi wataendelea na utaratibu huu wa kung’ang’ania siasa za visasi, majungu na fitina.”

Alisema, “Kabla ya kufikia uamuzi huu, tumejiuliza kilichosababisha kutuangusha kutoka asilimia 80 mwaka 2005 hadi asilimia 61 mwaka 2010? Mbona tunajitengenezea bomu litakalotulipukia wenyewe?”

Mjumbe huyo alinukuliwa akisema Sitta ni miongoni mwa viongozi wachache sana ndani ya CCM ambao wanaheshimika mbele ya wananchi kutokana na msimamo wake wa kupinga vita vya ufisadi hadharani.

“Sitta amejijengea heshima kubwa ndani na nje ya bunge. Amekuwa akijitambulisha kuwa mpiganaji wa vita dhidi ya ufisadi. Sasa tukimuondoa kwa njia hii, nani ataelewa kwamba tumemuondoa ili kuweka spika mwanamke,” alihoji Membe.

Alisema kama lengo lilikuwa kuwa na spika mwanamke, hilo lingeelezwa mapema ili kutoa nafasi kwa Sitta kuachana na mpango wake wa kugombea nafasi hiyo.

Alisema kama walitaka kuweka spika mwanamke, “kwa nini hatukumshirikisha? Mbona hatukumueleza ili asaidie katika mchakato wa kumtafuta?”

Alisema iwapo angeshirikishwa angejiona kuwa ni sehemu ya mpango huo, kuliko hatua iliyochukuliwa ambayo “wengi wanaiona kama imelenga kumdhalilisha.”

Naye Chiligati aliweka msisitizo kuwa siasa za visasi na kukamiana haziwezi kukiweka mahali salama chama chao.

Wakati hayo yakitokea ndani ya mkutano wa CC, habari nyingine zinaeleza kuwa ni Rostam aliyesafiri hadi Iringa kukutana na Makinda ili kumshawishi kugombea nafasi ya spika.

Kabla ya kwenda Iringa, Rostam alikutana na Makinda kabla bunge la tisa la bajeti kufungwa.

Makinda amethibitishia mmoja wa marafiki zake wa karibu, ambaye ni mbunge, kwamba ni kweli aliombwa na Rostam kugombea nafasi hiyo.

Hata hivyo, alisema hiyo haina maana kwamba “…nimewekwa kulinda maslahi ya Rostam.”

“Hawa waliona kuwa ninaweza kumuangusha Sitta. Ndiyo wakanitafuta na kutaka kutumia fursa hiyo kumuangusha mbaya wao. Hii haina maana kwamba mimi nimewekwa nao,” Makinda amenukuliwa akieleza mwandani wake huyo siku moja baada ya kupitishwa na chama chake kuwania nafasi hiyo.

MwanaHALISI liliwahi kuchapisha taarifa kwamba kujitosa kwa Makinda katika nafasi hiyo kulitokana na kutekeleza ombi la Rostam.

Mara baada ya mpango wa kummaliza Sitta kufanikiwa, taarifa zinasema Rais Kikwete alituma ujumbe ili kuonana na Sitta. Waliotumwa na Kikwete wametajwa kuwa Malecela na Membe.

“Nimekutana na Sitta, lakini amesema hataki nafasi yoyote. Amepanga kuondoka katika chama kwa sababu familia yake na wenzake wengine wamemueleza kuwa hatakiwi katika chama,” kilisema chanzo cha taarifa kikinukuu mmoja wa wabunge ambao wanatajwa kuwa ni wafuasi wa Sitta. Haijafahamika kama Sitta anaendelea na msimamo wake huo.

Mbunge huyo aliongea na Sitta siku moja baada ya kiongozi huyo kuenguliwa kwenye kinyang’anyiro cha nafasi ya uspika.

Katika mazungumzo yake na rais ambayo yalidumu kwa saa nzima, tangu saa tatu asubuhi ya Alhamisi iliyopita, Sitta alieleza jinsi alivyodhalilishwa na uamuzi wa kumuondoa katika mbio za kutetea kiti chake, taarifa zimeeleza.

0
Your rating: None Average: 4.1 (10 votes)
Soma zaidi kuhusu: