Sitta, Nape wapigwa kombora


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 02 November 2011

Printer-friendly version
Nape Nnauye

MKUTANO ulioitishwa na viongozi wakuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) juzi Jumatatu kama jitihada za kutafuta ufumbuzi wa mgawanyiko mkubwa unaokikabili chama hicho umeshindwa kujenga msingi wa usuluhishi, MwanaHALISI limeelezwa.

Taarifa kutoka ndani ya mkutano huo uliofanyika kwenye ukumbi wa Karimjee, jijini Dar es Salaam, zinasema dawa ya migawanyiko hiyo bado haijapatikana.

“Picha niliyoiona katika mkutano huu ni kwamba makundi ndani ya chama chetu hayajaisha. Kila mmoja anahaha kutengeneza kundi lake ili kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na uchaguzi wa chama mwaka ujao,” ameeleza mmoja wa washiriki wa mkutano huo.

Anasema tatizo kubwa linalosababisha kushindwa kupata dawa ya mpasuko ni kule alikoita, “kuwapatanisha makoplo, wakati majemedari wanaendelea na vita.”

Mtoa taarifa huyo hakutaja alioita majemedari wanapendelea na vita, lakini bila shaka alilenga mahasimu wakuu wa siasa ndani ya chama hicho, Samwel Sitta na kundi lake kwa upande mmoja na Edward Lowassa na kundi lake kwa upande wa pili.

Mkutano huo uliokuwa chini ya Pius Msekwa makamu mwenyekiti wa chama hicho Tanzania Bara na Wilson Mukama, katibu mkuu ulishirikisha wenyeviti wa mikoa yote 26 Bara na visiwani.

MwanaHALISI limeelezwa na mtoa taarifa wake, ndani ya mkutano huo uliolenga kutafuta suluhu, wajumbe waliishia kushutumiana na kushambuliana, badala ya kutafuta vyanzo vya mpasuko na namna ya kupata ufumbuzi.

Mgawanyiko wa wazi ulionekana pale mwenyekiti wa CCM mkoani Mtwara, Dadi Mbulu alipomshambulia waziwazi katibu mwenezi wa chama hicho, Nape Nnauye, akisema ndiyo kinara wa makundi yanayokitafuna chama.

“Huyu Nape anatembea na ‘briefcase’ (mkoba) yenye majina ya viongozi wa mikoa anaowapigia debe na wale asiowataka kwa kusema, ‘majina yao hayatarudi kwenye vikao vya uteuzi,” alinukuliwa Mbulu akisema.

Kauli yake iliungwa mkono na Hamis Mgeja, mwenyekiti wa chama hicho mkoani Shinyanga.

Katika mchango wake, Mgeja alisema, “Huyu kijana anasema kuna uasi katika chama. Lakini hajasema hasa ni nani hao waasi. Anazua maneno yanayotilia mashaka viongozi wenzake. Tunataka mumdhibiti, vinginevyo chama chetu kitaelekea kubaya.”

Akiongea huku akitolea macho viongozi wake wakuu, Mgeja alisema, “Nape ni sehemu ya makundi ndani ya chama chetu. Anafahamika kuwa anatoka kundi la wale waliokwenda Mbeya na kutukana chama na serikali.” Alisisitiza, “Musipomdhibiti, tusije kulaumiana…”

Nape alituhumiwa pia kuwa amekuwa akijadili na kutolea kauli mambo ambayo hayakuamuliwa na vikao vya chama. Mfano ulitolewa ni uamuzi wa kuvuana magamba; mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), uliofanyika Aprili mwaka huu haukutaja majina ya watuhumiwa.

Naye Sitta alishambuliwa kwa tuhuma za kusaliti chama kwa kuanzisha Chama cha Jamii (CCJ) na kauli yake, kwamba kilichosababisha yeye kuong’olewa kwenye nafasi ya uspika ni njama za mafisadi.

Vick Swai, mwenyekiti wa chama hicho mkoani Kilimanjaro, John Guninita (Dar es Salaam), Mgeja (Shinyanga) na Onesmo Ngowi (Arusha), ndiyo waliojadilia kile walichoita, “kauli tata za Samwel Sitta.”

“Mheshimiwa Samwel Sitta amesikika katika kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa na ITV akisema, kung’olewa kwake kwenye kiti cha uspika kulitokana na nguvu ya mafisadi. Lakini sisi tunajua kwamba uamuzi wa kuwa na spika mwanamke ulikuwa ni wachama. Huyu bwana ametudhalilisha sisi na amemdhalilisha mwenyekiti wetu, Rais Jakaya Kikwete,” alisema Mgeja.

Mgeja anayefahamika kuwa ni kutoka kundi la Lowassa, alipinga dhana ya kujivua gamba kwa kusema inachochea mpasuko ndani ya chama.

Wakati hali ndani ya chama ikiwa tete, taarifa zinasema mkakati umesukwa wa kuuvunja uongozi wa sasa wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UV-CCM).

Kuvunjwa kwa uongozi wa sasa, kunadaiwa kunatokana na kushamiri makundi yanayomhusisha mtoto wa Rais Kikwete, Ridhiwani na baadhi ya wajumbe wa sekretarieti, kamati ya utekelezaji na baraza kuu la umoja huo.

Ndani ya UV- CCM, taarifa zinasema Ridhiwani haivi chungu kimoja na mwenyekiti wake, Benno Malisa na wala katibu mkuu, Martine Shigella.

Mgogoro kati ya Ridhiwani na makada wenzake ulianza mara baada ya baraza kuu la vijana kumteuwa Hussen Bashe, mfuasi wa karibu wa Lowassa kuwa mwenyekiti wa kamati ya kutafuta mpasuko ndani ya umoja huo.

Aidha, hatua ya Shigella kuridhia baadhi ya vijana kutoa kauli, tena nje ya vikao kuituhumu serikali ya baba yake na CCM, inatajwa kuwa ni kiini kingine cha mivutano kati ya Ridhwani na kigogo huyo.

“Unajua kaka, mgogoro wa sasa umetokana na hatua ya Shigella na Benno kugoma kumtumikia Ridhiwani, badala yake kukitumikia chama. Kuona hivyo, Ridhiwani na kundi lake wakaamua kutafuta njia ya mkato kuvunja uongozi wa sasa wa UV-CCM,” ameeleza mjumbe mmoja wa UV-CCM kwa sharti la kutotajwa gazetini.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: