Sophia Simba ajiundia kitanzi


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 02 December 2009

Printer-friendly versionSend to friend

KITANZI ambacho Sophia Simba, mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) anasuka ili “kunyongea” wabunge wa viti maalum, huenda kikaanzia kwake.

Chini ya uenyekiti wake mjini Dodoma mwezi uliopita, Baraza Kuu la UWT lilipitisha, kwa kauli moja, kanuni kwamba ubunge wa viti maalum uwe kwa awamu mbili tu (miaka 10) ili wanawake wengi waweze “kuonja keki” ya bungeni.

Iwapo mradi huo utapitishwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho UWT ni jumuia yake, jumla ya mawaziri wanne na wabunge 13 waliopata ubunge kupitia viti maalumu kwa miaka 10 mfululizo, watakuwa wametupwa nje.

Miongoni mwa hao watakaotupwa nje ni mwenyekiti wa UWT kitaifa, Sophia Simba.

Kanuni inasema wabunge wa CCM wa viti maalum sharti wawe bungeni kwa miaka kumi na baada ya hapo, wanaotaka kuendelea kuwa bungeni, waende majimboni kugombea.

Kwa kanuni hiyo, wabunge 21 kwa tiketi ya CCM watakuwa wamepoteza sifa ya kupata ubunge kwa viti maalumu.

Sophia Simba ambaye kwa sasa ni mbunge wa kuteuliwa na rais amewahi kuwa bungeni kwa vipindi viwili mfululizo kwa tiketi ya viti maalum.

Aidha, waziri Simba anaendelea katika kipindi cha tatu bungeni akiwa ameteuliwa na rais baada ya kushindwa katika kinyang’anyiro cha wazi jimboni Ilala, Dar es Salaam, viti maalum na kuambulia nafasi ya pili katika kapu.

Sophia Simba aweza kukumbana na kitanzi chake mwenyewe mwaka kesho wakati anajiandaa kuwa mbunge kwa njia ya viti maalum kupitia uenyekjiti wa UWT.

Akiwa tayari amemaliza vipindi viwili mfululizo na yumo katika kipindi cha tatu, hata kama ameteuliwa na rais, bado atabanwa na kanuni inayositisha uwakilishi kwa njia ya viti maalum nje ya miaka 10.

Alipoombwa kueleza iwapo ameishaanza kujiandaa kuingia bungeni kupitia kugombea na katika jimbo lipi, Sofia aliangua kicheko na kusema, “Jimbo langu lilelile la siku zote.”

Mwandishi: Lipi?

Sophia: Si lilelile! Ilala…

Bali alipong’ang’anizwa kuwa naye aweza kupoteza fursa anayoipata ya kuingia bungeni kwa tiketi ya mwenyekiti wa UWT-Taifa, kwa vile naye amekuwa mbunge kwa miaka 10 mfululizo, kwanza Sophia alisita na baadaye alisema:

“Sina mpango wa kugombea ubunge kupitia jimbo lolote kwa sababu nitakuwa na jukumu la kuzunguka nchi nzima, kuongeza nguvu kwa wanawake wenzangu watakaogombea kupitia majimboni.”
 
Amesema endapo “itathibitika” kuwa kwa kanuni hiyo hastahili kuingia bungeni, hatalalamika kwa sababu lengo kuu la umoja wake ni kuhakikisha idadi ya wanawake bungeni inaongezeka.

Hata hivyo Sophia anasema tofauti na ilivyo kwa baadhi ya wabunge wanawake, yeye amewahi kugombea ubunge jimbo la Ilala. Alishindwa.

“At least (angalau) nilionyesha kuthubutu. Tulikuwa wanawake saba, akina Anne Kilango, Jenista Mhagama, Ruth Msafiri na wengine. Watano kati yetu walishinda, wawili tukashindwa,” alibainisha.

Anasema kwa msingi huo, anaamini kanuni aliyotunga haitamning’iniza.

Hata hivyo bado kuna dhana kwamba kanuni hiyo itaibua mtafaruku ndani ya CCM kufuatia kuwepo taarifa zenye uhakika kwamba hoja ya kuweka ukomo wa ubunge kwa kupitia viti maalumu ilikataliwa na moja ya vikao vya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa suala hilo ni moja ya mambo yaliyojadiliwa na NEC kufuatia kuwa miongoni mwa mapendekezo ya Tume ya Bilali.

Hoja iliyojengwa na mmoja wa wajumbe wa mkutano huo na kufanikiwa ‘kuua’ pendekezo hilo la Tume, ni iliyotaka ubunge kupitia majimbo pia uwekewe ukomo endapo ubunge wa viti maalumu utaamuliwa kuwa na ukomo.

Hitimisho juu ya suala hilo lilifikiwa kwamba ubunge kwa viti maalumu usiwe na ukomo. Katika hali isiyo ya kawaida, baraza kuu la UWT limeibua uamuzi mpya unaokinzana na maamuzi makuu ya chama.

Katibu Mkuu wa CCM-Taifa, Yusuph Makamba, alipoombwa kueleza kinachoendelea kuhusu uamuzi huo wa UWT alisema kwa njia ya simu, “Mambo hayo nakuomba umtafute Chiligati (John Chiligati Katibu Mwenezi wa CCM-Taifa) ndiye mwenye jukumu la kuzungumzia masuala hayo.” Baada ya hayo, alikata simu.

Hata hivyo, baadhi ya wajumbe wa Baraza Kuu ambao pia ni viongozi wa UWT wa mikoa mbalimbali, wanasema ni wakati muafaka kwa uamuzi huo  kutekelezwa kwa vitendo.

Amina Kanyogoto ambaye ni Katibu wa UWT mkoani Dodoma, anasema mwanasiasa aliyedumu bungeni kwa miaka 10 anakuwa ameimarika katika nyanja mbalimbali za kisiasa kuweza kukabiliana na mashindano ya kisiasa jimboni.

Anasema mtu huyo akipambanishwa na wanawake wengine ndani ya UWT, kugombea ubunge kwa viti maalumu lazima ataibuka mshindi na hivyo kuwakosesha wanasiasa chipukizi fursa ya kujijenga kisiasa.

Kuna madai kwamba Sophia amesimamia kanuni ya vipindi viwili kwa wabunge wa viti maalum ikiwa njia ya kutaka kupata nafasi za kuzawadia wenyeviti na makatibu wa mikoa waliomuunga mkono.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: