Spika Makinda na ‘kiatu pwayu’


Edson Kilatu's picture

Na Edson Kilatu - Imechapwa 04 May 2011

Printer-friendly version

NAUNGANA na wanaosema Spika Anne Makinda hana uwezo wa kuongoza bunge; hasa bunge la sasa. Chombo hiki kikuu nchini – Bunge – kina majukumu matatu makuu: kutunga sheria, kushauri na kusimamia serikali na kuwakilisha wananchi.

Mamkala ya spika yaliyoainishwa katika Kanuni Na. 8 ya Kanuni za Kudumu za Bunge za mwaka 2007, pamoja na mambo mengine, yanamtaka spika “…kuendesha shughuli za Bunge na kutoa maamuzi kwa haki, uadilifu na bila chuki wala upendeleo wowote kwa kuongozwa na katiba ya nchi.”

Kanuni inasema, “Spika hatafungwa na msimamo utakaowekwa au makubaliano yatakayofikiwa na kamati yoyote ya chama cha siasa kinachowakishwa bungeni.”

Lakini sote ni mashahidi wa jinsi Makinda alivyotanguliza ushabiki wa chama chake katika kuendesha Bunge.

Hatua ya Makinda ya kumtaka mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema kuleta ushahidi bungeni kutokana na kauli ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda juu ya hoja ya mauaji ya Arusha, kisha asimruhusu kuiwasilisha bungeni, ni moja ya vidhibiti kuwa kiongozi huyo wa bunge amekwama.

Lema aliomba mwongozo wa spika juu ya hatua gani zinaweza kuchukuliwa kwa kiongozi kama waziri mkuu pale itakapobainika kuwa  amedanganya bunge na taifa. Lakini Makinda alikuja juu, nje kabisa ya hoja ya mbunge, na kumtaka mbunge atoe uthibitisho kuwa Pinda alisema “uwongo.”

Kanuni Na. 63 inampa fursa mbunge yeyote anayetilia shaka kauli ya mbunge mwenzake, kutoa ukweli wa jambo hilo na baada ya hapo, kwa mujibu wa Kanuni Na. 63(5), spika au mbunge mwingine aweza kumtaka mbunge huyo kulithibitisha jambo hilo.

Lakini kinyume na kanuni hii, spika Makinda alimshutumu Lema bila kujenga misingi ya shaka yake. Vitisho hivi ni kinyume na Ibara ya 100 ya katiba ya Muungano inayolinda uhuru wa mawazo wakati wa majadiliano.

Hata katika chaguzi ndani ya bunge kumetokea ukiukwaji wa kanuni. Mfano hai ni uchaguzi wa wabunge wanaokwenda kwenye mabunge mengine.

Katika uchaguzi huo, kanuni Na. 12 pamoja na nyongeza ya pili fasiri ya 5 (2) (c) ilikiukwa. Kanuni inaweka bayana kuwa ikiwa itatokea mgombea hana mpinzani, wabunge watapigakura ya ndiyo au hapana.

Lakini katika hali ya kushangaza Spika Makinda alimtangaza Sophia Simba kuwa mshindi wa nafasi hiyo bila kufuata utaratibu uliobainishwa kwenye kanuni. Kisheria nafasi hii iko wazi kwa sababu utekelezaji wake ulikiuka kanuni.

Nao uchaguzi wa wenyeviti wa bunge uliendeshwa bila kufuata taratibu. Kanuni Na. 11 inatoa utaratibu wa uchaguzi; pamoja na mambo mengine inahitaji majina sita kupigiwa kura ili kupata washindi watatu.

Kama kawaida spika alitumia ubabe kwa kuleta majina matatu na kusababisha malumbano kati yake na wabunge wa upinzani, hasa CHADEMA.

Si hivyo tu. Spika amekuwa akipuuza maslahi ya umma, hasa kanuni Na.  8(b) inayomtaka asifungwe na misimamo ya chama anamotoka.

Kwa mfano, wakati wa mjadala wa mswada wa mahakama, Spika Makinda alionekana wazi kutothamini mchango wa Tundu Lissu, mbunge wa CHADEMA (Singida Mashariki).

Ilionekana wazi kuwa spika alitaka kutetea muswada wa serikali ya chama chake; wakati ukweli ni kwamba, pamoja na mjadala kuchukua  muda mwingi, serikali italazimika kufanyia mabadiliko sheria hiyo si muda mrefu kutoka sasa.

Ni nani asiyejua madhara ya kuwapo wakuu wa mikoa na maafisa usalama wa wilaya katika kamati za nidhamu za mahakama? Je, hilo limewekwa kwa maslahi ya nani?

Hata pale kura zilipopingwa kwa njia ya kuita mbunge mmojammoja, spika alishangaa kuonawaziri mkuu Mizengo Pinda akipiga kura upande wa upinzani.

Alilazimika kuamuru katibu wa bunge kumuuliza Pinda mara tatu, iwapo anapiga kura kinyume cha matakwa ya serikali. Hii haikuwa kwa maana ya kuona nani ana hoja bora kwa taifa, bali nani anaunga mkono serikali. Muswada huu utaendelea kuwa donda katika utendaji wa Spika Anne.

Kimsingi hakuna mwenye mashaka na uzoefu wa Makinda ndani ya bungeni, akiwa mbunge wa kawaida. Lakini katika uspika, na kwa kulinganisha na mtangulizi wake, Samwel Sitta, hakika miguu ya Makinda bado inapwaya katika “kiatu” hiki.

Spika Makinda ataendelea kulaumiwa iwapo ataendelea kusimamia matakwa ya CCM na serikali yake, badala ya matakwa ya wananchi. Kwani, kwa mifano tuliyoona hapo juu, hakuna uzalendo; hakuna ujasiri wa kutetea ukweli, uwazi na haki.

Labda tuendelee kukubali kuwa bado anajifunza.

Mwandishi wa makala hii, Edson Kilatu amejitambulisha kuwa msomaji wa MwanaHALISI. Anapatikana kwa simu Na. 0713 - 815001, imeili: kilatu2004@yahoo.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: