Sura tatu muhimu za kukidhi matumaini ya Wazanzibari

WAJUMBE wapatao 200 wanatangaziwa hivi: ALI Mohamed Shein 117, Mohamed Gharib Bilal 54 na Shamsi Vuai Nahodha 33.
Tangazo linatolewa ndani ya ukumbi wa mikutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (NEC-CCM) mjini Dodoma.
Ukumbi huu unaoitwa kwa jina jingine la White House, pembeni mwa jengo la Makao Makuu ya CCM, unatajwa kuwa unatunza jina lake la umaarufu kwa wanachama wa Zanzibar – Machinjio ya maslahi ya Wazanzibari.
Sina hakika kama wanaolalamika wanaangalia maslahi ya Wazanzibari au yao au ya chama chao CCM.
Wanachama waliofurahia hatua ya Dk. Bilal kuchukua fomu na kuirudisha kwa mbwembwe nyingi, leo wanatoa vilio. Wamekasirika na wameanza kuahidi chuki dhidi ya chama chao.
Wanatofautiana na matokeo hayo. Hawataki kuyaamini kwa kuwa wanasema, “tunaamini mgombea kipenzi chetu amehujumiwa.” Eti ameibiwa kura.
Nawasikitikia bali nawaonea huruma. Wanataka maslahi yao; chama kina maslahi yake; siasa za kinchi zenyewe zina maslahi yake vilevile. Labda wakuu wa CCM wamezingatia yote haya. Nani anajua kutegua kitendawili kisichotegwa?
Tulio nje ya wigo wa CCM tunajua harakati za uteuzi wa jina la mgombea wa kiti cha urais wa Zanzibar kwa uchaguzi wa Oktoba 2010, zimekwisha. CCM imepata mgombea wa kushindana na wagombea wa vyama vingine vitakavyoshiriki uchaguzi.
Ni hadithi ndefu. Mazingira yalijitengeneza na yakawezesha wenye macho makubwa, waona mbali na karibu, kufahamu mapema. Wapo wasomaji wa alama za nyakati wanajua khabari hizi.
Zanzibar imeanza. Inaendelea. Dhamira iliyojengwa na Rais Amani Abeid Karume, Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, pamoja na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad imepata nguvu.
Wanataka kuiona nchi inatulia. Inapata serikali madhubuti ya kupendwa na kila mwananchi. Wanataka serikali ya kupata mchango wa kila mwananchi. Wanataka serikali inayopenda watu na ya viongozi wanaojali watu na haki zao. Wanataka serikali inayochukia maovu ikiwemo dhulma na utawala mbaya. Wanataka siasa ya maridhiano ili kujenga uchumi imara na jamii safi.
Hatua ya CCM kutoka na jina la Dk. Shein, Makamu wa Rais wa Tanzania tangu Julai 2002, inachukuliwa na wachambuzi na wadadisi wa siasa za Zanzibar, kama nguvu muhimu katika dhamira yao hiyo.
Na kila nikiangalia yaliyokuwepo wakati wa harakati za CCM kupata mgombea urais Zanzibar, yanayotokea baada ya kutajwa kwake, naona ni kweli kazi moja muhimu imekamilika. Tuendelee mbele.
Dk. Shein ni mmoja wa makada watatu, kati ya 11 waliochukua fomu za kuomba CCM iwateue kugombea urais Zanzibar, waliotamka waziwazi kuunga mkono dhamira inayosubiri idhini ya wananchi wa Unguja na Pemba, kupitia kura ya maoni.
Yeye alisema kura ya maoni ni hatua iliyotokana na maamuzi ya vikao vya juu vya CCM vya Butiama mwaka 2008. Kilichobaki baada ya serikali kukamilisha maandalizi ya kisheria ni kuipitisha siku itakapofika.
Kura ya maoni itapigwa 31 Julai. Ililetwa kwa sheria na Baraza la Wawakilishi baada ya kukubali hoja binafsi ya kiongozi wa upinzani barazani, Abubakar Khamis Bakary, ambaye ni mwakilishi wa Mgogoni, Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Kura hii inalenga kutandika mazingira yatakayowezesha Zanzibar kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa kama hatua muhimu ya kumaliza mgogoro wa kisiasa uliodumu kwa miaka mingi, ambao kwa kiasi kikubwa umezidishwa na utamaduni mbaya wa watawala kutotaka mabadiliko na hivyo kutumia dola kuvuruga uchaguzi usiwe uliokidhi vigezo vya kidemokrasia.
Maendeleo haya ya kisiasa yamekuwa yakiumiza baadhi ya wanasiasa magwiji Zanzibar na wamekuwa wakitumia uzoefu wao na kukubalika kwao kuwashawishi wananchi waikatae kura na hivyo kukwamisha dhamira ya kujenga maridhiano.
Ni bahati njema Dk. Shein si mmoja wa wanasiasa hao. Alieleza msimamo wake kwa ufasaha katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika 7 Juni katika Hoteli ya Bwawani, Zanzibar, mara tu baada ya kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya chama chake.
Kwa sababu umma ulikuwa ukisubiri kwa hamu mgombea wa CCM kwa kuamini kwamba msimamo wake utakuwa nguvu au udhaifu wakati wa kura ya maoni, sasa uhakika umepatikana. Matumaini ni kura kufanikiwa kwani anatumainiwa anaridhia maridhiano.
Katika siasa hakuna lisilowezekana. Nani aliamini itatokea siku CCM itapitisha jina la kada wake kutoka kisiwa cha Pemba ili agombee urais Zanzibar? Kwa Mwenyezi Mungu hakuna kubwa. Sasa imekuwa.
Lakini pia wangapi waliamini itakuja siku nafasi hii ya uongozi ya juu kabisa nchini petu itawaniwa na wanasiasa wa vyama vinavyovutana wote wakitokea Pemba? Wangapi? Sasa imetokea.
Dk. Shein ni mzaliwa wa Chokocho, jimbo la Mkanyageni, Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba. Mwenyewe anasema ametoka kwenye mifupa ya Afro-Shirazi Party (ASP).
Mgombea mshindani wake mkubwa, Maalim Seif, ni mzaliwa wa Mtambwe, Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba. Naye anajulikana alivyokuwa amezama ndani ya siasa za ASP na hatimaye CCM kabla ya kutupwa nje mwaka 1987 akiwa na wenzake kadhaa.
Kwa mara ya kwanza Zanzibar itafanya uchaguzi kwa kuwatazama wanasiasa wawili wanaotoka Pemba. Ni rahisi kusema rais ajaye Zanzibar atakuwa ni Mpemba (bali hili si kabila).
Mabadiliko makubwa kiasi gani haya! Ndivyo hali ya mambo ilivyojijenga; ndivyo muumba ametaraji na amewezesha waja wake tufike hapa.
Bali kufika tulipo, hata hivyo, haikuja hivihivi. Mambo hayakuwa rahisi hivyo. Vilikuwepo vishindo na misuguano mingi kati ya wanasiasa. Wapo wasiopenda mabadiliko – wahafidhina – wamekuwa wakivuta kamba nyuma ili wananchi wasifike kwenye neema kama yalivyo matumaini yao.
Matumaini yao sasa yanasubiri siku ya mwisho ya mwezi huu wapige kura muhimu ya kuthibitisha mabadiliko wanayoyataka ya kimfumo katika uendeshaji wa nchi yao.
Wazanzibari sasa wanatizama sura tatu: Karume anayetoka, na Seif na Shein wanaoingia. Karume atakabidhi kiti kwa mmoja wa hao. Nao watatarajiwa kushirikiana kuiongoza Zanzibar, pamoja na kuwa watiifu wa vyama tofauti – CCM na CUF. Mazingira yamevilazimisha vishirikiane.
Ni vipi wataongoza jahazi lililojaa abiria – Wazanzibari wenyewe – wanaotaka kuvuka salama bahari iliyojaa mawimbi na dhoruba kali kwa muda mrefu. Iwe safari ya kheri Inshaallah.