Suzan Lyimo: Nitagombea ubunge Kinondoni


Aristariko Konga's picture

Na Aristariko Konga - Imechapwa 02 June 2009

Printer-friendly version
Suzan Lyimo,  Mbunge wa Viti Maalum kupitia CHADEMA

“NINATAKA kugombea ubunge jimboni mwaka 2010. Ni ama Ubungo au Kinondoni.” Hiyo ni kauli ya Suzan Lyimo, Mbunge wa Viti Maalum kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wakati wa mahojiano maalum na MwanaHALISI, Jumamosi wiki iliyopita.

Anazo sababu za kufanya hivyo pamoja na changamoto kubwa ambazo akinamama wanakabiliana nazo wanapojiingiza kwenye uchaguzi wa ubunge kwenye majimbo.

Kwanza, ni kutokana na changamoto nyingi alizozipata akiwa mbunge kuanzia mwaka 2005. Amekuwa ni mwenyekiti wa Chama cha Wabunge Wanawake Tanzania (TWPG).

“Kupitia chama hiki, nikiwa mwenyekiti, nimeshiriki kuunda Mpango Mkakati wa 2006 hadi 2010 wa kuhakikisha kunakuwa na wabunge wengi wanawake,” anasema Suzan Lyimo.

Wakati alipokuwa Afrika Kusini kwenye mkutano wa wabunge wanawake, alichaguliwa kuwa mjumbe wa Kamati ya Uratibu wa Wanawake katika Bunge la Dunia (IPU), akiwakilisha nchi za Mashariki mwa Afrika.

“Kutokana na kuwa mbunge pamoja na nyadhifa hizo nilizokuwa nazo, nimeweza kushiriki katika mikutano na mafunzo mbalimbali ya kitaifa na kimataifa…hizo fursa zimenisaidia kujua mambo mengi kiasi cha kunifanya nitafute jimbo la kugombea.”

Suzan anasema kuwa angependa sana agombee Jimbo la Ubungo, Dar es Salaam, kwa kuwa ameishi humo kwa zaidi ya miaka 20 akiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Hata hivyo, anasema kuwa hawezi kufanya hivyo hadi afikie mwafaka na aliyekuwa mgombea wa CHADEMA katika jimbo hilo mwaka 2005, John Mnyika.

“Ninaendelea kuzungumza na Mnyika. Ninasubiri uamuzi wake. Kama ataendelea kugombea pale (Ubungo), basi mimi nitagombea Jimbo la Kinondoni.”

Suzan anasema atajitosa katika Jimbo la Kinondoni kwa sababu tatu kubwa:

Kwanza, kwa kuwa jimbo la Kinondoni lina  makao makuu ya CHADEMA. Pili, kutokana na jimbo hilo kuwa karibu na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambako anaishi; na tatu, kwa sababu ameishi miaka yote katika Wilaya ya Kinondoni.

“Nimelazimika kugombea katika jimbo ili nitoe fursa kwa watu wengine kuingia katika Bunge kwa fursa za viti maalum na pia kutimiza wito wa kuhamasisha wanawake wengi zaidi kwenda kugombea kwenye majimbo.”

Suzan Lyimo anasema kwamba wanawaake wengi hivi sasa wana fursa nyingi zaidi za kuweza kushinda ubunge kwenye majimbo, tofauti na zamani, kwa kuwa wana uwezo mkubwa wa kuongoza baada ya kuwezeshwa kielimu na kiuchumi.

Anasema kuwa katika siku ambazo alipata huzuni kubwa akiwa mbunge ni pale Bunge lilipopitisha uamuzi wa kumsimamisha ubunge Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), kutokana na kauli katika Bunge kuhusu utata wa mkataba wa mgodi wa Buzwagi, Shinyanga, kusainiwa nje ya nchi.

“Jambo lililonikwaza nikiwa kwenye Bunge ni wakati ulipopitishwa uamuzi wa kumsimamisha Zitto Kabwe. Nilisikitishwa sana. Uamuzi ule ulipitishwa kutokana na uchache wa wapinzani. Tulijitahidi kumtetea na kupinga hatua ile, lakini wabunge wa CCM, kwa wingi wao, wakafanikiwa. Akasimamishwa kwa kutumia kanuni.

“Lakini kinachonifurahisha ni kuwa sisi wapinzani tumekuwa tukifanya tafiti za kina na za kutosha. Bila kufanya hivyo, viongozi waliojiuzulu wangekuwa bado wako madarakani.”

Hapo Suzan Lyimo anarejea viongozi waliolazimika kujiuzulu mapema mwaka jana kutokana na kashfa ya kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond Development.

Viongozi hao ni pamoja na aliyekuwa Waziri Mkuu  Edward Lowassa, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi na aliyekuwa Waziri wa Afrika Mashariki, Dk. Ibrahim Msabaha.

“Katika CCM nako, wanaofichua maovu wanapata hamasa kutoka kwa wapinzani,” anasema.

Kuhusu uchaguzi mdogo wa Bunge katika Jimbo la Busanda, wilayani Geita, Mwanza, anasema kuwa amepata mafunzo kadhaa.

Kwamba CCM walitumia ubabe wa hali ya juu kwa kuwatishia wananchi, kwamba wasipokichagua chama hicho basi hawawezi kupata maendeleo.

Lakini pia anasema kulikuwa na hujuma nyingi wakati wa kampeni. Kwamba kulikuwa na watu waliokuwa wamepandikizwa na chama tawala ili kuchukua shahada kwa mbinu mbalimbali.

“Nilikwenda Busanda katika hatua za mwisho za kampeni. CCM walikuwa wanagawa vitu kama vile chumvi na sabuni. Wananchi wanatoa shahada zao kwa madiwani, mabalozi wa mashina na watendaji. Matokeo yake ni kwamba siku ya uchaguzi wengi walidai zimepotea.

“Kingine nilichojifunza ni uchanga wa vyama vya upinzani. Elimu ya uraia ni ndogo. CCM wanawatumia viongozi hao kwa manufaa yao. Ujue mabalozi wa mashina, watendaji na madiwani wanaonekana miungu-watu vijijini. Ni pigo sana kwetu.

“Kuna watu wengi, lakini hawana uelewa. Vijijini watu wanajihusisha sana na kilimo. Hawafiki kwenye mikutano. Kuna dalili za watu kukata tamaa. Wanaona hakuna haja ya kushiriki kwenye uchaguzi kwa kuwa wanaona hawanufaiki nao,” anasema Lyimo.

Kwa mtazamo huo, anaona njia mojawapo ya wapinzani kuondokana na hali hiyo ni kuanza kuelekeza nguvu vijijini mapema kwa sababu hakuna mtandao mzuri wa upinzani.

Funzo jingine ni kuwa CCM na serikali hawahamasishi watu kupiga kura. Kwamba wengi hawaelewi umuhimu wa shahada za kupiga kura. “Wakipoteza au kuuza, kwao ni sawa tu.”

Suzan Lyimo aliingia rasmi kwenye siasa mwaka 2004 alipojiunga na CHADEMA, ingawa kabla ya hapo alikuwa anashiriki kwenye harakati za kisiasa chinichini.

Suzan na mumewe, ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wamejaliwa kupata watoto wanne, watatu wakiwa ni wa kiume.

Anapendelea zaidi kuangalia televisheni na kusoma magazeti mara baada ya kazi.

Suzan ana shahada ya kwanza ya Sanaa na Ualimu (B.A with Education) kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Pia ana shahada ya uzamili katika Saikolojia ya Jamii.

Amewahi kufundisha katika Shule ya Sekondari ya Jangwani, Dar es Salaam. Mpaka sasa ni Waziri Kivuli wa Elimu.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: