Tahadhari ichukuliwe uraia wa nchi mbili
MWISHONI mwa wiki iliyopita, serikali kupitia Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, ilitangaza uamuzi wake wa kuruhusu uraia wa nchi mbili.
Chini ya utaratibu huo, Watanzania sasa wataruhusiwa kuwa na uraia wa nchi mbili, tofauti na sasa.
Kwa mujibu wa Membe, ili utaratibu huo uanze kutumika nchini, ni muhimu ukapata ridhaa ya mawaziri na kufuata taratibu nyingine zilizowekwa kwa mujibu wa Katiba.
Tanzania haitakuwa nchi ya kwanza duniani kuruhusu raia wake kuwa na uraia wa nchi mbili. Nchi zilizoendelea kama Canada zina utaratibu wa aina hii na nchi zinazoendelea kama Brazil pia zina utaratibu huu.
Tunafahamu ya kuwa Watanzania wengi bado wana wasiwasi na utaratibu huu mpya. Wengi wanaona hii inaweza kuondoa utaifa wa watu wao.
Hata hivyo, uzoefu umeonyesha kwamba kinyume cha mawazo ya namna hiyo, utaratibu wa uraia wa nchi mbili umekuwa hauna athari zozote kwenye namna wananchi wanavyopenda taifa lao.
Taifa kwa mtu ni sawa na mzazi. Hata kama atakuja kuwa mtu wa namna gani huko baadaye, hakuna mtu anayeweza kusahau mzazi wake.
Katika dunia ya sasa ya utandawazi, ambapo makumi kwa mamia ya Watanzania wanaishi na kufanya kazi nje ya nchi, suala hili la uraia wa nchi mbili ni muhimu.
Kaka, dada, baba na ndugu zetu waliochukua uraia wa nchi nyingine kwa sababu za kutafuta maisha na kujikwamua kiuchumi, wataweza sasa kuendelea kuwa Watanzania.
Wanasoka na wanamichezo wengine wenye asili ya Tanzania lakini walio na uraia wa nchi nyingine, sasa wataweza kuchukua uraia wa nchi yetu na kulisaidia taifa hili katika upande huo huku wakiendelea kuhesabika raia wa nchi hizo pia.
Rai yetu kwa serikali ni kwamba katika kipindi hiki inapofanya kila iwezalo kuhakikisha utaratibu huu mpya unaanza, ihakikishe pia inachukua tahadhari fursa hiyo iditumike vibaya.
Hii isiwe fursa ya kuwapa watu wasiohusika uraia kwa kigezo tu cha uraia wa nchi mbili.
Hivyo, tunashauri serikali izibe mianya yote ya maovu na mabaya mengine ambayo yanaweza kujipenyeza kutokana na utaratibu huu wa sasa kuanza kufanya kazi.