Tamko la CHADEMA mauaji Arusha


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 12 January 2011

Printer-friendly version

JUMATANO iliyopita, Jeshi la polisi nchini lilishambulia wanachama, viongozi na wafuasi wa chama kikuu cha upinzani nchini (CHADEMA) waliokuwa wanaelekea katika mkutano wa hadhara uliopangwa kufanyika katika uwanja wa Unga Limited, ambapo watu watatu inadaiwa walikufa na wengine kadhaa kujeruhiwa. Kufuatia tukio hilo, CHADEMA makao makuu ilitoa tamko lililosomwa kwa waandishi wa habari na mwanasheria wa chama hicho, Mabere Marando, 6 Januari 2011. Ifuatayo ni sehemu ya maelezo hayo…

 

Tarehe 5 Januari 2011, zilitokea vurugu katika jiji la Arusha zilizosababishwa na jeshi la polisi kuzuia viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), pamoja na wananchi wengine kutembea kwa miguu kwenda katika mkutano wa hadhara uliopamgwa kufanyika katika viwanja vya Unga Limited.

Jeshi la polisi lilikuwa na habari na mkutano huo na waliahidi kuwepo ili kulinda usalama.

Siku chache kabla ya mkutano huo kufanyika viongozi wa CHADEMA mkoani Arusha walitoa taarifa ya nia ya kufanya maandamano pia.

Polisi waliwaandikia barua ya kukubaliana na nia hiyo na kuwahidi kutoa ulinzi katika maandamano hayo.

Lakini siku moja baada ya maandano hayo kuruhusiwa, mkuu wa jeshi la polisi alionekana kwenye vyombo vya habari akisema, “Maandamano hayo yamezuiwa.”

Kauli hiyo haikueleweka kwa viongozi wa CHADEMA kwa sababu hakuwa na mawasiliano ya maandishi yaliyofikishwa katika chama CHADEMA yakibatilisha ile barua yao ya awali iliyokubali maandamano.

Hivyo, uongozi wa CHADEMA taifaifa, kutokana na kibali hicho cha awali, ulishasafiri kwa ndege na usafiri mwingine kwenda Arusha kushiriki katika tukio hilo.

Kufuatia kauli ya mkuu wa jeshi la Polisi (IGP), uongozi wa CHADEMA uliamua kusitisha maandamano hayo, huku wao wenyewe wakiamua kutembea kwa miguu kwenda kwenye viwanja vya mkutano.

Baadhi ya wananchi na wanachama waliamua kutembea pamoja na viongozi wao. Walitembea hivyo kwa takribani kilomita mbili, wakisindikizwa na polisi wa doria na wa kawaida.

Matembezi hayo yaliendelea kwa umbali huo kwa utulivu na amani kubwa mpaka walipofika sehemu inayoitwa Sanawari ambapo polisi waliamua kuwatawanya kwa mabomu ya machozi na risasi za moto zilizojeruhi wananchi kadhaa na kuuwa wengine bila hatia.

Kimsingi yaliyotokea hapo ni mengi na mengine yameandikwa katika vyombo vya habari na hatuna haja ya kuyarudia hapa.

Je, kwanini chadema walikuwa arusha kwa wakati huo?

Baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana wananchi wa mkoa wa Arusha walichagua viongozi wengi wa upinzani kuliko Chama Cha Mapinduzi (CCM); kwa matokeo hayo, walikuwa na haki ya kuchagua Meya na uongozi wa halmashauri ya jiji la Arusha.

Hata hivyo, kwa baraka za makao makuu ya CCM na serikali ya Jakaya Kikwete, madiwani wa CCM mkoani Arusha walikutana peke yao wakiwa na viongozi wa kiserikali Arusha na kufanya mapinduzi kama ya Gbogbo wa Ivory Coast.

Katika mkutano huo, wakajichagulia Meya kutoka CCM na wakampachika diwani wa Tanzania Labour Party (TLP) cheo cha naibu meya bila ridhaa yake.

CHADEMA wakalaani hatua hiyo na kukataa kumtambau Meya huyo. Wakataka kufanyika mkutano wa pamoja na serikali kujadiliana suala hilo ili uchaguzi mpya wa halali na unaoendana na kanuni ufanyike. Serikali ya CCM imekataa ombi hilo.

Kutokana na hali hiyo, CHADEMA wakaamua kuitisha mkutano na maandamano kwa mara ya kwanza 18 Desemba 2010.

Hata hivyo, baada ya mashauriano na polisi hatimaye chama chetu kilifuta mpango wake huo na kuandika barua kuitaka serikali kutatua tatizo hilo ndani ya kipindi cha wiki mbili.

Ni muhimu ikaeleweka kwamba ni haki ya kikatiba ya CHADEMA kulalamika na kuwaeleza wananchi wa Arusha juu ya mgogoro huu, na kwamba mkutano wa hadhara jijini Arusha ulilenga kujadili hali ya kisiasa iliyoibuka na kuzaa mgogoro huo.

Ni kwa sababu, mgogoro huu unawahusu sana wao, unazungumzia uchaguzi wa viongozi wao na hatua ya CCM na serikali yake kutumia nguvu kuchukua madaraka ya wananchi wa mkoa wa Arusha kihalali.

Msimamo wa serikali na maana yake kwa taifa.

Katika hotuba yake ya kufunga mwaka rais Kikwete alisema uchaguzi umekwisha na eti shughuli zozote za siasa za sasa, ni za watu binafsi kwa maslahi yao binafsi. Alitoa wito kwa vyombo vya dola kuhakikisha vinazuia shughuli za siasa zinazozuia maendeleo.

Vilevile, Rais Kikwete alitoa taarifa kuwa ataunda tume ya kuangalia upya katiba ya nchi.

Rais alikemea maandamano katika siku chache baada ya maandamano ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Tangazo la CHADEMA na lile la Shirikisho la Vyama huru vya wafanyakazi nchini (TUCTA) kutaka kuandamana kupinga bei mpya ya umeme nchini.

Sisi tunaamini kuwa matukio yaliyotokea Arusha ni maagizo ya CCM na serikali ya Rais Kikwete kutumia polisi kulazimisha CCM kupora Umeya na uongozi wa Jiji la Arusha.

Msimamo huo wa CCM na serikali yake siyo kwa Jiji la Arusha tu ila na nchi nzima. Kwa kitendo cha Arusha, CCM hawatakuwa tayari kuachia madaraka hata wakishindwa kihalali katika sanduku la kura.

Watanzania waelewe kuwa ifikapo mwaka 2015 CHADEMA kina uhakika wa kushinda uchaguzi mkuu; haya yanayotokea Arusha ni maandalizi ya kupora ushindi kwa nguvu.

Kufuatia hali hii, CHADEMA inasema yafuatayo:

Kwanza, vurugu za Arusha za tarehe 5 Januari 2011 zimesababishwa na jeshi la polisi kwa maagizo ya Chama Cha Mapinduzi na Serikali ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete.

Pili, tunatoa wito kwa Watanzania kukataa mpango mzima wa CCM kukataa kuachia madaraka hata pale wanaposhindwa kwa kura halali za wananchi, kama ilivyotokea Arusha, na kwingineko, na kama itakavyokuwa mwaka 2015.

Tatu, vurugu za Arusha ni ushahidi wa wazi zaidi juu ya umuhimu wa kuandikwa kwa Katiba Mpya itakayodhibiti madaraka ya rais na chama kinachotawala.

Katiba itakayoainisha kwa uwazi zaidi kuwa madaraka ya rais kama Amiri Jeshi Mkuu siyo kuamrisha majeshi dhidi ya wananchi wake, bali ni kulinda haki za wananchi na mipaka ya nchi yetu.

Nne, CHADEMA siyo chama cha msimu kwa ajili uchaguzi, ni chama cha siasa kitakachotetea haki za Watanzania kila siku, kila wiki, kila mwezi na kwa miaka yote.

Nia yetu ni kupanua na kuboresha demokrasia katika nchi yetu. CHADEMA hakitatulia hadi siku Watanzania watakaposema hawaonewi na viongozi wao, hawaibiwi na viongozi wao mpaka watakapoheshimiwa na kuhudumiwa na viongozi wao.

Kwa hiyo kazi ya kisiasa za CHADEMA kama mikutano ya hadhara, maandamano na shughuli zingine zitaendelea nchi nzima.

Tano, CHADEMA kinalaani mauaji ya wananchi  wasiokuwa na hatia, kinalaani kujeruhiwa kwa wananchi ambao hawakuwa na hatia, na kinalaani kukamatwa kwa viongozi wake mkoani Arusha. Tunatoa wito kuachiwa mara moja na bila masharti, vingenevyo tutaitisha maandamano nchi nzima kushinikiza kuachiwa huru.

Sita, Pamoja na kutumia njia za mazungumzo na majadiliano bungeni na kimtandao, CHADEMA  kitaendelea kutumia na njia zingine za kidemokrasia na za haki za msingi za kikatiba kama maandamano katika kuunganisha nguvu ya umma katika kulinda haki na kutetea maendeleo.

Hivyo, pamoja na yaliyojiri Arusha bado azima ya kuandamana kuhusu kupanda kwa bei ya umeme katika kipindi hiki hiki ambapo serikali inakusudia kulipa kifisadi kampuni ya Dowans ipo pale pale.

Mwisho CHADEMA inasisitiza kuwa yote haya yamefanyika kutokana na maelekezo ya hotuba ya rais Kikwete ya kufunga mwaka.

Tunakumbusha kuwa hayo ni matumizi mabaya ya madaraka; na hayawezi kukubalika. Rais Kikwete ameruhusu matumizi makubwa yasiyo na lazima kutumiwa na jeshi la polisi na kusababisha mali nyingi kuharibika.

Hivyo basi, tunatoa wito kwa wananchi na jumuiya ya kimatifa kulaani hatua hiyo ya Kikwete kutumia jeshi la polisi kushambulia viongozi wakuu wa CHADEMA na wafuasi wao; na tunaomba vitendo vya namna hii, vikomeshwe mara moja.

Tunatoa wito kwa waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha, naibu waziri, Balozi Khamisi Kagasheki na Ispkta Jenerali wa Polisi (IGP), Said Mwema kuwajibika kwa kujiuzulu kutokana na maafa yaliyotokea ambapo mpaka sasa imeripotiwa kuwa watu watatu wamefariki dunia kutokana na kushambuliwa kwa risasi na polisi.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: