TANESCO 'wachomoa' umeme Kipawa


Editha Majura's picture

Na Editha Majura - Imechapwa 20 January 2010

Printer-friendly version

MAKAZI ya Kipawa ambayo serikali inataka yahamishwe ili kupisha upanuzi wa uwanja wa ndege wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam hayakaliki tena. Hakuna umeme, na maji hayapatikani.

Umeme umekuwa shida kwa sababu mzalishaji na msambazaji mkuu wa huduma hiyo nchini, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), amebadilisha transfoma.

TANESCO limeondoa transfoma ya uwezo wa Kilovoti 200 iliyokuwa ikisambaza umeme eneo hilo na kuweka yenye uwezo wa Kilovoti 100. Ni dhahiri umeme unaopatikana ni mdogo usiotosheleza mahitaji ya wakazi.

Kwa sababu hakuna umeme wa kutosha, maji nayo hayapatikani. Chanzo cha maji yanayotumiwa na wakazi wa Kipawa ni visima ambavyo vinahitaji pampu kusukuma maji. Pampu hufanya kazi kwa umeme.

Wakazi wenyewe sasa wanaamini yanayowasibu ni njama za makusudi za serikali katika kuwashinikiza wahame. Wakazi waliopinga malipo ya fidia ndio waliopo eneo hilo.

Eneo la Kipawa lilizuiwa na serikali kuendelezwa ili kutekeleza mpango wa upanuzi wa uwanja wa ndege wa Mwalimu Nyerere. Tathmini ya mali za wakazi ilifanywa mwaka 1997.

Lakini malipo ya fidia yaliyochukua miaka 11, yalianza kulipwa Agosti mwaka jana yakizingatia Sheria ya Ardhi ya Mwaka 1967. Wakazi hao walipinga lakini baadhi wamepokea fidia. Waliogoma walifungua kesi Mahakama Kuu wakipinga kutumika kwa sheria hiyo.

Badala yake wakaitaka mahakama iamuru malipo hayo yafanywe kwa kuzingatia marekebisho ya sheria hiyohiyo yaliyofanywa mwaka 1999 na kuanza kutumika mwaka 2002.

Kesi hiyo inayowahusu wakazi 343 ilifutwa na Mahakama Kuu ya Ardhi kwa maelezo kuwa ni dhaifu. Mwenyekiti wa Kamati ya wakazi hao, Magnus Mulisa anasema wameshakata rufaa kwenye Mahakama ya Rufaa.

Wakati hatima ya kesi yao ingali kitendawili, maisha yao yameanza kuwa ya tabu. Wakati wenzao waliopokea malipo ya fidia wamekuwa wakivunja wenyewe nyumba na kuhamisha mali zao, wale 343 wanahaha kwani hali ya mazingira hairuhusu maisha kuendelea hapo.

Wenyewe wanasema “maisha ni magumu sana kwa sababu hatupati maji maana pampu haziwezi kusukuma maji kutoka visimani kwa kuwa hakuna umeme. Usalama wa maisha na mali zetu upo hatarini.”

Hawawezi kubaki Kipawa lakini kwa sababu bado wana kesi yao mahakamani, pia hawawezi kuachia nyumba na mali zao zipotee mikononi mwa wahuni. Wameamua kulinda mali zao kwa mbinu wakati wakiwa wameshahamisha familia zao kwa ndugu na wasamaria.

Sasa kila usiku unapoingia, wakazi hao wanalazimika kurudi Kipawa kulinda nyumba na mali zao dhidi ya wanaowaita wahuni ambao wamekuwa wakitega na kutafuta mwanya wa kuvamia na kuwaibia.

Yaliyobaki ni masikitiko kama anavyosema Mulisa, “Hakuna anayetusikiliza.” Walimfuata Afisa Tawala Wilaya ya Ilala awasaidie lakini majibu yakawa, “Serikali haihusiki wala hatuna taarifa hizo na kwa sababu tunawajibika kulinda usalama wa raia na mali zao, naahidi kushughulikia tatizo hilo ili kufahamu kinachoendelea.”

Mkuu wa Wilaya, Evance Balama anasema serikali haina mkono katika matatizo yanayowasibu wakazi wa Kipawa kwa sasa. Anasema TANESCO ni shirika linaloendesha shughuli zake kibiashara na “inashangaza kupoteza wateja wake kwa masuala yasiyolihusu.”

Anasema serikali haiwezi kufanya uhuni kwa wananchi. Wale waliokubali kulipwa fidia watahama kwa utaratibu unaoeleweka ila waliokataa, bado serikali inasubiri mkondo wa mahakama umalizike.

Meneja wa TANESCO Mkoa wa Ilala, Richard Nsulau anakiri “Tumebadilisha transfoma iliyokuwa ikisambaza umeme Kipawa na kuweka nyingine.” Anakana madai kuwa wameshinikizwa na serikali.

Kwanini wameondoa transfoma yenye uwezo mkubwa wakaweka ndogo? Nsulau anasema “Transfoma ya uwezo wa kilovoti 315 iliyokuwa Kariakoo imeharibika. Hatukuwa na transfoma ya akiba ya uwezo kama huo bali tuzonazo zenye uwezo wa kilovoti 100. Tulipofuatilia zaidi tukakuta transfoma iliyokuwa Kipawa ina kilovoti 200 kwa hiyo lazima ibadilishwe maana hatukuwa na jinsi.”

Anadai kumbukumbu zinaonyesha wateja halali Kipawa matumizi yao yanatosheleza transfoma ya kilovoti 100 “Ndiyo tukaifunga hiyo.”

Nsulau anasema hawajapokea malalamiko yoyote kutoka kwa wateja baada ya ubadilishaji transfoma ya awali. Lakini alikuwa na nyongeza, “Idadi kubwa ya wakazi hao ni wadaiwa sugu.”

Nimefanikiwa kupata nyaraka zinazoonyesha wateja 224 wanaodaiwa ankara za thamani ya Sh. 1,118,479,077.61 (Sh. 1.1 bilioni), akiwepo mteja anayedaiwa peke yake Sh. 38 milioni na mwenye deni dogo kabisa ni Sh. 861,625.30.

Nsulau anadai wateja hao ni wasumbufu mno kwani huwapiga mawe mafundi wa TANESCO wanapokwenda kukata umeme. “Hata wakifanikiwa kukata umeme, wakazi hao wanajiunganishia tena.”

Anahitimisha kwa kulalamika kuwa shirika haliwezi kukua endapo wateja wanalihujumu.

0
No votes yet